Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uhaba wa chanjo ya kipindupindu wasitisha mkakati wa dozi mbili- WHO

Watoto wakipatiwa chanjo dhidi ya kipindupindu katika wilaya ya Dondo nchini Msumbiji.
UN
Watoto wakipatiwa chanjo dhidi ya kipindupindu katika wilaya ya Dondo nchini Msumbiji.

Uhaba wa chanjo ya kipindupindu wasitisha mkakati wa dozi mbili- WHO

Afya

Kundi la kimataifa la kuratibu usambazaji wa chanjo nyakati za dharura, ICG limeamua kusitisha kwa muda mkakati wa utoaji wa dozi mbili za chanjo dhidi ya ugonjwa wa kipindupindu kutokana na hofu ya uwezekano wa uhaba wa chanjo hiyo.

Taarifa iliyotolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO huko Geneva, Uswisi imesema sitisho hilo ni kwa dunia nzima na badala yake mwelekeo sasa utakuwa ni dozi moja tu.

Taarifa hiyo imesema uamuzi huo utawezesha chanjo zilizopo kutumika katika nchi nyingi zaidi wakati huu ambapo idadi ya nchi zinazoripoti ugonjwa wa kipindupindu inaongezeka.

Kasi ya milipuko ya kipindupindu imeongezeka

Tangu mwezi Januari mwaka huu, nchi 29 zimeripoti ugonjwa wa kipindupindu zikiwemo Haiti, Malawi na Syria ambako mlipuko ni mkubwa zaidi.

WHO inasema ikilinganisha na miaka mitano iliyopita, nchi zilizokuwa zimeripoti mlipuko wa kipindupindu zilikuwa 20.

Shirika hilo linasema mwelekeo ni kuweko kwa milipuko zaidi kutokana na mafuriko, ukame, mapigano, mienendo ya watu kuhamahama na vigezo vingine ambavyo vinakwamisha watu kupata huduma ya majisafi na salama na hivyo kuongezeka hatari ya milipuko ya kipindupindu.

Mtoto kutoka Mtedera Zambia akipweza chanjo ya kipindupindu
Picha ya Gavi Alliance/Duncan Graham-Rowe
Mtoto kutoka Mtedera Zambia akipweza chanjo ya kipindupindu

Dozi moja ni bora kuliko kukosa dozi kabisa

Mkakati wa dozi moja umeonekana kuwa fanisi kwenye kukabili milipuko ingawa bado kuna Ushahidi kidogo kuhusu kipindi cha kinga iwapo mtu atapatiwa dozi moja na kinga inakuwa ni kidogo zaidi kwa mtoto.

Kupitia dozi mbili, dozi ya pili inapotolewa ndani ya kipindi cha miezi 6 baada ya dozi ya kwanza, kinga dhidi ya maambukizi inakuwa kwa kipindi cha miaka 3.

Hata hivyo WHO inasema faida ya dozi moja bado inazidi ile ya kutokuwa na chanjo kabisa na kwamba sitisho la sasa la dozi mbili litasababisha kupungua kwa muda wa kinga mwilini dhidi ya kipindupindu.

Hata hivyo ICG imesema itaendelea kufuatilia mienendo ya milipuko ya magonjwa pamoja na hali ya akiba ya chanjo dhidi ya kipindupindu na itakuwa inatathmini uamuzi wake kila wakati.