Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto milioni 244 hawako shuleni muhula mpya wa shule ukianza:UNESCO

Watoto wakisubiri kuingia darasani katika moja ya shule nchini Burkina Faso
© UNICEF/Vincent Tremeau
Watoto wakisubiri kuingia darasani katika moja ya shule nchini Burkina Faso

Watoto milioni 244 hawako shuleni muhula mpya wa shule ukianza:UNESCO

Utamaduni na Elimu

Wakati msimu mpya wa shule ukianza sehemu mbalimbali duniani , takwimu mpya zilizotolewa leo mjini Paris Ufaransa na shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni UNESCO zinaonyesha kwamba watoto na vijana milioni 244 wenye umri wa kati ya miaka 6 na 18 duniani kote bado hawako shule.

Mkurugenzi mkuu wa UNESCO Audrey Azoulay, Director-General, ametoa wito wa hatua za pamoja ili kuhakikisha kwamba haki ya kila mtoto kupata fursa ya elimu bora inaheshimiwa.
Takwimu hizo zimeonyesha kuwa nchi za Afrika zilizoko Kusini mwa Jangwa la Sahara zinasalia kuwa ukanda wenye Watoto wengi zaidi wasio shuleni ambao ni milioni 98 na pia ndio ukanda pekee ambako idadi inaongezeka.
Ukanda wa Kati na Kusini mwa Asia unashikilia nafasi ya pili ya idadi kubwa ya watoto ambao hawako shuleni, milioni 85.


Malengo ya elimu hatarini

"Hakuna anayeweza kukubali hali hii," amesems Audrey Azoulay, mkurugenzi mkuu wa UNESCO, akisisitiza haja ya kuheshimu haki ya kila mtoto ya kupata elimu.
Ameonya kwamba "Kwa kuzingatia matokeo haya, lengo la elimu bora kwa wote ifikapo mwaka 2030, lililowekwa na Umoja wa Mataifa, lina hatari ya kutofikiwa. Tunahitaji uhamasishaji wa kimataifa ili kuweka elimu katika kipaumbele cha ajenda ya kimataifa."
Bi. Azoulay amerudia wito wake katika mkutano wa kihistoria wa kubadili elimu utakaofanyika tarehe 19 Septemba mwaka huu, katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ameitisha mkutano huo ili kuhamasisha hatua na suluhu, ikiwa ni pamoja na kubadili athari za kielimu zilizotokana na janga la COVID-19.