Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bado kuna uwekezaji mdogo kwenye sekta ya afya ya umma- Katibu Mkuu UN

Mgonjwa akimeza dawa ya Malaria nchiin Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC. Mfumo wa TRVST unatarajiwa kusambaa na kusaidia kuthibitisha ubora, viwango na ufanisi wa dawa na chanjo.
UNICEF/UN0Gwenn Dubourthoumieu
Mgonjwa akimeza dawa ya Malaria nchiin Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC. Mfumo wa TRVST unatarajiwa kusambaa na kusaidia kuthibitisha ubora, viwango na ufanisi wa dawa na chanjo.

Bado kuna uwekezaji mdogo kwenye sekta ya afya ya umma- Katibu Mkuu UN

Afya

Mkutano wa viongozi wa dunia kuhusu afya umefunguliwa hii leo huko Berlin nchini Ujerumani ambako Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres ameelezea wasiwasi wake juu ya uwekezaji mdogo kwenye mifumo inayotakiwa kwa ajili ya afya na ustawi wa wakazi duniani.

Katika hotuba yake aliyoitoa kwa njia ya video, Katibu Mkuu amesema kiasi kidogo sana cha fedha kinawekezwa duniani kwenye mifumo yenye wajibu wa kuhakikisha afya na ustawi wa wakazi wa dunia.

Janga la COVID-19 limefichua udhaifu

Amesema uwekezaji mdogo umejidhihirisha wazi kwani “tunaishi katika zama za hatari kubwa na ukosefu wa uhakika. Mataifa na jamii bado zinahaha kujikwamua kutoka madhara makubwa ya janga la COVID-19,” amesema Guterres.

Janga la COVID-19 limedhihirisha ni kwa kiasi gani hatujajiandaa kukabili majanga. Wanawake wameathirika zaidi. “Wanabeba mzigo mkubwa unaoongezeka kwa huduma na malezi kwenye familia na pia kama wahudumu wa afya mstari wa mbele.”

Guterres amesema na wakati huo huo, wanawake wengi wamekumbwa na punguzo la kipato kutokana na kupoteza ajira zao au kutokuweko kwa mifumo ya  hifadhi ya jamii.

Utashi wa kisiasa unahitajika kuleta mabadiliko

Katibu Mkuu anasema hali ya sasa lazima ibadilike kwa kuwa mfumo wa fedha duniani usio na mizania unaangusha nchi zinazoendelea kwa sababu serikali zao zinahitaji msaada kutoka jamii ya kimataifa kupatia kipaumbele suala la afya.

Amesisitiza kuwa suala la afya duniani na kujiandaa kukabili majanga vinapaswa kuimarishwa kupitia utashi endelevu wa kisiasa na uongozi, na hili linahitaji serikali kupatia afya kipaumbele.

Tweet URL

Na wakati huo huo nchi tajiri na taasisi za fedha za kimataifa zinahitajika kusaidia nchi zinazoendelea kutekeleza uwekezaji huo kwenye afya.

Afya ya mwili na akili viende pamoja

Katibu Mkuu amekumbusha kuwa watu wote wanahitaji huduma ya afya jumuishi, isiyoegemea upande wowote na wanayoweza kuipata kupitia Mpango wa huduma ya afya kwa wote.

Amesema katika zama za sasa za matatizo makubwa na kiwewe “tunapaswa kuhakikisha kuwa afya ya akili haipuuzwi katika suala zima la afya.”

Ameongeza kuwa afya ya mwili na akili ni msingi wa jamii zenye amani na endelevu na hivyo ametamatisha hotuba yake kwa kuwatakia washiriki mkutano wenye tija ambao utaibuka na hatua za kuwezesha huduma ya afya kwa wote.

Kuhusu WHS2022

Hii ni mara ya  kwanza kwa WHO kuwa muaandaaji mwenza wa mkutano huu wa viongozi kuhusu afya ambapo mwaka huu unaandaliwa kwa pamoja baina ya WHO na serikali ya Ujerumani, Ufaransa na Senegal.

Zaidi ya wazungumzaji 300 wanatarajiwa kuzungumza wakitoka katika kanda zote za WHO duniani, na kati yao hao ni wataalamu zaidi ya 40 wa WHO ambao watashirikisha ufahamu, maoni na dira yao kuhusu masuala ya afya duniani.

Mkutano huu wa afya wa viongozi unalenga kuimarisha mabadilishano ya taarifa, kuchochea ubunifu na ugunduzi wa miundombinu ya afya na kitababu na kuweka hoja ya suala la afya kama moja ya vipaumbele vya kisiasa sambamba na kusongesha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.

Unaweza kufuatilia mkutano huo moja kwa moja hapa.