Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vijana kesho yetu ni bora kuliko leo – Balozi wa vijana EAC

Jessica Mshama, Balozi wa Vijana wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, (kulia) akihojiwa na Flora Nducha wa  Idhaa ya Kiswahili ya  Umoja wa Mataifa.
UN/ Assumpta Massoi
Jessica Mshama, Balozi wa Vijana wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, (kulia) akihojiwa na Flora Nducha wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa.

Vijana kesho yetu ni bora kuliko leo – Balozi wa vijana EAC

Utamaduni na Elimu

Balozi wa vijana wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, EAC, Jessica Mshama ambaye hivi karibuni alishiriki mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu marekebisho ya elimu kwenye Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani, amesema ujumbe wake kwa vijana ni kwamba “kesho yetu ni bora kuliko jana.”

Bi. Mshama amesema hayo wakati akihojiwa na Flora Nducha wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa na akiongeza hata hivyo  wafanye kazi kwa bidii bila kukata tamaa.

Vijana tusikate tamaa lakini tujielimisha kila uchao

Pamoja na kutokata tamaa amesema ni muhimu wajielimishe “katika kila iitwapo leo” kwa sababu dunia inakwenda kwa mabadiliko ya kasi na “sisi lazima tujikite katika kuendeleza kupata elimu iliyo bora ili kufikia malengo yetu.”

Balozi huyu wa vijana wa EAC ambaye pia ni Msimamizi na Mkurugenzi wa shule ya kidijitali iitwayo Assumpter Digital School alipoulizwa kile ambacho kimemgusa zaidi kwenye suala la elimu, amesema ni kiu aliyo nayo kila uchao ya kuona ni vipi “sisi kama vijana tunaweza kushirikiana na vile vile sisi na taasisi za kimataifa ili kuboresha mfumo wa elimu. Kama tunavyojua elimu ni chachu ya maendeleo, kwa hiyo vijana wakipata elimu iliyo bora inayoendana na muda na kasi ya sasa hivi  tunayo nafasi kubwa ya kuwa chachu ya maendeleo ya taifa letu.”

Kuna nuru ya elimu bora siku zijazo

Bi. Mshama akaenda mbali zaidi kuelezea kile ambacho anaondoka nacho baada ya kushiriki mkutano huo ulioleta viongozi wa nchi na serikali, wawakilishi wa mashirika ya kimataifa, vijana na wadau mbali,  akitaja ni suala la elimu kutokuwa na mifumo inayoendana na wakati wa sasa, jambo alilogundua kuwa ni tatizo la nchi nyingi na linakumba vijana wengi.

Kwa hivyo basi, “kufika hapa kuonana na viongozi ambao wameshiriki kwenye vikao vya kuboresha mfumo wa elimu duniani kote, ni faraja kwetu sisi vijana na pia kwa sekta ya elimu kwa ujumla kwamba sasa hivi mifumo ya elimu yetu itarekebishwa kulingana na dunia inavyoendana lakini pia soko la ajira ambalo vijana wanategemea hapo baadaye,” amefafanua Jessica.

Akirejea Afrika Mashariki ni uchechemuzi upi atafanya?

Bi. Mshama anasema pendekezo lake kwa nchi za Afrika Mashariki ni kwamba mfumo wa elimu uwe na elimu ya ziada. “Si tu elimu ya kufaulu mitihani darasani, bali elimu yetu ihusishe elimu ya fedha kuanzia elimu ya awali kwa watoto. Elimu ya kujitegemea, elimu ya kuhusu hali ya hewa, wakati huu ambapo hali ya hewa inaleta majanga duniani kote.”

Ametamatisha akisema elimu hiyo ihusishe hali halisi ya ulimwengu.