Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Elimu sio ufunguo wa maisha tu ni msingi wa maendeleo:UN 

Wanafunzi wakishiriki katika mpango wa elimu katika kituo cha Kashonjwa nchini Uganda
© UNICEF/ Zahara Abdul
Wanafunzi wakishiriki katika mpango wa elimu katika kituo cha Kashonjwa nchini Uganda

Elimu sio ufunguo wa maisha tu ni msingi wa maendeleo:UN 

Utamaduni na Elimu

Elimu ni nguzo muhimu katika jamii na ndio ufunguo wa maisha. Ili kuleta usawa katika jamii, juhudi nyingi zimeongezwa kasi ili bidhaa hiyo iwafikie watoto na vijana wa jinsia zote mbili kwa mujibu wa ripoti ya karibuni iliyotolewa na mashirika ya Umoja wa Mataifa japo imetoa angalizo kwamba maeneo ya vijijini bado yamesalia nyuma hata baada ya harakati kuimarishwa. 

Ripoti hiyo ya pamoja ya shirika la umoja wa mataifa la elimu na utamaduni, UNESCO na lile la kuhudumia watoto UNICEF na wadau iliyotokana na utafiti imebaini kuwa idadi ya watu wasiojua kusoma na kuandika ilipungua kwa milioni 7.7 katika kipindi cha miaka 10 iliyopita. 

Vijini bado kuna changamoto 

Hali katika maeneo ya vijijini bado ni mbaya imeongeza ripoti hiyo kwani asilimia 12.8% ya vijana na watu wazima bado hawajui kusoma na kuandika. 

Hata hivyo, idadi ya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano wanaosajiliwa shuleni imeongezeka hasa katika maeneo ya vijijini na kwenye familia za walio masikini imeendelea kusema ripoti hiyo. 

Watoto wakiwa wameketi kimduara na mwalimu wao katika kituo cha awali cha maendeleo ya mtoto kwenye kijiiji cha Garin Badjini, kusini-mashariki mwa Nigeria
© UNICEF/Giacomo Pirozzi
Watoto wakiwa wameketi kimduara na mwalimu wao katika kituo cha awali cha maendeleo ya mtoto kwenye kijiiji cha Garin Badjini, kusini-mashariki mwa Nigeria

Katika kipindi cha mwaka 2015 na 2020, idadi ya wanafunzi wanaohitimu sekondari iliongezeka kwa 2.1%. 

Centrine Wanjala ni msichana wa miaka 20 na alifanikiwa kusoma baada ya kupata ufadhili wa shirika la kijamii la Zinduka lililoko eneo la Kehancha kaunti ya Migori na anasimulia kuwa,”Zinduka ilinifadhili kwa kila haja niliyokuwa nayo kuanzia mahitaji ya shuleni na hata ya nyumbani na binafsi. Nimefanikiwa kumaliza shule kwasababu ya juhudi hizo.Wazazi wangu walitatizika kunitimizia niliyoyahitaji lakini wasamaria walinishika mkono.” 

COVID-19 imeongeza changamoto 

Ripoti ya tume ya Umoja wa mataifa ya maeneo ya Amerika ya Kusini na Caribbea, ECLAC, imebaini kuwa idadi ya watoto wasioenda shule ya msingi na sekondari haikubadilika kutokea mwaka 2015 hadi 2020. 

Wakati janga la corona lilipoutikisa ulimwengu, kiasi ya watoto milioni 10.4 na vijana walishindwa kupata elimu. 

Juma Tsunusi ni mwalimu kutokea Vanga na anaelezea kuwa,”Mchango wa wazazi katika kuhakikisha watoto wanasoma ni kuwaunga mkono kwa hali zote.Wanafunzi wanahitaji uelekezi kila wakati na pia nasaha kutoka kwa walimu maana wakati mwengine akili zao zinatapatapa.” 

Mlo shuleni ni muhimu hususan kwa watoto maskinia
WFP/Sierra Leone
Mlo shuleni ni muhimu hususan kwa watoto maskinia

Utafiti wa UNESCO na UNICEF 

Harakati za kupanua wigo wa vyuo anuwai zimewashirikisha wanafunzi milioni 17 katika kipindi cha miaka 20 iliyopita hazijakuwa na usawa katika maeneo yote.Maeneo ya vijijini yameachwa nyuma. 

Philomena Mwilu ni naibu jaji mkuu wa Kenya na anaamini kuwa suluhu ni kuwapa nguvu watoto katika hatua za msingi na anasisitiza kuwa “Bila watoto hatuna jamii au kizazi kijacho.Ni muhimu kulinda maslahi ya watoto kuanzia hatua za mwanzo ili kuwalinda na kuwaepusha kuingia kwenye ndoa za utotoni zinazosababisha mimba zisizotakikana.Inaumiza sana kuona watoto wanajivuruga na mambo kama hayo kadhalika mila zilizopitwa na wakati.” Utafiti huo wa UNESCO na UNICEF unaashiria kuwa idadi ya wanawake wanaosajiliwa kwa masomo ya vyuo anuwai na vile vikuu lifikia asilimia 61.7% kwa wanawake na asilimia 46.8% kwa wanaume ilipofikia mwaka 2020.Mwaka 2000 idadi ya wanawake na wanaume wanaosajiliwa kwa masomo baada ya sekondari ilikuwa sawa.Rose Ghati ni mkaazi wa Kuria na anasubiri kupata stashahada yake na mtazamo wake ni kuwa “Maono yangu ni kuwasaidia hasa wasichana wa Kikuria kwani hawana uhuru wa kuwa na mawazo ya binafsi.Aghalabu kwetu sisi wanawake wa Kikuria tumeamini kazi zetu ni za ndani tu na hilo linatunyima nafasi ya kushiriki kwenye mipango ya maendeleo ya taifa.” 

Mpango wa mlo shuleni kwa hisani ya WFP hapa watoto wako kwenye kituo cha elimu Kibera, Kenya.
WFP/Challiss McDonough
Mpango wa mlo shuleni kwa hisani ya WFP hapa watoto wako kwenye kituo cha elimu Kibera, Kenya.

Ukielimisha mtoto wa kike umeelimisha jamii 

Ripoti ya UNESCO na UNICEF inazipa uzito harakati za kuimarisha elimu hasa ukizingatia athari za janga la corona. 

Kipindi hicho kiliwafanya wanafunzi kukosa kusoma kwani shule karibu zote zilifungwa. 

Mama Katharina James Mwita alifanikiwa kuwasomesha wanawe wa kike ijapokuwa jamii yake hailipi uzito suala hilo.Kwa sasa anakula matunda ya juhudi hizo kwani “Niliamua kuwasomesha wanangu wa kike japo wengi hawakuona faida yake wakati huo.Kwa sasa ninafurahia sana kwani wanangu wako sawa na wananisimamia kila nitakalo.Ukiwatazama walio na umri kama wangu, wameisha kabisa na maisha yamewashinda nguvu lakini mimi namshukuru Mola kwani ameniweka pazuri.Hata wajukuu wangu pia wananitazama kadri ya uwezo wao.” 

Kongamano la kubadili na kuimarisha mifumo ya elimu lililofanyika New York lilidhamiria kuiongeza kasi ya kutimiza lengo la 4 la malengo endelevu ya milenia ya umoja wa mataifa, SDGs.