Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwelekeo wa Mkataba wa Amani Sudan Kusini utupiwe jicho

Familia iliyotawanywa ikiondoka katika kambi ya ulinzi wa raia ya Umoja wa Mataifa mjini Juba kurejea nyumbani kwao Jonglei Sudan Kusini
UN Photo/Isaac Billy
Familia iliyotawanywa ikiondoka katika kambi ya ulinzi wa raia ya Umoja wa Mataifa mjini Juba kurejea nyumbani kwao Jonglei Sudan Kusini

Mwelekeo wa Mkataba wa Amani Sudan Kusini utupiwe jicho

Haki za binadamu

Jumuiya ya kimataifa inapaswa kuangazia zaidi na kwa mwelekeo wa mkataba wa amani Sudan Kusini pamoja na ongezeko la ghasia miongoni mwa jamii nchini kote Sudan Kusini, wameonya wataalamu wa Umoja wa Mataifa wa haki za binadamu nchini humo baada ya kuhitimisha ziara yao jijini New York, Marekani ambako wamepata fursa ya kuzungumza na maafisa mbalimbali.

Taarifa ya ofisi ya Umoja wa Mataifa ya haki za binadamu iliyotolewa leo jijini Juba Sudan Kusini na Geneva, Uswisi imemnukuu Yasmini Sooka ambaye ni Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Mataifa ya haki za binadamu Sudan Kusini akisema wakati wa ziara yao jijini New York, wamezungumza na maafisa wa Umoja wa Mataifa ili kuwafikishia ujumbe  ya kwamba ni muhimu kwa wahisani na nchi wanachama kuendelea kufuatilia mkataba mpya wa amani wa mwaka 2018, marekebisho ya sekta ya ulinzi na kuhakikisha sheria ya katiba inapitishwa kabla ya uchaguzi.

Bi. Sooka amesema bila hatua hizo, kuna uwezekano wa kuona mamilioni ya wakimbizi wa ndani Sudan Kusini au wengine wakivuka mipaka na kusababisha ghasia kwa nchi Jirani na kwa mashirika ya misaada.

Kipindi cha mpito chasogezwa mbele kwa miaka miwili

Tarehe 4 mwezi uliopita wa Agosti, pande husika kwenye mkataba wa mwaka 2018 walitia saini kuongezwa kwa miaka miwili zaidi kwa kipindi cha mpito na kusogeza mbele uchaguzi hadi mwishoni mwa mwaka 2024.

Hadi sasa, muundo wa mfumo wa uchaguzi haujabainishwa, hali kadhalika licha ya uchaguzi kuhitaji mazingira rafiki, raia wa Sudan Kusini wanaojaribu kuhoji serikali au wanaofichua vitendo vya ukatili wanapata vitisho vya kuuawa, wanaswekwa korokoroni, wanateswa huku fursa za kisiasa zikizidi kubinywa.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa Mkataba wa Amani ulijumuisha mchakato wa mashauriano ya kitaifa na kuanzishwa kwa Tume ya Ukweli, Maridhiano na Uponyaji.

Mashauriano yalifanyika katikati yam waka huu lakini yaliengua maeneo yaliyo chini ya upinzani pamoja na mamilioni ya wakimbizi ambao walikimbia kutokana na hofu ya maisha yao.

Hakuna chombo cha haki kilichoanzishwa

Na katika miaka minne, hakuna chombo hata kimoja kati ya vitatu vilivyopendekezwa kwa ajili ya usimamizi wa haki ambacho kimeundwa: Kamisheni ya Ukweli, Maridhiano na Uponyaji, Mahakama na Mamlaka ya fidia.

Kamishna Barney Afako amesema “huwezi kuengua kwenye mfumo ujao wa haki, idadi kubwa ya watu ambao wameathirika. Na pia huwezi kuchagua kimoja kati ya vyombo vya haki, vyote vinapaswa kufanya kazi pamoja ili kuletea hitimisho wananchi wa Sudan Kusini.”