Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mlinda Amani wa Umoja wa Mataifa auwawa nchini DRC

Wakimbizi kutoka Burundi wakichota maji katika kambi ya Lusenda, Kivu Kusini, Jamhuri ya Kidemkrasia ya Congo, DRC.
UNHCR/Colin Delfosse
Wakimbizi kutoka Burundi wakichota maji katika kambi ya Lusenda, Kivu Kusini, Jamhuri ya Kidemkrasia ya Congo, DRC.

Mlinda Amani wa Umoja wa Mataifa auwawa nchini DRC

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani shambulio lililotokea hapo jana tarehe 30 Septemba 2022 nchini Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo DRC katika kambi ya COB iliyopo chini ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini humo, MONUSCO na kusababisha kifo cha mlinda amani mmoja raia wa Pakistan.

Taarifa iliyotolewa leo na Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric jijini New York Marekani imesema shambulio hilo lililotokea Katika jimbo la Kivu Kusini limeshukiwa kutekelezwa na kikundi cha wapiganaji wa Twirwaneho.

“Katibu Mkuu ametuma salamu za rambirambi kwa familia ya mlinda amani aliyefariki dunia na kwa Serikali na watu wa Pakistan.” Amesema Dujarric na kuongeza kuwa “Katibu Mkuu anakumbusha kuwa mashambulizi dhidi ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa yanaweza kuwa uhalifu wa kivita chini ya sheria za kimataifa. Anatoa wito kwa mamlaka ya DRC kuchunguza tukio hilo na kuwafikisha haraka wale waliohusika mbele ya sheria.”

Amehitimisha taarifa yake kwa kusema Katibu Mkuu anasisitiza tena kwamba Umoja wa Mataifa kupitia Mwakilishi wake Maalum katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ( Bintou Keita) utaendelea kuiunga mkono Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo na wananchi wake katika juhudi zao za kuleta amani na utulivu mashariki mwa nchi hiyo.