Maendeleo ya nchi zilizo kusini mwa dunia yanategemea suluhu zenye mshikamano: Guterres
Maendeleo ya nchi zilizo kusini mwa dunia yanategemea suluhu zenye mshikamano: Guterres
Leo, Septemba 12, ni Siku ya Kimataifa ya Ushirikiano wa nchi zilizo Kusini mwa Dunia. Kupitia ujumbe wake wa kuadhimisha siku hii Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema katika zama hizi za changamoto na msukosuko ambao haujawahi kushuhudiwa, “suluhu ziko katika mshikamano”.
Siku hii ya Ushirikiano wa nchi za kusini au ikifahamika kama Ushirikiano wa Kusini-Kusini ni umoja kati ya watu na nchi zinazoendelea, unaojulikana kama Kusini mwa ulimwengu, ambayo inachangia ustawi wa kitaifa, kujitegemea kwa pamoja na kufikia malengo ya kimataifa.
Katibu Mkuu Guterres anasema “Ushirikiano wa Kusini-Kusini na pembetatu ni muhimu kwa nchi zinazoendelea ili kupunguza na kukabiliana na uharibifu unaoletwa na athari za mabadiliko ya tabianchi, kushughulikia janga la afya ulimwenguni, ikiwa ni pamoja na kupona kutokana na coronavirus">COVID-19, na kufikia Malengo yote 17 ya Maendeleo Endelevu (SDGs)”.
Ameeleza changamoto zinazokabili ulimwengu kuwa ni pamoja na mzozo wa kisiasa na kiuchumi ulimwenguni uliosababishwa na vita vya Ukraine pamoja na mabadiliko ya tabianchi ambapo amesema nchi zinazoendelea kwa msaada wa washirika wao kutoka nchi za Kaskazini, taasisi za kifedha za kimataifa, sekta binafsi pamoja na timu za wataalamu wanaofikiria na kuja mapendekezo ya suluhu ni lazima ziimarishe ushirikiano wa Kusini-Kusini na pembetatu.
“Ushirikiano wa Kusini-Kusini na pembetatu lazima kila mara uongeze uwezo wa kutatua changamoto zetu za pamoja”.
Hata hivyo ameeleza kuwa ushirikiano huu haimaanishi nchi tajiri zisichukue jukumu lao la kufanya kazi ili kujenga ulimwengu ulioendelea hususan kupunguza pengo la usawa kati ya mataifa.
“Katika maadhimisho ya siku hii lazima tuzudishe ushirikiano kwa kujenga madaraja ya kufikia kwenye usawa kati ya nchi na ndani ya nchi. Nahimiza mataifa na jumuia zoye kuzidisha ushirikiano na kujenga madaraja ili kufikia mustakabli ulio sawa na endelevu kwa wote,” amesema Katibu Mkuu.
Historia ya Umoja wa Mataifa ya ushirikiano wa nchi zilizo Kusini mwa dunia ilianza mwaka 1949 na kuanzishwa kwa mpango wa kwanza wa misaada ya Baraza la Kiuchumi na Kijamii kwenye Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo Duniani mwaka 1965.