Juhudi za kikanda kwa amani DRC ziwe za dhati, zisidumaze amani- UN
Hii leo wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wamepatiwa Ripoti ya Katibu Mkuu wa Umoja huo na kujulishwa kuwa kasi ya ongezeko la idadi ya wakimbizi nchi humo ambayo sasa imefikia milioni 5.5 ni kiashiria ya kwamba hali ya usalama inazidi kudorora kila uchao.
Ripoti hiyo ya Katibu Mkuu ya matukio ya kati ya tarehe 17 Juni mwaka huu hadi tarehe 16 mwezi huu wa Septemba imewasilishwa na Mwakilishi wake Maalum nchini DRC, Bintou Keita ambaye pia ni Mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini humo MONUSCO.
Ripoti imemulika hali ya usalama, kisiasa, haki za binadamu na utoaji wa misaada ya kibinadamu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC pamoja na usaidizi wa kimkakati wa kuimarisha taasisi.
Kuibuka upya kwa M23 kuliibua chuki dhidi ya MONUSCO
Mathalani kuhusu amani na usalama, Guterres amesema vikundi vilivyojihami vimeendelea kuwa tishio kubwa na vinatekeleza ukatili dhidi ya raia.
“Vitendo vingi vya ukatili vinatekelezwa na vikundi vya CODEDO, ADF na M23 kwenye majimbo ya Ituri na Kivu Kaskazini, ilhali kikundi cha Mai-Mai na vinginevyo vinaimarisha mashambulizi yake jimboni Kivu Kusini.”
Amesema ukosefu wa usalama umechochea ukiukwaji wa haki za binadamu na kuongeza idadi ya wahitaji wa misaada ya kibinadamu ambapo “takribani watu milioni 27 wanahitaji misaada na wengi msaada wa ulinzi.”
Amefafanua kuwa kuibuka upya kwa mashambulizi yanayofanywa na M23 kumeibua janga la wananchi wa Mashariki mwa DRC kukosa imani na majukumu ya MONUSCO.
Juhudi za kikanda ziwe za dhati zichagize amani
Hata hivyo ameshukuru juhudi zinazoendelea za kusaka suluhu ya kudumu. “Ushiriki wa dhati wa wadau wa kikanda unasalia mazingira ya msingi ya amani ya kudumu na utulivu Mashariki mwa DRC,” amesema Guterres kwenye ripoti hiyo huku akitanabaisha kuwa “ni vyema kwa wadau wa kikanda kuzingatia kwa dhati wajibu wao wa kujiepusha na vitendo vyovyote vinavyoweza kudumaza amani au mamlaka ya mipaka ya nchi.”
Amepongeza michakato ya mazungumzo kati ya Rais Etienne-Antoine Tshisekedi wa DRC na Paul Kagame wa Rwanda; yale yanayoratibiwa na Rais João Lourenço, wa Angola, pamoja na ya hivi karibuni kando ya UNGA77 yaliyoongozwa na Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa.
Ametaja pia mchakato wa Nairobi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki unaoongozwa na Rais wa zamani wa Kenya ,Uhuru Kenyatta.
Kuhusu mpango wa EAC kupeleka jeshi la kikanda DRC, Katibu Mkuu amesema “kwa kuzingatia ugumu wa hali iliyoko mashariki mwa DRC, uratibu wa karibu wa MONUSCO na jeshi la kikanda la EAC, pindi litakapopelekewa, utakuwa ni muhimu ili hata wakati operesheni za kijeshi dhidi ya vikundi vilivyojihami, zikiendelea, ulinzi wa raia uwepo, misaada ya kibinadamu iweze kufikishwa, halikadhalika ufuatialiaji wa haki za binadamu.
Vikundi vilivyojihami vimegeuza msitu wa Congo kuwa makao yao makuu- Angaza Institute
wa mkutano huo, Emery Mudinga ambaye ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Angaza inayohusika na uhifadhi wa misitu nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC alizungumzia madhara ya uwepo wa vikundi vilivyojihami mashariki mwa nchi hiyo ambako wamegeuza eneo hilo kuwa makao yao makuu.
“Vikundi hivi vilivyojihami vinakata miti na kuchimba madini kiholela na kuuza kinyume chas heria. Ukataji misitu holela kunaathiri upatikanaji wa mvua, chakula na hata mbinu za kipato mashariki mwa DRC, halikadhalika hata shughuli za utalii zimekwama kutokana na ukosefu wa usalama,” amesema Bwana Mudinga.
Ametoa mapendekezo kadhaa kwa wajumbe wa Baraza ikiwemo kuwezesha DRC kuwa na jeshi linaloweza kudhoofisha nguvu za vikundi. Halikadhalika kufadhili miradi na barabara kwenye maeneo ya misitu ili kuweza kufuatilia vitendo haramu vinavyofanywa na vikundi vilivyojihami.