Guterres asikitishwa mkutano wa NTP kumalizika bila muafaka
Guterres asikitishwa mkutano wa NTP kumalizika bila muafaka
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amesisitiza haja ya mazungumzo ili kupunguza tishio la nyuklia baada ya nchi kushindwa kufikia maafikiano katika mkutano wa kuupitia mkataba wa kihistoria wa kuzuia kusambaa kwa silaha za nyuklia (NPT).
Taarifa iliyotolewa na msemaji wake inasema kufuatia wiki nne za majadiliano makali katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, mkutano wa kumi wa mapitio ya nchi wanachama NPT ulimalizika Ijumaa jioni bila matokeo ya muafaka kwa sababu Urusi ilipinga kutuma ujumbe kuhusu udhibiti wake kwenye vituo vya nyuklia vya Ukraine.
Katibu Mkuu ameelezea kusikitishwa kwake kwamba nchi hazikuweza kufikia makubaliano juu ya "matokeo muhimu", na kutumia fursa ya kuimarisha mkataba huo uliodumu kwa miaka 52 na kuendeleza malengo yake, msemaji wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric amesema katika taarifa hiyo.
Hatari inayoongezeka
Wakati mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa akikaribisha ushirikiano wa dhati na wa maana wa pande husika, na ukweli kwamba mkutano huo ulitambua NPT kama msingi wa udhibiti wa upokonyaji silaha duniani na kutoeneza silaha za nyuklia , amesikitika kwamba haikuweza kutatua changamoto kubwa zinazotishia usalama wa pamoja wa kimataifa.
"Mazingira magumu ya kimataifa na hatari kubwa ya silaha za nyuklia kutumika, kwa bahati mbaya au kwa makosa, yanahitaji hatua za haraka na madhubuti. Katibu Mkuu anatoa wito kwa mataifa yote kutumia kila njia ya mazungumzo, diplomasia na majadiliano ili kupunguza mivutano, kupunguza hatari ya nyuklia na kuondoa tishio la nyuklia mara moja na kwa wote," Bwana. Dujarric alisema.
Ameongeza kuwa "Ulimwengu usio na silaha za nyuklia unasalia kuwa kipaumbele cha juu zaidi cha Umoja wa Mataifa cha kutokomeza silaha na lengo ambalo Katibu Mkuu anaendelea kujitolea kwa dhati."
Ucheleweshaji
Mkataba wa NPT, ambao ulianza kutekelezwa Machi 1970, ndio ahadi pekee ya lazima kwa lengo la kupokonya silaha na mataifa ambayo huhifadhi rasmi silaha za nyuklia.
Umeandaliwa karibu na nguzo tatu ambazo ni upokonyaji silaha, kutoeneza, na matumizi ya amani ya nishati ya nyuklia na nchi 191 zimejiunga na mkataba huo.
Kongamano la mapitio ya mkataba huo hufanyika kila baada ya miaka mitano. Kikao cha 2015 pia kilimalizika bila hati ya matokeo huku mkutano wa 2020 ukiahirishwa kwa sababu ya janga la coronavirus">COVID-19.
Balozi Gustavo Zlauvinen wa Argentina, Rais wa mkutano wa mapitio, aliwaambia waandishi wa habari kuwa amechanganyikiwa kwamba pande husika hazikupitisha waraka wa matokeo kwa makubaliano.
Kibvuli cha vita ya Ukraine
Bwana. Zlauvinen amesema alijua matarajio yalikuwa madogo sana hata kabla ya mkutano kuanza, kutokana na mitazamo tofauti kuhusu masuala kama vile ahadi za hapo awali kuhusu uhakikisho wa usalama.
"Lakini uvamizi wa Ukraine uliofanywa na Urusi mwezi Februari umezidisha mivutano hiyo, na tulijua kwamba vita ya Ukraine ingeweka kivuli kwenye Mkutano wa Mapitio," alisema katika mkutano na waandishi wa habari Ijumaa jioni.
Mkutano wa mwisho ulicheleweshwa na baadaye kusimamishwa kwa masaa kadhaa, kwa sababu ya mazungumzo ya dakika za mwisho, haswa na ujumbe wa Urusi, ambao haukuweza kukubaliana na maandishi "isipokuwa mabadiliko muhimu sana yataletwa katika lugha na kuhusu hali ya vifaa vya nyuklia vya Ukraine vilivyo chini ya udhibiti wa Urusi.”
Bwana. Zlauvinen alijaribu kuona ikiwa wajumbe wengine wangekubali lugha hii, "na haikuwa hivyo".
Aliamini kuwa kwa ujumla, mkutano wa mapitio ulikuwa wenye maana. Wajumbe walishiriki katika majadiliano juu ya masuala magumu sana, na ukosefu wa hati ya matokeo haukupunguza kazi yao.
"Ni kama tulikuwa na sinema kwa wiki nne, lakini hatukuweza kupiga picha mwishoni mwa filamu," alisema. "Kwa hivyo kutokuwa na picha hiyo hakuonyeshi kwamba sinema hiyo haikuwepo. ."
Juhudi zahitajika maradufu
Mwakilishi mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya upokonyaji silaha, Izumi Nakamitsu, pia alihutubia wanahabari na kusema alisikitishwa na matokeo.
"Rasimu ya mwisho, bila shaka, haikuwa hati kamilifu. Sote tulijua hilo. Lakini pande nyingi za mataifa zilihisi kuwa bado itakuwa kwa manufaa ya jumuiya ya kimataifa,” alisema.
"Kwa hivyo, changamoto yetu sasa ni kuhakikisha kwamba tutaanza kutoka hapa na, ikiwa tutaweza, kuongeza juhudi zetu ili kuhakikisha kuwa juhudi za kutokomeza silaha za nyuklia, kwa kweli, zitaimarishwa tena."
Nakamitsu alisisitiza kuwa ingawa hii ilikuwa mara ya pili mfululizo mkutano huo ulimalizika bila matokeo ya makubaliano, NPT haitaanguka au kupata uharibifu wa haraka.
"Hata hivyo, nadhani inabidi tuhakikishe kwamba tutabadili mwelekeo huu wa imani na dhamira katika udhibiti huu wa NPT unaoendelea kupungua. Tunahitaji kubadilisha hali ya kuchanganyikiwa,” alisema.
Aliongeza kuwa "Na ili hilo lifanyike, inabidi tuhakikishe kuwa kutakuwa na ushirikiano mkubwa na wa kati ya mataifa yenye silaha za nyuklia na mataifa yasiyo ya nyuklia, na bila shaka, muhimu sana, ni kati ya mataifa yenyewe yenye silaha za nyuklia pia."