Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Madagascar yatakiwa kukomesha imani potofu dhidi ya watu wenye ualbino

Mwanamke huyu akipita eneo kavu lenye mchanga mwingi huko Kusini mwa Madascar baada ya kujipatia mgao wa chakula kutoka WFP
© WFP/Tsiory Andriantsoarana
Mwanamke huyu akipita eneo kavu lenye mchanga mwingi huko Kusini mwa Madascar baada ya kujipatia mgao wa chakula kutoka WFP

Madagascar yatakiwa kukomesha imani potofu dhidi ya watu wenye ualbino

Haki za binadamu

Mtaalamu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya ualbino ametoa wito wa kuchukuliwa hatua za haraka ili kukabiliana na mashambulizi dhidi ya watu wenye ualbino ikiwa ni pamoja na mauaji na ukeketaji, ambayo yanaongezeka nchini Madagascar wakati huu ambapo imani potofu na umaskini ukizidi kushamiri.

Walengwa wakubwa wa matukio hayo ni watoto.

Kupitia taarifa iliyotolewa kwa waandishi wa habari jijini Geneva Uswisi, Mtaalamu Huru wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Ualbino, Muluka-Anne Miti -Drummond amesema "Imani potofu na ushirikina kwamba macho ya watu wenye ualbino yanaweza kuleta bahati nzuri na utajiri vimeanzisha mashambulizi yanayolenga zaidi watoto katika eneo la kusini mwa nchi hiyo, ambako umaskini umekithiri," alisema.

Mtaalumu hiyo ambaye alifanya ziara ya siku 10 nchini Magadascar katika siku za hivi karibuni, ameeleza kuwa watu wenye ualbino, katika maeneo hayo wamekuwa wakiishi kwa hofu ya kudumu na wengine kuamua kuwachukua watoto wao na kuwaacha katika vituo vya polisi na vituo vingine kwa ajili ya kupatiwa ulinzi.

Serikali itoe elimu

Umoja wa Mataifa umeishauri serikali ya Madagascar kuanzisha kampeni nchi nzima za kuelimisha na kuongeza uelewa wa kukabiliana na imani potofu, imani za kishirikina na kutoelewa kuhusu ualbino.

Taarifa za kati ya mwaka 2020 na mwaka 2022 kutoka vyombo vya usalama viliripoti takriban kesi 45 ambazo ni pamoja na utekaji nyara, ukeketaji na mauaji.

Mashambulizi ya mwaka 2022 yameongezeka maradufu ikilinganishwa na 2021. Ndani ya mwezi mmoja mashambulio manne yamerekodiwa ambayo waathiriwa ni pamoja na mtoto wa miezi tisa.

"Shambulio lingine liliripotiwa kwangu siku chache zilizopita, likisisitiza hitaji la ulinzi wa haraka, thabiti kwa watu wenye ualbino, haswa katika mikoa ya mbali, ambayo umaskini umekidhiri," Miti-Drummond alisema.

Tatizo ni umasikini

Katika ziara yake nchini Magadascar Mtaalamu huyo alitembelea jamii maskini huko Fort Dauphin, Ambovombe na Amoboasary.

Akielezea alicho shuhudia maeneo hayo alisema eneo la kusini limeathiriwa zaidi na mabadiliko ya tabianchi na limekumbwa na ukame, vimbunga, uhaba mkubwa wa chakula na ukosefu wa usalama unaosababishwa na wezi wa mifugo wanaojulikana kama dahalo.

"coronavirus">COVID-19 imeongeza umaskini zaidi na hii imetoa msingi mzuri wa imani hizi hatari potofu kuzidi kuenea na kudhihirika katika mashambulizi na mazoea mengine mabaya kwa matumaini ya kupata utajiri," Miti-Drummond alisema.

Kipindi cha siasa nacho kinaongeza uhalifu kwa watu wenye ualbino, "Mashambulizi pia yanasemekana kuongezeka kabla ya uchaguzi, na ninaomba kuwa macho kwa kuzingatia uchaguzi unaosubiri mwaka ujao." Alitoa angalizo.

Wanaokamatwa na kuhukumiwa ni wachache sana

Mtaalam huyo pia alikuwa na wasiwasi juu ya kiwango cha chini cha hukumu. "Ninafahamu hukumu mbili pekee katika kesi nilizopokea na hakuna hata moja ya uhalifu mbaya zaidi kama vile ukeketaji na mauaji. “

Alisema mbinu moja wapo ya kuhakikisha tabia hii inakomeshwa ni wahusika lazima wafikishwe mahakamani ili kuepusha dhana za kutoadhibiwa ambazo zinaweza kusababisha watu kujichukulia hatua mkononi.

Watu wengi wenye ualbino wanazuiwa kupata ajira yenye maeneo mazuri zaidi na kupata elimu ya kutosha kutokana na unyanyapaa na ubaguzi. Kupata mafuta ya kuzuia jua kama bidhaa ya kuokoa maisha pia ni ghali sana kwa wengi.

Mtaalamu huyo alipongeza kuundwa kwa kamati ya kitaalamu ya hali ya juu kuhusu ualbino ambayo inalenga kuandaa mpango kazi wa kitaifa.

Utafiti na uchambuzi wa nchi nzima wa watu wenye ualbino pia umepangwa kufanyika.

Miti-Drummond atawasilisha ripoti ya kina kuhusu ziara yake katika Baraza la Haki za Kibinadamu mnamo Machi 2023.