Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kichaa cha mbwa bado ni tishio licha ya kuweko kwa chanjo- WHO

Kuvunja maambukizi ya kichaa cha mbwa ni kupitia hatua kwa binadamu, wanyama na udongo.
Isabelle Roger/PAHO/WHO
Kuvunja maambukizi ya kichaa cha mbwa ni kupitia hatua kwa binadamu, wanyama na udongo.

Kichaa cha mbwa bado ni tishio licha ya kuweko kwa chanjo- WHO

Afya

Hii leo tarehe 28 mwezi Septemba ni siku ya kichaa cha mbwa duniani siku ambayo shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO linaitumia kuelimisha umma juu ya madhara ya ugonjwa huo ambao licha ya kuwa na kinga bado unasababisha vifo hususan barani Afrika na Asia.

WHO inasema waathirika wengi wa ugonjwa huo ambao mbwa ndio chanzo chake kikuu ni watoto katika jamii maskini kwenye mabara hayo.

 

Ujumbe wa mwaka huu ni “Kichaa cha mbwa:Afya moja, hakuna kifo,” ikimulika uhusiano wa mazingira na wanyama na binadamu.

WHO inasema program za kudhibiti kuenea kwa virusi aina ya Rabies vinavyosababisha ugonjwa wa kichaa cha mbwa, ni mfano bora wa utekelezaji wa mradi wa Afya moja na utokomezaji wa magonjwa yanayotoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu.

Shirika hilo linasema Afya Moja kwa kuwa tayari dunia ina chanjo, dawa, mbinu na teknolojia za kuvunja mzunguko wa ugonjwa huu ambao ni moja ya magonjwa ya zamani.

WHO inasema waathirika wengi wa ugonjwa huo ambao mbwa ndio chanzo chake kikuu ni watoto katika jamii maskini kwenye mabara hayo.

Takwimu zinasemaje?

Kichaa cha mbwa ni ugonjwa unaosababishwa na virusi aina ya Rabies, ingawa una chanjo bado unapatikana katika nchi na maeneo zaidiya 150 duniani.

Mbinu za kuzuia ugonjwa huo ni kupitia chanjo anayopatiwa mbwa, halikadhalika kuzuia mbwa wenyewe kung’ata binadamu.

Maambukizi ya kichaa cha mbwa husababisha vifo vya makumi ya maelfu ya watu kila mwaka hususan Asia na Afrika.

Dola bilioni 8.6 hupotea kila mwaka kutokana na ugonjwa wa kichaa cha mbwa: ikiwa ni matibabu, hasara ya nguvu kazi inayopotea.

Asilimia 40 ya watu wanaong’atwa na wanyama wanaosambaza ugonjwa huo wakiwemo mbwa ni watoto wenye umri wa chini ya miaka 15.

Maambukizi ya kichaa cha mbwa

WHO inasema ugonjwa wa kichaa cha mbwa huambukizwa kwa kungatwa na mnyama aliyebeba virusi hivyo viitwavyo #Rabies.

Barani Amerika, popo nao wanatajwa kuwa chanzo kikuu cha maambukizi ya ugonjwa huo kwa kuwa maambukizi yanayosababishwa na mbwa yamedhibitiwa kwenye eneo hili.

Maambukizi kutoka kwa mnyama kwenda kwa binadamu yanaweza kutokea pia iwapo mnyama mwenye virusi hivyo atagusana na kidonda kibichi cha binadamu.

Maambukizi kutoka kwa binadamu mwenye virusi hivyo kwenda kwa binadamu mwingine kwa njia ya mate yaonekana kuwa inawezekana lakibi bado haijathibitishwa.

Nchini Laos, daktari akifunika sindano tayari kutupa sindano hiyo aliyotumia kumdunga mtoto wa kiume aliyeng'atwa na mbwa na kuambukizwa virusi vya Rabies vinavyosababisha kichaa cha mbwa.
UNICEF/Jim Holmes
Nchini Laos, daktari akifunika sindano tayari kutupa sindano hiyo aliyotumia kumdunga mtoto wa kiume aliyeng'atwa na mbwa na kuambukizwa virusi vya Rabies vinavyosababisha kichaa cha mbwa.

Dalili za kuwa umeambukizwa kichaa cha mbwa

WHO inasema kipindi cha virusi kushamiri mwili na dalili kuanza kuonekana ni kati ya miezi 2 hadi 3 lakin inaweza kuwa hata wiki moja hadi mwaka mmoja kulingana na vigezo mbalimbali ikiwemo ni eneo gani virusi vimeingilia mwilini na kiwango chake.

Dalili ni pamoja na homa ikiambatana na maumivu au mtekenyo mwilini usioelezeka na kwenye kidonda mtu anapata hisia kama za kuungua. Kadri virusi vinasambaa kwenye mfumo wa fahamu mwilini, vivyo hivyo uvimbe kwenye ubongo na uti wa mgongo.

Hatua za kuchukua ung’atwapo na mbwa

Hata hivyo WHO inasema kitendo cha kusafisha jeraha kwa kutumia maji na sabuni ni muhimu na kinaweza kuokoa maisha.

Halikadhalika matibabu hospitalini ikiwemo kudungwa sindano, PEP, kwa mujibu wa viwango vinavyotambulika ili kuzuia virusi kuingia mfumo wa fahamu wa mwili wa binadamu.

WHO inasema inashirikisha sekta mtambuka na kuchukua hatua kama vile kuelimisha jamii kuhusu ugonjwa huo sambamba na kampeni za chanjo kwa mbwa.

Kwa sasa WHO inaongoza kampeni iitwayo “Muungano dhidi ya Kichaa cha Mbwa,” kampeni ambayo inachagiza maendeleo ya kutokomeza vifo vya binadamu vitokanavyo na kichaa cha mbwa ifikapo mwaka 2030.