Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto wangu wananiuliza Syria ni nini? Kambi ya Zaatar ikiingia muongo mwingine

Kambi ya wakimbizi ya Za'atari nchini Jordan inayoonekana kutoka juu ina wakimbizi kutoka Syria.
UN Photo/Mark Garten)
Kambi ya wakimbizi ya Za'atari nchini Jordan inayoonekana kutoka juu ina wakimbizi kutoka Syria.

Watoto wangu wananiuliza Syria ni nini? Kambi ya Zaatar ikiingia muongo mwingine

Wahamiaji na Wakimbizi

Mwaka 2022 ni  miaka 10 tangu kuanzishwa kwa kambi ya wakimbizi ya Za’atari nchini Jordan, kambi ambayo inasimamiwa na Umoja wa Mataifa. Ni kambi kubwa zaidi Mashariki ya Kati na moja ya kambi kubwa zaidi duniani ikiwa ni maskani ya wasyria 80,000. UN News au Habari za UN imezungumza na baadhi ya wakimbizi kuhusu maisha katika kambi hiyo, na matumaini yao kwa siku zijazo. 

Adil Tughan, mkimbizi wa Syria akiwa katika kambi ya wakimbizi ya Al Zaatari nchini Jordan

Adil Tughan aliwasili kambi ya Za’atari mwezi Aprili 2013, kutoka mji wa Al-Sanamayn katika mkoa wa Daraa kusini mwa Syria, pamoja na mke wake na watoto wawili wadogo. 

Tangu wakati huo, yeye na mke wake wamezaa watoto wengine watatu, ambao hawajui lolote kuhusu nchi yao ya Syria. 

“Familia yangu na mimi tumepitia mateso mengi tulipoondoka Syria. Tulivuka zaidi ya kituo kimoja cha ukaguzi na zaidi ya nchi moja. Kwa sasa hali ya maisha ni ni shwari, usalama na miundombinu pia viko sawa. Hali ya elimu ni bora  kwani kuna shule 32 kambini, vituo vya kijamii 58, na zahanati nane. Umeme unapatikana kwa saa nane kwa siku. Kuna mfumo wa maji taka na mfumo wa maji safi. Kuna barabara za lami na mfumo wa usafiri wa ndani. Tunataka watoto wetu wawe na maisha bora kuliko sisi, kwa upande wa elimu, masomo na kazi." 

Hakuna aliyekuja hapa kwa hiyari yake 

 

Ghasim Al-Lubbad, mkimbizi kutoka Syria akiwa kambini Zaatari nchini Jordan

Qassim Lubbad, kutoka mkoa wa Daraa, alikujanaye aliwasili kambini Zaatar  Mei 2013. Na hadi sasa hana matumaini kuhusu hali ya Syria. 

“Hakika hakuna aliyekuja hapa kwa kupenda kwake. Nilitoka Syria nikiwa na watoto watano na nimepata watoto wengine watatu hapa kambini. Kila mtu alikuja kwa sababu walilazimishwa kutafuta amani na usalama. Kulikuwa na mateso. Familia zilichukua njia tofauti. Tulitumia zaidi ya saa 72 kuhama kutoka kijiji kimoja hadi kingine hadi tulipofika  na mpaka na kuingia Jordani.” 

Qassim anaendelea kusema kwamba Ninapozungumza na watoto wangu kuhusu Syria, na kuwaambia kwamba tuna familia huko, wananiuliza: Syria ni nini? Ninawaeleza kwamba vita vilizuka, na tukaja kambini. Ninawaambia kwamba kukaa hapa kambini sio chaguo letu mambo yakitulia na hali ya usalama ikiimarika, tutarejea Syria. 

Wananiuliza kuhusu maisha yao ya baadaye hapa na kama watamaliza masomo yao na kisha kuoa na kumiliki nyumba hapa.  

“Ninawajibu kwamba jambo hili haliko mikononi mwetu, bali liko mikononi mwa Mungu, na kwamba kama tulivyokuja bila mipango ya awali, tunaweza pia kurudi Syria bila mipango ya awali.” 

Qassim anamalizia kwa kusema “Natumai kuwa hali itabadilika na kuwa bora. Ninakosa kila kitu nchini Syria, hewa na maji, utoto wangu, kumbukumbu, wazazi na jamaa". 

Nataka kuwa polisi ili kusaidia watu 

 

Ghena Adil Tughan, mkimbizi kutoka Syria akiwa kambini Zaatari nchini Jordan

Zaidi ya watoto 20,000 waliozaliwa kambini Za’atari wamesajiliwa tangu ilipofunguliwa kambi hiyo muongo mmoja uliopita.  

Kizazi kizima cha watoto kimekulia huko, na kambi imekuwa ulimwengu wao. 

Ghina mwenye umri wa miaka kumi alizaliwa Syria na alikuja na familia yake kwenye kambi ya Za’atari alipokuwa na umri wa miezi 6 tu. 

“Nasoma darasa la tatu. Ninapenda shule hapa. Ninapenda hisabati na Kiingereza, lakini somo ninalopenda zaidi ni Kiarabu. Ndoto yangu ni kuwa polisi nitakapokuwa mkubwa, kwa sababu ninataka kuwatumikia watu wangu.” 

Ninawakumbuka sana babu na babu. Bado wako Syria. Mimi huzungumza nao kila siku, nao hunionyesha picha za nyumba yetu na kuniambia mambo yaliyopita. Ninashauku sana ya kuwaona. 

Hali bado mbaya Syria 

Mohammed Gasim Al-Lubbad, mkimbizi kutoka Syria akiwa kambini Zaatari nchini Jordan

Kijana Muhammad mwenye umri wa miaka 14 alifika kambini hapo alipokuwa na umri wa miaka minne tu. Anasema anakumbuka kuwasili kambini hapo. 

“Nilijua tumekuja kambini kutafuta ulinzi na usalama. Sitaki kurudi Syria kwa sababu hali bado si nzuri. Nataka kuwa daktari katika siku zijazo, kwa sababu udaktari ni taaluma nzuri na ajira nzuri.”