Burian Mikhail Gorbachev, ulikuwa kiongozi wa aina yake:Guterres
Burian Mikhail Gorbachev, ulikuwa kiongozi wa aina yake:Guterres
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema ameshtushwa na taarifa za kifo cha aliyekuwa Rais wa zamani wa shirikisho la Urusi Mikhail Gorbachev.
Kupitia taarifa iliyotolewa Jumanne jioni na msemaji wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema “Gorbachev alikuwa kiongozi wa aina yake ambaye alibadili historia. Alifanya mengi zaidi kuliko mtu mwingine yeyote ili kumaliza kwa amani wa vita baridi.”
Katibu Mkuu kwa niaba ya Umoja wa Mataifa, ametuma rambirambi zake za dhati kwa familia ya Mikhail Gorbachev na kwa watu na serikali ya Shirikisho la Urusi.
Guterres amekumbusha kuwa wakati Gobachev akipokea tuzo ya amani ya Nobel mwaka 1990, alisema kwamba “Amani sio umoja katika kufanana bali ni umoja katika utofauti.”
Aliweka mtazamo wake katika vitendo
Taarifa hiyo ya Guterres imeendelea kusema kuwa aliweka ufahamu huo muhimu katika vitendo kwa kufuata njia ya mazungumzo, mageuzi, uwazi na kupokonya silaha.
Katika miaka yake ya baadaye, Mikhail Gorbachev alikumbatia changamoto mpya muhimu vile vile kwa ustawi wa wanadamu, kuunda mustakabali endelevu kwa kukuza uhusiano wenye usawa kati ya wanadamu na mazingira. “Ilikuwa katika Imani hiyo ndio kwamba alianzisha Green Cross International.”
Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema “Ulimwengu umempoteza kiongozi mahiri wa kimataifa, mtetezi wa ushirikiano wa kimataifa aliyejitolea, na mtetezi wa amani asiyechoka.”
Kwa mujibu wa duru za Habari Gorbachev ameaga dunia mjini Moscow akiwa na umri wa miaka 91 baada ya kuugua kwa muda mrefu. Alizaliwa 2 Machi mwaka 1931 mjini Misha Urusi na alikuwa kiongozi wa 9 na wa mwisho wa Muungano wa Soviet ukijulikana kama USSR.
Pamoja na kumaliza vita baridi alisaini mkataba wa kupunguza silaha na Marekani na washirika wengine wa Ulaya ili kuondoa pazia la chuma ambalo liliiganywa Ulaya tangu vita ya pili ya dunia na kurejesha muungano kati ya Ujerumani Mashariki na Magharibi ambayo sasa ni nchi moja ya Ujerumani.