Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mpango wa Urusi kutaka kutwaa maeneo ya Ukraine ni kinyume na Chata ya UN

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akizungumza na waandishi wa habari 29 Septemba 2022 kuhusu mpango wa Urusi kutaka kutwaa maeneo ya Ukraine
UN/ Mark Garten
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akizungumza na waandishi wa habari 29 Septemba 2022 kuhusu mpango wa Urusi kutaka kutwaa maeneo ya Ukraine

Mpango wa Urusi kutaka kutwaa maeneo ya Ukraine ni kinyume na Chata ya UN

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres leo amezungumza na waandishi wa habari jijini New York, Marekani akisema Urusi lazima isitishe sherehe yake iliyopanga kufanya kesho ya uzinduzi wa mchakato wa kutwaa majimbo ya Ukraine ya Donetsk, Luhansk, Kherson na Zaporizhzhia.

Bwana Guterres amesema mpango huo wa Urusi ni kinyume na Chata ya Umoja wa Mataifa, hakina uhalali wowote  kisheria na kinapaswa kulaaniwa.

“Katika zama hizi za vitisho, lazima nisisitiza jukumu langu kama Katibu Mkuu la kutetea Chata ya Umoja wa Mataifa,” amesema Katibu Mkuu akiongeza kuwa Chata hiyo iko wazi na dhahiri.

Kitendo cha ardhi ya taifa moja kutwaliwa na taifa lingine kwa vitisho au kwa matumizi ya nguvu ni ukiukwaji wa misingi ya Chata ya Umoja wa Mataifa na sheria ya kimataifa.

Guterres amenukuu pia Azimio la Kirafiki la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa la tarehe 24 Oktoba mwaka 1970 ambalo limetaja kanuni na sheria za kimataifa za Mahakama ya Kimataifa ya Haki.

Baraza hilo Kuu lilitangaza kuwa eneo la nchi halipaswi kuwa kifaa cha kutwaliwa na nchi nyingine kwa misingi ya tishio au nguvu na kwamba hakuna utwaaji wa eneo la nchi ambao utatambuliwa kisheria.

Kitendo cha kutwaa majimbo hayo kilaaniwe

Katibu Mkuu amesema hilo lazima lieleweke na kwamba Urusi ikiwa moja ya nchi zenye ujumbe wa kudumu kwenye Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa linashikiri wajibu wa kuheshimu Chata ya Umoja wa Mataifa.

Katibu Mkuu amesema kitendo chochote cha Urusi kutwaa majimbo ya Ukraine lazima kilaaniwe.

Ni kinyume na mifumo ya kisheria ya kimataifa. Ni kinyume na kila kitu ambacho jumuiya ya kimataifa inatetea. Kinakiuka Malengo na Misingi ya Umoja wa Mataifa na ni hatari kwa kuwa kitaendeleza vurugu.

Guterres amesisitiza kuwa “utwaaji eneo la nchi nyingine hauna nafasi kwenye dunia ya sasa na katu haikubaliki.

Msimamo wa UN

Msimamo wa Umoja wa Mataifa ni wazi: Tumeazimia kwenye kulinda mamlaka ya taifa, umoja, uhuru na eneo la mipaka ya Ukraine ndani ya mipaka inayotambulika kimataifa, kwa mujibu wa maazimio husika ya Umoja wa Mataifa.

Kura ya maoni haina mashiko

Katibu Mkuu amesisitiza kuwa kile kinachodaiwa kuwa ‘kura ya maoni’ iliyoendeshwa na Urusi kwenye maeneo yanayokaliwa  iliendeshwa wakati vita inaendelea, kwenye maeneo ambayo yanakaliwa na Urusi, na nje ya mfumo wa kikakatiba na kisheria wa Ukraine.

“Huo hauwezi kuitwa kuwa utashi halisi wa walio wengi,” amesema Katibu Mkuu akiongeza kuwa “uamuzi wowote utakaochukuliwa na Urusi kuendelea na shughuli hiyo utaharibu zaidi matumaini ya amani.”

Amesema hatua hiyo itaongeza madhara zaidi kwenye uchumi wa dunia hasa kwa nchi zinazoendelea na “kukwamisha uwezo wetu wa kupeleka misaada ya kuokoa maisha Ukraine na maeneo mengine.”

Guterres amesema ni wakati sasa kubadili uamuzi huo ili kuepusha janga zaidi akiongeza kuwa, “sasa kuliko wakati wowote tunapaswa kufanya kazi pamoja kumaliza vita hii isiyo na maana na kuzingatia Chata ya Umoja wa Mataifa na sheria ya kimataifa.”