Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Teknolojia mpya zibuniwe kupunguza uchafuzi wa mazingira utokanao na safari za majini

Meli ikipita katika sehemu ya mfereji wa Panama, moja ya njia zilizo na shughuli nyingi za biashara duniani.
UN News/Jing Zhang
Meli ikipita katika sehemu ya mfereji wa Panama, moja ya njia zilizo na shughuli nyingi za biashara duniani.

Teknolojia mpya zibuniwe kupunguza uchafuzi wa mazingira utokanao na safari za majini

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Ikiwa leo ni siku ya kimataifa ya usafirishaji bidhaa baharini, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema meli zitakazosafiri katika muongo huu zitatoa majibu iwapo sekta ya usafirishaji baharini imejipanga kutotoa hewa chafuzi ifikapo mwaka 2050 au la.

Guterres amesema hayo katika ujumbe wake wa siku hii ambayo maudhui yake ni teknolojia mpya kwa usafirishaji majini usiochafua mazingira.

Katibu Mkuu amesema “meli janja na zisizotoa kabisa hewa chafuzi lazima ziwe ndio chaguo la kawaida na ziwe zinapatikana kibiashara kwa watu wote ifikapo mwaka 2030.”

Amefafanua kuwa hatua hiyo ni muhimu kwa kuzingatia kuwa ujumbe wa mwaka huu unamulika umuhimu wa majawabu ya usafirishaji baharini endelevu, majawabu ambayo yatapunguza utoaji wa hewa chafuzi ikiwemo hewa ya ukaa, majawabu yatakayolinda mazingira na kuhakikisha kiwango cha joto hakizidi nyuzi joto 1.5 katika kipimo cha Selsiyasi kwa mujibu wa Mkataba wa Paris wa Mabadiliko ya Tabianchi.

Meli ya mizigo ikipakua makasha ya mizigo bandarini
IMO
Meli ya mizigo ikipakua makasha ya mizigo bandarini

Sekta ya usafirishaji majini ifanye nini?

Katibu Mkuu Guterres anasema sekta ya usafirishaji majini inapaswa iongeze kasi ya safari yake ya kupunguza utoaji hewa ya ukaa.

“Bila hatua za pamoja, kiwango cha hewa chafuzi kutoka katika sekta ya usafirishaji majini kinatarajiwa kuongezeka kwa asilimia 230 ifikapo mwaka 2050, ikiwa ni kiwango cha juu ikilinganishwa na kile cha mwaka 2008.

Kwa mantiki hiyo anataka serikali na sekta binafsi kufanya kazi pamoja kuibuka na teknolojia bunifu kama vile matumizi ya dijitali na utumiaji wa mitambo inayojiendesha yenyewe, sambamba na kuchagiza mpito wa haki wa kutumia nishati jadidifu, mpito ambao utajumuisha pia nchi zinazoendelea.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu usafirishaji majini huchangia zaidi ya asilimia 80 ya biashara duniani na kwamba vita ya Ukraine na Mkataba wa Bahari Nyeusi wa kusafirisha nafaka, “vimetumbusha jukumu muhimu la usafirishaji majini na lishe kwa dunia.

Meli zikiwa katika bandari ya Antwerp
Picha/ IMO
Meli zikiwa katika bandari ya Antwerp

Katibu Mkuu amesema “usafirishaji bidhaa kwa njia ya meli baharini unavyoendelea kuunganisha ubinadamu, vivyo hivyo unapaswa kuwa na dhima muhimu katika kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu na kujenga mustakabali wa haki na wenye ustawi kwa wakazi wote wa sayari dunia.”

Siku ya kimataifa ya usafirishaji baharini huadhimishwa kila alhamisi ya mwisho ya mwezi Septemba.