Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Siku ya kimataifa ya hewa safi: Katibu Mkuu UN atoa wito kwa ushirikiano wa kimataifa

Picha inayoonesha tofauti ya mji wa Beijing. Picha ya juu inaonesha uchafuzi wa hewa na ya chini inaonesha anga ya buluu.
UN News
Picha inayoonesha tofauti ya mji wa Beijing. Picha ya juu inaonesha uchafuzi wa hewa na ya chini inaonesha anga ya buluu.

Siku ya kimataifa ya hewa safi: Katibu Mkuu UN atoa wito kwa ushirikiano wa kimataifa

Tabianchi na mazingira

Ikiwa leo ni siku ya kimataifa ya hewa safi kwa anga la buluu, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guteress ametoa wito kwa mataifa yote ulimwenguni kufanya kazi kwa pamoja kukabiliana na uchafuzi wa hali ya hewa kwani uchafuzi wa hewa hautambui mipaka.

Bwana Guterres katika ujumbe wake kuhusu siku hii ambayo maadhimisho yake ya leo ni ya tatu tangu ipoanzishwa kupitia azimio la mwaka 2019 la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, anasema, Hewa safi sasa ni haki ya binadamu. Hali ya hewa imara ni haki ya binadamu. Asili yenye afya ni haki ya binadamu. Leo, uchafuzi wa hewa unawanyima mabilioni ya watu haki zao. Hewa chafuzi huathiri asilimia 99 ya watu kwenye sayari. 

Katibu Mkuu Guterres anaendelea kueleza kwamba watu maskini wanateseka zaidi, “hasa wanawake na wasichana, ambao afya yao inaathirika na kupikia na kutengeneza joto kutokana na mafuta machafu. Maskini pia wanaishi katika maeneo yaliyosongwa na moshi wa magari na viwanda. Vichafuzi vya hewa pia husababisha ongezeko la joto duniani.” 

Akionesha hali ya sasa ilivyo ya hatari kwa maisha ya binadamu anasema, moto wa nyika unazidi kuchafua hewa. Wakati watu wanakabiliwa na uchafuzi wa hewa na joto kali, hatari yao ya kifo ni asilimia 20 zaidi. 

Mabadiliko ya hali ya tabianchi na uchafuzi wa hewa ni vitu viwili hatari sana, anasema Guterres akieleza kuwa, “katika maadhimisho haya ya tatu ya Siku ya Kimataifa ya Hewa Safi kwa Anga ya Buluu, natoa wito kwa nchi zote kufanya kazi pamoja ili kukabiliana na uchafuzi wa hewa. Tunajua la kufanya. Wekeza katika nishati mbadala na tubadilike kwa haraka kweda mbali na nishati ya kisukuku. Haraka sana nenda kwenye magari yasiyotoa hewa chafuzi na njia mbadala za usafiri. Ongeza upatikanaji wa nishati safi ya kupikia, kutengeneza joto na ya kupozea. Rejeleza taka badala ya kuzichoma moto. Hatua hizi zinaweza kuokoa mamilioni ya maisha kila mwaka, kupunguza kasi ya mabadiliko ya hali ya tabianchi na kuharakisha maendeleo endelevu. Uchafuzi wa hewa haujui mipaka. Kwa hivyo, mataifa lazima yafanye kazi pamoja.” 

Aidha Bwana Guterres anaendelea kutoa ushauri kwa mataifa duniani kwamba yatufuatilie uchafuzi wa hewa. yatengeneza sheria ili kukidhi Mwongozo wa Ubora wa Hewa wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Ulimwenguni, WHO na kutoa mipango ya kuaminika ya kupunguza uzalishaji wa hewa chafuzi kutoka katika magari, mitambo ya kuzalisha umeme, ujenzi, na viwanda. Kwa pamoja, tunaweza kupunguza uchafuzi wa hewa na kuweka watu na sayari wakiwa na afya na usalama. 

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liliteua tarehe 7 Septemba kuwa Siku ya Kimataifa ya Hewa Safi kwa anga ya buluu mwaka 2019, na Siku ya kwanza iliadhimishwa mwaka wa 2020. Siku ya Kimataifa ya Hewa Safi kwa anga ya buluu inatoa wito kwa kila mtu kuendelea na ushirikiano wa kimataifa, kati ya serikali na serikali, mashirika pamoja na mashirika ya kiraia na watu binafsi, kuwahimiza kuchukua hatua kwa ajili ya kupunguza uchafuzi wa hewa na kuleta mabadiliko ya mabadiliko ya hewa tunayoshiriki.