Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maabara inayotembea mkombozi kwa shule zisizo na maabara Tanzania

Wanafunzi wanne wakiwa wamevaa makoti ya maabara katika jaribio la sayansi darasani nchini Tanzania.
Evarist Mapesa / UN News Kiswahili Wilson akiwa na wanafunzi wakijianda kuanza kuonesha kwa vitendo vifaa wanavyovitumia katika maabara

Maabara inayotembea mkombozi kwa shule zisizo na maabara Tanzania

Utamaduni na Elimu

Wadau wa elimu nchini Tanzania wamebuni maabara inayotembea ili kuwafikia wanafunzi wengi zaidi katika shule za msingi na secondary ambazo zina uhaba wa vifaa vya masomo ya sayansi kwa lengo la kufundishia kwa vitendo na kuwahamasisha kuyapenda masomo hayo.

Hatua hiyo inalenga kufikia lengo namba 4 la malengo ya maendeleo endelevu ya Umoja wa Mataifa linalohimiza elimu bora yenye usawa na kukuza fursa za kujifunza maishani kwa wote ifikapo mwaka 2030.

Bilauri  za vioo, plastiki, mapulizio, Box, chupa za maji, na karatasi laini (Tissue) ni miongoni mwa vifaa vya kufundishia masomo ya biolojia ,chemia, na fizikia ambavyo kwa kawaida hupatikana majumbani na madukani,lakini sasa vimegeuzwa matumizi maeneo ya shule na kugeuka kuwa mkombozi kwa wanafunzi wa shule za msingi na secondary nchini Tanzania.

Wilson Kamunye, ni mwakilishi wa Shirika la sayansi duniani upande wa bara la Africa,ambaye ndiye aliyebuni maarifa haya kwa kutafuta uwepesi huu kwa wanafunzi kushiriki katika masomo ya sayansi kwa kubuni njia hii ya kufundishia masomo hayo kwa kutumia vifaa rahisi ambavyo wakati mwingine huvibeba na Kwenda katika shule za msingi na secondary nchini Tanzania.

Wilson ameamua kutumia njia hii ya Maabara inayo safiri, ambapo huchukua vifaa vyake na Kwenda katika shule nchini Tanzania ambzo zina Changamoto ya upungufu wa vifaa vya sayansi hivyo kutumia nafasi yake kuwafundisha wanafunzi kwa vitendo Zaidi.

kupitia ubunifu huu ambao ameufanya hadi sasa amefanikiwa kuzifikia  takribani shule 125 za msingi Tanzania na shule moja ya upili na malengo yake ni kuhakikisha anafika maeneo yote yenye uhaba wa vifaa hivyo ili kuwahamasisha wanafunzi kuyapenda masomo ya sayansi na kuwa wabobevu katika eneo hilo.

“Tunatarajia tuwe na vituo vya sayansi na pia tufungue vyumba maalum au vyumba vya kufundishia sayansi na kuendeleza hizi maabara ambazo zina safiri zifikie maeneo yote nchini kwetu (Tanzania) na hata kama ikivuka mipaka ya nchi yetu ifikie bara la afrika waweze pia kujifunza kwa kupitia hizi zana ambazo ni rahisi Zaidi”,alisema Kamunye.

Wilson Kamunye, mwanzilishi wa Moving Laboratory, anasimama nyuma ya meza iliyojaa vifaa vya maonyesho ya sayansi na vifaa vya maabara.
Evarist Mapesa / UN News Kiswahili Wilson Kamunye muasisi wa maabara inayo safiri akiwa na baadhi ya vifaa anavyotumia kufundishia wanafunzi

Je Maabara inayo safiri ni nini?

Kwa mujibu wa Kamunye hii ni Maabara inayofika katika maeneo mbalimbali kwa kuchukua vifaa vyepesi vinavyobebeka na vinavyopatikana kwa urahisi katika maeneo mengi na kuviweka katika sehemu maalumu ya kutunzia kisha kuondoka navyo hadi katika eneo ama shule husika.

Hata hivyo vyombo hivyo hubebwa katika ma kontena ya kubebea vifaa na kufikisha huduma katika maeneo ambayo hayana maabara ili kutoa ili kuweka urahisi wa kufundisha Watoto.

“Tumeanzisha maabara inayotembea kama moja wapo ya program zetu hasa kutatua Changamoto iliyopo kwenye nchi yetu maana maeneo mengi hayana vifaa vya maabara,n ahata maabara zilizopo unaweza kukuta hazina vifaa vinavyokidhi haja ya watoto kujifunza”,amesema Kamunye.

“Tunakuja na hizi mbinu za kufundisha kwa njia rahisi Zaidi na kwa kusafiri maana unaweza kubeba vifaa vyako ukaenda kufundisha Watoto kwa urahisi kabisa ndiyo maana niliamua kuanzisha hii maabara inayosafiri”,aliongeza Kamunye.

Amekuwa akifanya maonesho ya sayansi kwa njia ambayo ni rahisi kumuweka mtoto katika utayari wa kiakili kupokea kile atakachoelekezwa kwani hadi hutumia mbinu ya uchekeshaji ili kumfanya mtoto ashangae na kushawishika kuanza kujaribu kufanya mwenyewe kwa vitendo.

“Tuna njia ambazo tunazitumia kuwasiliana na Watoto katika kufundishia, vifaa vyenyewe tu jinsi unavyovitumia mtoto anahamasika kwenda kuvitafuta nyumbani,lakini pia namna yanavyofanyika majaribio yanavutia, kwa maana kwamba mtoto anashangaa, ile kumshangaa tu ni hatua ya kumvutia mtoto, anataka nay eye aendelee kujifunza zaidi”,alisema Kamunye.

Kupitia njia hizo zimekuwa zikiwavutia wanafunzi wengi ambao wamefikiwa na huduma hii kuanza kuyapenda masomo hayo ambayo kila mara Umoja wa Mataifa, Serikali, Wadau na Asasi za kiraia wamekuwa wakiwahamasisha kuyasoma ili kuwa wanasayansi watakao saidia mataifa yao na ulimwengu kwa ujumla.

Wanafunzi watatu waliovaa makoti ya maabara na miwani ya rangi wanashikilia bia katika maabara ya sayansi. Skrini kubwa nyuma yao inaonyesha saa 11:20 na tarehe Jumatatu, Agosti 29.
Evarist Mapesa/ UN NEWS Kiswahili Wanafunzi wakiwa maabara

Hali ya Maabara za shule na upatikanaji wa vifaa ipoje nchini Tanzania?

Kwa miaka mingi nchini Tanzania kumekuwa na upungufu wa maabara katika shule za msingi na upili hali ambayo imekuwa ikisababisha wanafunzi wanaosoma masomo ya sayansi kuishia kukariri,na kupata majaribio ya vitendo kwa kiasi kidogo.

Baadhi ya shule hususani zile za upili zimekuwa zikienda kuazima vifaa vya kufanyia majaribio katika shule Jirani ili waweze kufanya kwa vitendo hali inayowafanya wengine kuishia njiani na kuamua kusoma masomo ya Sanaa.

Katika shule za msingi zinazomilikiwa na serikali hazima maabara ya masomo ya sayansi hivyo huishia tu kuona vifaa hivyo kwenye  michoro ya vitabu wakisubiria watakapofika shule ya upili ndipo waanze kuviona kwa uhalisia na kujifunza matumizi yake.

Kwa mujibu  wa Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Tamisemi katika mwaka wa fedha 2018/19 ilijenga maabara 165 za masomo ya sayansi katika shule mbalimbali nchini huku ikitaka kila shule inayofundisha masomo ya sayansi kuwa na maabara tatu za masomo ya Fizikia, Kemia na Baiolojia.

Licha ya jitihada hizo za Serikali, takwimu za elimu za elimu msingi (BEST) mwaka 2017 zilionyesha kulikuwa na upungufu wa asilimia 42.7 za maabara katika shule zote nchini.
Lakini kubuniwa kwa maabara hii kunaenda kuleta ahueni kwa wanafunzi wanaosoma masomo ya sayansi nchini Tanzania.

“kwa asilia ya masomo ya sayansi unapaswa uyafundishe kwa vitendo na siyo nadharia, na muda mwingine Watoto wanashindwa kupambanua zile ndoto zao ambazo wanazo na kushindwa kuzitimiza”,alisema Kamunye.

“Ninavyoona kwa hali hii na mwamko walionao utawasaidia sana Watoto kupenda masomo kwasababu Watoto ambao nimeshakutana nao asilimia kubwa ninapokuwa ninawafundisha baada ya kipindi kumalizika unaona kabisa Watoto wanatamani, kwahiyo hali hii inawavutia Watoto”,aliongeza Kamunye.

Wanafunzi watatu vijana wa kiume Weusi waliovaa makoti meupe ya maabara na miwani ya usalama wanafanya jaribio la sayansi mezani wakiwa na vifaa vya maabara. Skrini kubwa inayoonyesha muda iko nyuma.
Evarist Mapesa / UN News Kiswahili Wanafunzi wakiwa maabara wakijifunza kwa vitendo

Wanafunzi wamerahisishiwa kujifunza

Wanafunzi nchini Tanzania wamekuwa wakikatishwa tamaa na uhaba wa vifaa vya kujifunzia masomo ya sayansi kutokana na baadhi ya shule kujikuta wakiwapanga katika makundi ya watu 10 ili waweze kujifunza.

Hali hiyo huwapa umugu wa kuelewa na hatimaye kuamua kuachana na masomo hayo na badala yake Kwenda kujifunza masomo ya Sanaa ambayo yamekuwa yakichukuliwa kuwa ni rahisi kuyafaulu.

Ramadhan Mrisho ni mwanafunzi wa kidato cha tatu shule anayesoma masomo yake jijini Mwanza Kaskazini Magharibi Mwa Tanzania, awali kabla ya kuanzishwa kwa mradi huo alikuwa ameshaanza kuvunjika moyo.

“kabla ya mwalimu hajaja kutufundisha kwa vitendo,sayansi kwangu ilikuwa ni ngumu na nilitamani kuweza kuiacha”,alisema Ramadhan.

Kwa mujibu wa sera mpya ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014, asilimia tano ya wanafunzi wanaomaliza elimu ya msingi ndiyo wanaofika mpaka kidato cha tano na sita 
Sera hiyo ilienda mbali Zaidi na kueleza kuwa katika wanafunzi wanaosoma sekondari nchini, 30 hadi 35 kati ya 100 ndiyo wanaosoma masomo ya sayansi wakiwa kidato cha tatu na nne.

Lakini program hii imeanza kuleta tabasamu kwa wanafunzi katika shule ambazo zimefikiwa na mradi huu wa maabara inayotembea katika shule za msingi na secondary nchini Tanzania.

Annah William Pima anasema “tulikuwa tunajifunza lakini tulikuwa hatupati fursa ya kujifunza kwa vitendo zaidi,kwa hiyo tulikuwa tunajifunza tu darasani kwa nadharia tu,tulikuwa hatufanyi majaribio ya vitendo kama hivi lakini tangu alipokuja, tunasoma darasani kwa nadharia wakati huo huo tunaelekezwa na kwa vitendo na tunaelewa vizuri Zaidi yah apo awali”,alisema Pima.

Walimu watoa neno

Kutokana na Changamoto ya uhaba wa vifaa vya kufundishia masomo ya sayansi, walimu katika shule za msingi na upili nchini Tanzania wamekuwa wakitumia muda mwingi kuwaelekeza wanafunzi juu ya mada husika.

Kuwepo kwa maabara hii kumewasaidia walimu kupata mafunzo ya kujengewa uelewa wa kufundisha masomo hayo kwa kutumia vifaa rahisi na vinavyopatikana katika maeneo ya nyumbani.

Mwalimu wa masomo ya sayansi Yohana Herman,anasema “masomo yetu ya sayansi yanahitaji vifaa ili kujifunza kwa vitendo,kama vifaa havipo inakuwa ni Changamoto, na kitu nilichokigundua kutoka kwa wanafunzi tangu kuanzishwa kwa huu mradi nimegundua kuwa hakuna mwanafunzi ambaye hajui”alisema Herman.

Malengo ya Kamunye ni kuhakikisha kuwa wanafunzi wa Tanzania na mataifa ya Afrika wanasoma masomo hayo kwa vitendo ili kupata wanasayansi mahiri hapo baadae.