Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sekta ya Utalii yazidi kuimarisha duniani kote

Utalii endelevu hunufaisha mazingira, uchumi na jamii husika
© Unsplash/Beth Macdonald
Utalii endelevu hunufaisha mazingira, uchumi na jamii husika

Sekta ya Utalii yazidi kuimarisha duniani kote

Ukuaji wa Kiuchumi

Leo ni siku ya utalii duniani na ulimwengu uko kwenye mwelekeo mzuri katika sekta ya utalii ikilinganishwa na miaka miwili iliyopita kufuatia janga la COVID-19.

unKwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii UNWTO sekta ya utalii inazidi kuimarika na taarifa za kuanzia mwezi Januari mpaka mwezi julai mwaka huu 2022 zinaonesha idadi ya watalii kimataifa iliongezeka mara tatu sawa na asilimia 172 ikilinganishwa na kipindi hicho hicho mwaka jana 2021.

Ongezeko la idadi hii ya watalii inamaanisha kuwa sekta hii ya utalii imeimarika kwa asilimia 60 ikilinganishwa na kipindi cha kabla ya janga la COVID-19.

Katibu Mkuu wa UN atoa tahadhari

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika ujumbe wake wa siku hii amekumbusha na kutoa tahadhari kuwa utalii ufanyike vyema kwa kujali utunzaji wa mazingira, sayari dunia na kulinda asili pamoja kukuza uelewa wa kitamaduni.

“Utalii ni kichocheo kikubwa cha maendeleo endelevu. Unachangia elimu na uwezeshaji wa wanawake na vijana na kuendeleza maendeleo ya kijamii na kiutamaduni ya jamii. Utalii unachukua sehemu muhimu katika mifumo ya ulinzi wa kijamii ambayo inaunda msingi wa uthabiti na ustawi.” Amesema Guterres

Mkuu huyo wa UN amesema wakati huu utalii ukizidi kuimarika duniani kote ni lazima serikali na wafanyabiashara kuwekeza katika utalii safi na endelevu, kupunguza matumizi ya nishati, kupunguza uchafuzi wa hewa na kulinda bayoanuwai.

Hifadhi zinachukua hatua kukabiliana na COVID-19 na kuhakikisha utalii salama.Simba katika hifadhi ya Masai Mara nchini Kenya
UNEP GRID Arendal/Peter Prokosch
Hifadhi zinachukua hatua kukabiliana na COVID-19 na kuhakikisha utalii salama.Simba katika hifadhi ya Masai Mara nchini Kenya

“Ni lazima tutengeneze nafasi za kazi zenye staha na kuhakikisha faida inanufaisha nchi mwenyeji na jumuiya za ndani ya nchi hizo. Serikali,wafanyabiashara na watalii lazima zilinganishe desturi za wenyeji  za utalii na Malengo ya Maendeleo Endelevu na pia kuwaza kuhakikisha viwango vya joto vya 1.5°C. Uhai wa sekta hii na maeneo mengi ya watalii, kama vile Nchi Zinazoendelea za Visiwa Vidogo, inategemea hilo.” Alisisitiza.

Alieleza kuwa wakati huu ambao sekta ya utalii ukiimarisha ndio wakati wa muafaka kufikira upya ‘na kuunda upya utalii na kwa pamoja wahusika wote wa utalii wakishirikiana basi wataweza kuleta mustakabali endelevu zaidi, wenye mafanikio na uthabiti kwa wote.

Nini kimeimarisha utalii duniani?

Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii duniani  UNWTO miongoni mwa vivutio vya ongezeko la watalii ni kupungua kwa vizuizi vya usafiri.

Mpaka kufikia tarehe 19 Septemba 2022 nchi 86 hazikuwa kabisa na vikwazo vinavyohusiana na COVID-19. Hii imechangia ongezeko kubwa la mahitaji ya usafiri kimataifa.

Katibu Mkuu wa UNWTO Zurab Pololikashvili naye kwenye taarifa yake amesema pamoja na utalii kuendelea kuimarika kwa kasi, lakini changamoto kadhaa zimesalia “kutoka kwenye siasa za kijiografia hadi za kiuchumi. Sekta ya utalii inarudisha matumaini na fursa kwa watu kila mahali. Sasa ni wakati wa kufikiria upya utalii, unakokwenda na jinsi unavyoathiri watu na sayari.”

Kupata taarifa zaidi kuhusu sekta hii ya utalii, kufahamu nchi gani zimeimarika kwa kiwango , kufahamu sekta gani za biashara zimeimarika zaidi, kufahamu viwango vya ukuaji kwa kuzingatia ukanda na pia ujumbe wa shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii na mipango yao ya baadaye bofya hapa.