Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatari ya baa la njaa duniani: Tuna uwezo wa kubadili mwelekeo- Guterres

FAO inasaidia uzalishaji wa chakula jimboni Cabo Delgado nchini Msumbiji
FAO
FAO inasaidia uzalishaji wa chakula jimboni Cabo Delgado nchini Msumbiji

Hatari ya baa la njaa duniani: Tuna uwezo wa kubadili mwelekeo- Guterres

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Ikiwa leo ni siku ya chakula duniani, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema maadhimisho ya mwaka huu yanafanyika wakati dunia inakabiliwa na janga kubwa la uhakika wa kupata chakula.

Amesema ni janga kwa sababu idadi ya watu wanaokabiliwa na njaa imeongezeka maradufu katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.

Takribani watu milioni moja wanaishi kwenye mazingira ya baa la njaa, ambako kukosa chakula na kifo ni jambo la kawaida kila uchao.

Kama hiyo haitoshi watu bilioni 3 hawana uwezo wa kupata mlo wenye lishe bora, ikimaanisha wako hatarini kukumbwa na utapiamlo au utipwatipwa.

“Jamii zilizo hatarini zaidi zinakabiliwa na janga la COVID-19, madhara ya mabadiliko ya tabianchi, uharibifu wa mazingira, mizozo na kuzidi kuongezeka kwa kiwango cha ukosefu wa usawa,” amesema Katibu Mkuu,

Amesema vita nchini Ukraine imechochea kasi ya ongezeko la bei ya vyakula, nishati na mbolea.

Wengine wakikosa chakula, wengine wanatupa, kama inavyoonekana pichani katika soko moja nchini Uganda. Hii ni changamoto siyo tu kwa wauzaji wa vyakula bali pia wakulima na walaji
© FAO/Sumy Sadurni
Wengine wakikosa chakula, wengine wanatupa, kama inavyoonekana pichani katika soko moja nchini Uganda. Hii ni changamoto siyo tu kwa wauzaji wa vyakula bali pia wakulima na walaji

Tunaweza kubadili mwelekeo

Katibu Mkuu hajapoteza matumaini akisema, lakini tunaweza kubadili mwelekeo iwapo tutashirikiana.

Anasema hivyo akitambua kuwa duniani kuna chakula cha kumtosha kila mtu mwaka huu. “Lakini wakulima wanahitaji kupata haraka mbolea katika gharama nafuu ili tuhakikishe mwakani tuna chakula cha kutosha,” amesema Guterres.

Hakuna wa kuachwa nyuma: uzalishaji bora, lishe bora, mazingira bora, maisha bora

Akirejelea ujumbe wa mwaka huu wa siku ya chakula duniani, Hakuna wa kuachwa nyuma: uzalishaji bora, lishe bora, mazingira bora, maisha bora, Katibu Mkuu amesema serikali, wanasayansi, sekta binafsi, mashirika ya kiraia wanapaswa kushirikiana ili mlo wenye lishe bora uweze kupatikana kwa kila mtu, na kila mtu aweze kuumudu.

“Taasisi za fedha zinapaswa kuongeza usaidizi wao kwa ncih zinazoendelea ili ziweze kusaidia watu wao na kuwekeza katika mifumo ya chakula.”

Ametamatisha akisema “kwa pamoja tunaweza kusonga kutoka kwenye kukata tamaa hadi kwenye matumaini. Katika siku hii ya chakula duniani natoa wito kwako uwe sehemu ya mabadiliko.”

Kuhusu siku ya chakula duniani

Siku ya chakula duniani imeanza kuadhimishwa mwaka 1981 kufuatia azimio namba A/RES/35/70 la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lililopitishwa tarehe 5 mwezi Desemba mwaka 1980.

Na ilichaguliwa tarehe 16 Oktoba kwa kuwa ni tarehe ambayo mwaka 1945 lilianzishwa shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo FAO, lenye makao yake makuu mjini Roma, Italia.