Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ripoti imetuumbua, majanga mengi ya sasa si ya asili bali ya kujitakia- Katibu Mkuu UN

Wingu la kusababisha dhoruba likijikusanya kwenye pwani ya Barcelona, Hispania
© WMO/Carlos Castillejo Balsera
Wingu la kusababisha dhoruba likijikusanya kwenye pwani ya Barcelona, Hispania

Ripoti imetuumbua, majanga mengi ya sasa si ya asili bali ya kujitakia- Katibu Mkuu UN

Tabianchi na mazingira

Hii leo shirika la Umoja wa Mataifa la hali ya hewa duniani, WMO limezindua ripoti yake kuhusu hali ya hewa na Sayansi ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema ripoti hiyo inadhihirisha kuwa madhara ya mabadiliko ya tabianchi sasa yanaelekea kwenye uharibifu ambao haukuwahi kufahamika.

Katika ujumbe wake Guterres amesema hali ni dhahiri kwa kuzingatia mafuriko makubwa, ukame wa kupitiliza China , Pembe ya Afrika na Marekani bila kusahau mikondo joto barani Ulaya, akisema hakuna chochote cha kusema majanga ya asili bali ni malipo ya binadamu ya uraibu wa mafuta kisukuku.

Mafuriko yaliyokumba jimbo la Balochistan, Pakistani.
UN News/Shirin Yaseen
Mafuriko yaliyokumba jimbo la Balochistan, Pakistani.

Kiwango cha madhara

Idadi ya majanga yatokanayo na hali ya hewa, tabianchi na maji yameongezeka mara 50 katika kipindi cha miaka 50 iliyopita.

Majanga hayo yanasababisha hasara ya dola milioni 200 kila siku.

Guterres anasema licha ya sayansi kuonesha madhara ya mafuta kisukuku, “bado kila mwaka tunaongeza maradufu uraibu wetu wa mafuta kisukuku licha ya dalili za madhara kuendelea kuwa mbaya.”

Cha ajabu zaidi kwa mujibu wa Katibu Mkuu ni kwamba, “tiba tunaifahamu. Viongozi waliahidi kupitia Mkataba wa Paris wa Mabadiliko ya Tabianchi kuhakikisha kiwango cha joto duniani hakiongezeki kwa zaidi ya nyuzi joto 1.5 katika kipimo cha Selsiyasi na kujenga mnepo kwenye tabianchi.”

Ripoti inaonesha “bado tunazidi kwenda mrama. Hatua kwa tabianchi imedorora, na nchi maskini na watu wake ndio wameathirika zaidi,” amesema Katibu Mkuu.

Hakuna nchi ambayo ina kinga dhidi ya madhara ya tabianchi, ametanabaisha Guterres akieleza kuwa ripoti ya leo ni kumbusho la aibu kuwa hatua za kujenga mnepo dhidi ya tabianchi zimepuuzwa kabisa.

Maelfu ya wanyama wameangamia kutokana na ukame uliokithiri unaoikumba Somalia na maeneo mengine ya Pembe ya Afrika.
IOM
Maelfu ya wanyama wameangamia kutokana na ukame uliokithiri unaoikumba Somalia na maeneo mengine ya Pembe ya Afrika.

“Ni kashfa ya kwamba nchi Tajiri zimeshindwa kuzingatia kwa umakini hatua za kukabiliana na madhara ya mabadiliko ya tabianchi, na kupuuzia ahadi zao kwa nchi zinazoendelea,” amesema Mkuu huyo wa UN.

Nini kifanyike sasa” Uamuzi wa Glasgow ndio pa kuanzia

Katibu Mkuu anakumbusha kuwa nchi Tajiri kupitia uamuzi wa Glasgow zinatajiwa kutoa jumla ya dola bilioni 40 kila mwaka kufadhili miradi ya kukabiliana na madhara ya mabadiliko ya tabianchi.

Lakini kiwango hicho amesema hakitoshi Kwani kinatakiwa kuongezeka na kufikia angalau dola bilioni 300 kwa mwaka ifikapo mwaka 2030.

Miradi ya kuhimili mabadiliko ya tabianchi ina manufaa

Katibu Mkuu amesema uwekezaji kwenye miradi ya kuhimili mabadiliko ya tabianchi ina manufaa makubwa kwa binadamu, kwa wahisani na jamii na watu walio hatarini zaidi.

Ametaja nchi 20 zilizoendelea kiuchumi, G20 akisema zina wajibu wa kuleta mabadiliko katika utoaji wa ufadhili wa miradi ya aina hiyo.

Mifumo ya utoaji wa onyo wakati wa majanga

Guterres amegusia pia umuhimu wa mifumo ya utoaji wa onyo akisema, “ndio maana nimetangaza kuwa Umoja wa Mataifa utafanya kazi kuhakikisha mifumo hiyo inapatikana kwa kila mtu duniani ndani ya miaka mitano ijayo.”

India na Honduras, kupitia ushirikiano wa nchi za kusini, SSC, zimekuwa zikifanya kazi pamoja kuimarisha matumizi ya vyanzo vyao vya nishati jadidifu.
UNDP Honduras
India na Honduras, kupitia ushirikiano wa nchi za kusini, SSC, zimekuwa zikifanya kazi pamoja kuimarisha matumizi ya vyanzo vyao vya nishati jadidifu.

Amesema WMO itachukua dhima ongozi ya kufanikisha uwepo wa mifumo hiyo ya onyo wakati wa majanga, huduma ambazo amesema bado ni nadra kwa nchi nyingi zinazoendelea.

Kuhusu nishati jadidifu, Guterres amesema nchi za G20 zinawajibika kwa asilimia 80 ya hewa yote chafuzi duniani na hivyo lazima ziongoze kwa kuchukua hatua za kuondokana na mafuta kisukuku.

“Kusiweko na mtambo mpya wa makaa ya mawe, na makaa ya mawe yawe hayatumiki tena kwa nchi za ushirikiano wa kiuchumi na maendeleo, OECD ifikapo mwaka 2030 na kwa mataifa mengine mwaka 2040.”

Amesisitiza kuwa viongozi watumie ripoti yake kama onyo la kuondokana na mafuta kisukuku na pia waungane kwa kutumia sayansi na waahidi kuchukua hatua sasa.