Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatua zaidi zahitajika kuimarisha demokrasia jumuishi nchini Burundi- Mtaalamu

Wanawake Burudi wakitifua udongo kwa jembe katika maandalizi ya kupanda.
©FAO/Giulio Napolitano
Wanawake Burudi wakitifua udongo kwa jembe katika maandalizi ya kupanda.

Hatua zaidi zahitajika kuimarisha demokrasia jumuishi nchini Burundi- Mtaalamu

Haki za binadamu

Burundi lazima ichukue hatua zaidi kuimairisha demokrasia, utawala wa sheria na kutokomeza ukwepaji sheria dhidi ya matukio ya ukiukwaji wa haki na manyanyaso yaliyotekelezwa tangu mwaka 2015, amesema mtaalamu maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu nchini Burundi.

Katika ripoti yake aliyowasilisha leo kwenye Baraza la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu, mtaalamu huyo  Fortuné Gaétan Zongo, amesema licha ya ahadi na hatua zilizochukuliwa na serikali ya sasa, bado hali ya haki za binadamu nchini Burundi haijaimarika kiuendelevu.

Taarifa iliyotolewa na ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa jijini Geneva, Uswisi hii leo imemnukuu mtaalamu huyo akisema, ni muhimu na dharura zaidi kuanzisha marekebisho na mchakato jumuishi na halali wa kidemokrasia nchini Burundi ili kuepusha kutokea tena kwa ghasia zilizowahi kutokea.

Ikiwa ni mara yake ya kwanza kuhutubia Baraza hilo tangu kushika wadhifa huo,  Bwana Zongo amerejelea suala la uwajibikaji tangu ghasia za mwaka 2015 na kutoa wito wa marekebisho ya dhati ya kitaasisi.

Amesisitiza kuwa Burundi katika ripoti yake ya mapitio ya mapitio iliyowasilisha mwaka 2018 ilikubali mapendekezo ya kutokomeza ukwepaji sheria na kukubali kuanzisha mfumo wa wazi na wa haki wa mahakama kwa mujibu wa viwango vya kimataifa.

Kwa minajili hiyo, Mtaalamu huyo amependekeza kupitishwa kwa mikakati ya vipaumbele vya kukomesha ukiukwaji wa haki na kutoa fursa ya watu kulipwa fidia na kutekeleza mapendekezo mengine ikiwemo yale ya Kamisheni ya uchunguzi kuhusu haki za binadamu Burundi.

Kazi inafanyika lakini kuna madai ya upendeleo kwa wafikishwao mbele ya sheria

Ingawa hivyo ametambua hatua zilizochukuliwa na Burundi za kufungulia mashtaka watekelezaji wa vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu lakini ameeleza wasiwasi wake kuhusu uchaguzi wa matukio yanayochukuliwa hatua, mathalani upendeleo dhidi ya waliotekeleza makosa makubwa.

“Matukio machache ya malalamiko kuwa vitendo vya ukiukwaji mkubwa havijachunguzwa bila upendeleo, na hata kufunguliwa mashtaka au wahusika kuhukumiwa, hilo lenyewe ni ukiukwaji wa hatua ya kutibu,” amesema Bwana Zongo.

Kwa kutambua idadi ya kesi zinazosubiriwa kushughulikiwa na kikosi kazi kuhusu kutoweshwa kwa watu Burundi, Mtaalamu huyo amependekeza Burundi iridhie Mkataba wa Kimataifa dhidi ya kutoweshwa kwa watu.