Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tuunganishe nguvu ili kupata uhuru na kulinda haki za watu wote, kila mahali: Guterres

Matembezi ya amani na demokrasia nchini Madagascar. Matembezi hayo yaliandaliwa na wanawake.
Photo: UNDP Madagascar
Matembezi ya amani na demokrasia nchini Madagascar. Matembezi hayo yaliandaliwa na wanawake.

Tuunganishe nguvu ili kupata uhuru na kulinda haki za watu wote, kila mahali: Guterres

Haki za binadamu

Leo ni siku ya kimataifa ya demokrasia, na maudhui yanaangazia uhuru wa vyombo vya Habari ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika ujumbe wake amesema ingawa maadhimisho ya mwaka huu ni ya 15, bado duniani kote demokrasia inazidi kurudi nyuma. 

Guterres amesema matukio ya waaandishi wa Habari kunyanyaswa na kuteseka yanaongezeka, waaandishi wanawekwa vizuizini, wakikumbwa na unyanyasaji wa kimwili na hata kuuawa.

Amesema “mateso haya yanafanyika pia mtandaoni ambako wamekuwa wakifuatiliwa na kushambuliwa kwa maneno hususani wanawake na kuonya kuwa bila vyombo huru vya Habari, demokrasia haiwezi kuendelea, na kwamba bila uhuru wa kujieleza hakuna uhuru.”

Guterres amesema taarifa zinazoenesha kuwa hata uhuru wa wananchi kuzungumza unazidi kupungua, mkanganyiko wa taarifa potofu nazo zimezidi kusambaa miongoni mwa jamii huku ubaguzi ukizidi kudhoofisha taasisi za kidemokrasia.

Demokrasia, maendeleo na haki za binadamu vinaimarishana

“Sasa ni wakati wa kuongeza tahadhari. Sasa ni wakati wa kuthibitisha kwamba demokrasia, maendeleo na haki za binadamu vinategemeana na vinaimarishana. Sasa ni wakati wa kutetea kanuni za kidemokrasia za usawa, ushirikishwaji na mshikamano.”

Mkuu  huyo wa umoja wa Mataifa amehitimisha ujumbe wake wa siku hii kwa kusema katika siku ya Demokrasia na kila siku, tuunganishe nguvu ili kupata uhuru na kulinda haki za watu wote, kila mahali.