Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Elimu bora ni 'tofali' la jengo bora la amani, utulivu na maendeleo- Katibu Mkuu UN

Wanafunzi wakiwa darasani wilaya ya Kasese nchini Uganda.
© UNICEF/Maria Wamala
Wanafunzi wakiwa darasani wilaya ya Kasese nchini Uganda.

Elimu bora ni 'tofali' la jengo bora la amani, utulivu na maendeleo- Katibu Mkuu UN

Utamaduni na Elimu

Mkutano wa kimataifa wa marekebisho ya mfumo wa elimu ukiwa umeingia siku ya pili kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani hii leo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito kwa wahisani kuchangia fedha zaidi ili kukwamua sekta ya elimu ambayo sasa inakumbwa na changamoto lukuki hususan katika nchi zinazoendelea.

Guterres amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini New York, Marekani akiwa ameambatana na Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu elimu, Gordon Brown.

Guterres amesema “dunia inakabiliwa na majanga lukuki, serikali, sekta ya biashara na familia kila mahali zinakabiliwa na mahitaji makubwa ya fedha.”

Tangu kuanza kwa janga la COVID-19, amesema Katibu Mkuu, “theluthi mbili ya nchi duniani zimepunguza bajeti zao za elimu.”

Hata hivyo Katibu Mkuu amekumbusha kuwa elimu ni ‘tofali’ linalotumika kujenga jamii zenye amani, ustawi na utulivi.

Ameonya kuwa kupunguza uwekezaji kunatoa hakikisho la majanga zaidi siku za usoni.

Ni kwa mantiki hiyo amesema inahitajika fedha zaidi kwenye mifumo ya elimu na “si kupunguza bajeti.”

Tweet URL

Nani afanya nini?

Katibu Mkuu amesema nchi tajiri zinaweza kuongeza uwekezaji zaidi kutoka vyanzo vyao vya ndani vya fedha.

Kwa nchi zinazoendelea, amesema itakuwa ni changamoto kwa kuwa idadi kubwa zinakabiliwa na ongezeko kubwa la gharama yamaisha. “Hizi zinahitaji haraka usaidizi kwenye elimu.”

Hapo amesema ndipo inapoingia Mfuko wa kimataifa wa kufadhili elimu, IFFEd akisema hilo ndilo jukumu lake.

“Mfuko huu unalenga kufikisha nchi za vipato vya chini fedha, eneo ambako ndio kuna nusu ya watoto na vijana wote wa dunia, na idadi kubwa ya watoto wakimbizi,” amesema Guterres.

Katibu Mkuu amesema mfuko huo si kitu kipya, bali ni mfumo wa kuongeza rasilimali zilizo kwenye taasisi za kifedha ili zipeleke fedha kwa gharama ndogo ya elimu.

“Tunatarajia mfuko huo kukua na kuwa na dola bilioni 10 kwa ajili ya kufanikisha elimu ya kizazi cha kesho cha vijana,” amesema Katibu Mkuu.

Amesisitiza kuwa mfuko huo unafanya kazi pamoja na kuunga mkono mbinu zilizoko tayari kama vile Ubia wa Elimu duniani, GPE ambao unatoa fedha na misaada mbalimbali.

Ametumia fursa hiyo kumpongeza mjumbe maalum Bwana Brown na mataifa mengine na taasisi kwa kufanya kazi ili mfuko huo uweze kuanza kazi.

Tunajua la kufanya tuache sasa miradi ya majaribio

Katika siku hii ya pili, washiriki wa mkutano pamoja na wageni waliweza kupata fursa ya kukutana na kikaragosi Amal, ambacho kinawakilisha mamilioni ya watoto wakimbizi wanaoshindwa kupata elimu kutokana na mazingira waliyomo.

Miongoni mwa waliokutana naye ni Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina J, Mohammed.

Mapema Bi. Mohammed alihutubia mkutano huo wa marekebisho ya elimu uliolenga hii leo kusaka mawajabu ambako amesema, kinachohitajika ni uchangiaji bora wa fedha na “tunafahamu cha kufanya, hebu na tusianze tena mipango ya majaribio, tuchukue hatua.