Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Katibu Mkuu UN atoa wito wa kukomeshwa kwa 'vitisho vya nyuklia'  

Sanamu la Wema waushinda Ubaya - kwenye uwanja wa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, iliyowasilishwa kwa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Kisovieti wakati wa maadhimisho ya miaka 45 ya UN.
UN Photo/Manuel Elías
Sanamu la Wema waushinda Ubaya - kwenye uwanja wa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, iliyowasilishwa kwa Umoja wa Mataifa na Umoja wa Kisovieti wakati wa maadhimisho ya miaka 45 ya UN.

Katibu Mkuu UN atoa wito wa kukomeshwa kwa 'vitisho vya nyuklia'  

Amani na Usalama

Katika enzi ya "vitisho vya nyuklia", Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres siku ya Jumatatu alizitaka nchi kuondokana na tishio la maafa ya kimataifa wajitolee  tena kwa amani. 

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ameyaasema hayo hii leo alipokuwa akizungumza katika hafla ya kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kutokomeza Kabisa Silaha za Nyuklia, hafla iliyofanyika huku mjadala wa kila mwaka wa Baraza kuu ukifikia ukomo katika Ukumbi wa Baraza Kuu. 

"Silaha za nyuklia ndizo nguvu za uharibifu zaidi kuwahi kuundwa. Hazileti usalama wowote , ni mauaji na machafuko tu. Kuondolewa kwazo kungekuwa zawadi kuu tunayoweza kutoa kwa vizazi vijavyo.” amesema. 

Bwana Guterres alikuwa akiwahutubia viongozi wa dunia, mawaziri wa mambo ya nje, maafisa wengine wakuu wa serikali na mashirika ya kiraia waliokusanyika katika Baraza la Udhamini kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York. 

Guterres amekumbushia kwamba Vita Baridi ilileta wanadamu “ndani ya dakika chache za maangamizi.” Hata hivyo miongo kadhaa baada ya kumalizika, na kuanguka kwa Ukuta wa Berlin, "tunaweza kusikia tena mlio  nyuklia."  

“Niweke wazi. Enzi ya vitisho vya nyuklia lazima iishe. Wazo la kwamba nchi yoyote inaweza kupigana na kushinda vita vya nyuklia limepotoshwa. Utumiaji wowote wa silaha ya nyuklia zahma. Tunatakiwa kurudi nyuma.” Amesema Guterres 

Maono na ahadi mpya  

Bwana Guterres amesisitiza haja ya kuwa na maono mapya ya kutokomeza silaha za nyuklia akiashiria Ajenda yake Mpya ya Amani. Ajenda yake mpya inatoa wito wa kupokonya silaha na kuendeleza uelewa wa pamoja wa vitisho vingi vinavyoikabili jumuiya ya kimataifa. 

"Tunahitaji kuzingatia utaratibu wa nyuklia unaoendelea, ikiwa ni pamoja na aina zote za silaha za nyuklia na njia zao za usambazaji. Na tunahitaji kushughulikia mistari yenye ukungu kati ya silaha za kimkakati na za kawaida, na uhusiano na nyanja mpya za mtandao na anga za juu. " Amesisitiza Guteres 

Wakati mjadala wa Baraza Kuu ukimalizika, Katibu Mkuu ametoa wito kwa nchi wanachama kuondoka New York na dhamira mpya ya kufanya kazi kwa mustakabali wa amani na akaongeza kusema, “bila ya kuondoa silaha za nyuklia, hakuwezi kuwa na amani. Hakuwezi kuwa na uaminifu. Na hakuwezi kuwa na mustakabali endelevu.”