Taasisi ya Molteno imetwaa tuzo ya Confucius ya 2022 ya kujua kusoma na kuandika:UNESCO

Taasisi ya Molteno ya lugha, kusoma na kuandika kutoka nchini Afrika Kusini imetunukiwa tuzo ya kujua kusoma na kuandika ya mwaka 2022 ijulikanayo kama confucius ambayo hutolewa na shirika la elimu sayansi na utamaduni la Umoja wa Mataifa UNESCO.
Taasisi hiyo imeshinda tuzo kutokana na mpango wake wa ufundishaji na utayarishaji wa vipindi kupitia ushiriki wa jamii unaolenga kubadilisha mazingira ya shule kwa kuwaleta pamoja wazazi na jumuiya za mitaani kwa njia inayoleta tija na ya vitendo kwa maslahi ya watoto.
Mkurugenzi mtendaji wa taasisi hiyo Masennya Dikotla anasema katika ufundishaji wao wanatumia mazingira asilia ikiwemo vifaa vya kuchezea kwa sababu,“Mazingira ya michezo asilia yanaongeza tija ya jinsi wanafunzi wanavyoweza kujifunza, jinsi wanavyojiandaa kwa ajili ya masomo na pia shule inavyokuwa tayari kwa ajili yao.”
Masennya ameendelea kusema kuwa taasisi yake, “inatumia viwanja na vifaa asilia vya michezo ambavyo vimetengenezwa na kutayarishwa na wazazi na wana jamii.”
Tuzo ya confucius ilianzishwa na UNESCO mwaka wa 2005, kwa msaada wa serikali ya Jamhuri ya watu wa Uchina, na inazingatia mfumo maalum wa kusoma na kuandika, kwa kutumia mazingira ya kiteknolojia iliyopi ili kusaidia watu wazima katika maeneo ya vijijini na watoto waliooacha shule.
Baada ya kutangzwa washindi wa tuzo hiyo mwenyekiti wa bodi ya shule ya Molteno Emmanuel Ramaphakela amesema ‘”Kwa hakika kila tulichokitengezeza kama wazazi ni kutokana na kila tulichokuwa nacho nyumbani, kuanzia plastiki, majani , matairi kuukuu, basi la mbao hivyo hii inanisogeza karibu na kunifanya kuwa sehemu ya shule, na sehemu ya elimu ya watoto wetu na ndio maana tumefanya hivi.”
Kila mshindi wa tuzo hiyo ya kila mwaka hupokea medali, cheti cha diploma na dola za Kimarekani 30,000.