Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukosefu wa mazoezi ya mwili kichocheo cha utipwatipwa: WHO

Watoto wakimbizi kutoka Sudan Kusini wakicheza kuruka kamba katika makazi ya wakimbizi ya Palabek Ogili nchini Uganda
© UNICEF/Jimmy Adriko
Watoto wakimbizi kutoka Sudan Kusini wakicheza kuruka kamba katika makazi ya wakimbizi ya Palabek Ogili nchini Uganda

Ukosefu wa mazoezi ya mwili kichocheo cha utipwatipwa: WHO

Afya

 

Katika kipindi cha miaka 10 kuanzia mwaka 2020 mpaka mwaka 2030 inakadiriwa watu milioni 500 watakuwa wameugua magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo Kisukari, utipwatipwa na magonjwa ya moyo kutokana na kutofanya mazoezi ya mwili, imesema ripoti iliyotolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ulimwenguni WHO. 

Ongezeko la wagonjwa wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza ni hasara kubwa kwa uchumi wa kila serikali. Inakadiriwa kuwa serikali zitaingia gharama ya dola bilioni 27 kila mwaka kutibu wagonjwa wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza na kufikia mwaka 2030 takriban dola bilioni 300 zitakuwa zimetumika kutibu wagonjwa hao.

Gharama hii kubwa imeainishwa katika ripoti iliyotolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ulimwenguni WHO ambalo katika utafiti walioshirikisha nchi 194 kuhusu kufanya mazoezi ya mwili na namna serikali zinavyohamasisha wananchi wake kushirika katika mazoezi hayo, wamegundua kiujumla kuna maendeleo kidogo sana kwenye kampeni za uhamasishaji wananchi kufanya mazoezi ambayo matokeo yake ni kuzuia magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama vile utipwatipwa, kisukari na magonjwa ya moyo na hivyo serikali kujipunguzia mzigo wa kuwahudumia wagonjwa hao.

Tatizo la utipwatipwa ni kubwa sana nchini Marekani na linahusishwa na lishe isiyo bora
UNICEF/Toutounji
Tatizo la utipwatipwa ni kubwa sana nchini Marekani na linahusishwa na lishe isiyo bora

Chonde chonde serikali na wadau

Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema baada ya kutolewa ripoti hii wanaamini mataifa na wadau watachukua hatua kwakuwa lengo lao ni kuona wananchi wanahamasishwa kufanya mazoezi sababu tatizo linazidi kuwa kubwa.

Dkt Tedros amesema “Tunahitaji kuona nchi nyingi zinaongeza na kutekeleza sera za kusaidia wananchi kushirika zaidi katika mazoezi kwa kutembea, kuendesha baiskeli na kushiriki kwenye michezo mingine mingi ya kimwili. Faida ni kubwa si tu kwa afya ya mwili bali kiakili na jamii nzima itanufaika, mazingira yatakuwa bora na kiuchumi pia.”

Takwimu walizokusanya zinaonesha kuwa duniani kote chini ya asilimia 50 ya nchi zina será za kitaifa za kufanya mazoezi ya mwili na kati ya hizo ni asilimia 40 ndio zinazofanya kazi. Na kama hiyo haitoshi ni asilimia 30 pekee ya nchi zenye será ndio zimeweka miongozi ya namna ya kutekeleza sera hizo.

WHO imesema ingawa karibu nchi zote zinaripoti kuwa na mfumo wa kufuatilia shughuli za kimwili kwa watu wazima, asilimia 75 ya nchi hufuatilia shughuli za kimwili kwa vijana, na chini ya asilimia 30 hufuatilia iwapo watoto chini ya miaka 5 wanafanya mazoezi ya mwili au lah.

Watoto wakiwa nje ya madarasa yao wakicheza sehemu za Curaçao, Uholanzi.
Photo: UNICEF/Roger LeMoyne
Watoto wakiwa nje ya madarasa yao wakicheza sehemu za Curaçao, Uholanzi.

Je WHO inafanya nini katika kusaidia mataifa kutoka katika hali ya wananchi wake kuwa tipwatipwa?

WHO limekumbusha nchi kuhakikisha zinatekeleza mpango wa utekelezaji wa ufanyaji mazoezi ya viungio au GAPPA ya mwaka 2018-2030 ambayo imeweka mapendekezo ya sera 20 miongoni mwazo ni kuhamasisha mataifa kutengeneza barabra zilizo salama kwa watu kufanya mazoezi  na kutoa fursa za kufanya mazoezi katika maeneo kama vituo vya malezi ya watoto, mashuleni na mahala pa kazi.

Kiujumla ripoti hiyo inatoa wito kwa nchi kuweka kipaumbele katika shughuli za mazoezi ya kimwili kama jambo muhimu katika kuboresha afya na kukabiliana na magonjwa yasiyo ya kuambukizwa katika sera zote muhimu, na kuweka kanuni, miongozo na kutoa mafunzo ili kuhakikisha zinatekelezwa kwa ufanisi kwa manufaa ya mataifa yao.