Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tumepata mafanikio makubwa kwenye utoaji wa misaada Ukraine: OCHA

Vifurushi vya chakula vya WFP vinagawiwa kwa watu walioathiriwa na vita katika Mkoa wa Kharkiv kwa ushirikiano na Shirika la Msalaba Mwekundu la Ukraine.
© WFP/Ukrainian Red Cross/Yurii Chornobuk
Vifurushi vya chakula vya WFP vinagawiwa kwa watu walioathiriwa na vita katika Mkoa wa Kharkiv kwa ushirikiano na Shirika la Msalaba Mwekundu la Ukraine.

Tumepata mafanikio makubwa kwenye utoaji wa misaada Ukraine: OCHA

Msaada wa Kibinadamu

Mratibu wa Misaada ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa kwa nchi ya Ukraine, Denise Brown, yupo katika ziara ya siku tatu mashariki mwa Ukriane huko Kharkiv ambapo ameeleza mafanikio yaliyofikiwa mpaka sasa katika utoaji wa misaada ya Kibinadamu na changamoto zijazo na namna walivyojipanga kuzitatua.

Taarifa iliyotolewa na ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya dharura, OCHA nchini Ukraine imemnukuu Drown akieleza kuwa vita vinayoendelea nchini humo havijazuia jumuiya ya kibinadamu kutoa misaada.

“Tangu kuanza kwa vita, tumefikia zaidi ya watu milioni 12 haya ni mafanikio makubwa. Hii ni katika utoaji wa fedha taslimu ,usaidizi katika afya, usaidizi kwenye makazi, upatikanaji wa maji safi, ulinzi, na ukarabati. Kwa hivyo timu iliyo hapa inafanya kazi kwa bidii sana.”

Ameeleza pia wamefanikiwa kuwafikia watu wasiopungua milioni moja katika maeneo yasiyodhibitiwa na Serikali. Usaidizi upande wa Urusi

Hata hivyo ameeleza mara nyingi hawapati kibali cha kupata hakikisho la usalama tunalohitaji kutoka Serikali ya Urusi ili kuvuka mstari wa mbele kwa ajili ya kwenda kutoa misaada upande huo.

“Tuna wafanyakazi katika maeneo hayo, na wafanyakazi katika maeneo hayo wanathibitisha kwamba kuna mahitaji makubwa ya kibinadamu. Na hii ni moja ya wasiwasi mkubwa.”

Brown amesema wana uwezo wa kutoa msaada mpaka karibu na maeneo ya vita yanayoshikiliwa na Urusi na kueleza “Kwa siku ya leo tuna msafara unaoendelea hadi eneo la kilomita 5 kutoka mstari wa mbele wa vita.”

Nadia (Kulia) aligundua kwamba alikuwa mjamzito wakati wa mashambulizi makali ya makombora katika eneo la Kharkiv, mashariki mwa Ukraine
Source of Revival NGO
Nadia (Kulia) aligundua kwamba alikuwa mjamzito wakati wa mashambulizi makali ya makombora katika eneo la Kharkiv, mashariki mwa Ukraine

Mipango ya msimu wa baridi

Amesema tathmini waliyofanya wanaona kwa msimu wa baridi, watu wanahitaji kufanyiwa matengenezo ya madirisha, ukarabati wa milango, mifumo ya kawaida ya joto hasa kwa wazee na wanaoishi vijijini.

“Tunashughulikia kupanga mipango kwa kushirikiana na wafanyakazi wa kujitolea wa ndani ili kuhakikisha kuwa tunaweza kuwaangalia vyema.”

Amesema OCHA ipo mstari wa mbele kuhakikisha kuwa jamii zimejiandaa vyema kwa miezi ya msimu wa baridi ni kwakuwa watu walioko Ukraine wameteseka sana, nikama wamepoteza maisha yao, wamepoteza wapendwa wao na shughuli zao za uzalishaji wa kilimo.

Hata hivyo amesema badoa wana wasiwasi kama wataweza kuwasaidia walio upande ulio chini ya majeshi ya Urusi kwakuwa bado hawajapata kibali .

“Inabidi tutoe usaidizi kwa mtu yeyote yule. Ninatumaini Urusi itatoa hakikisho la usalama ili kuvuka. Hayo tu ndiyo tunayotaka kufanya, tunahitaji kutoa insulini kwenye hospitali, kutoa blanketi, kutoa magodoro, mafuta kama tunaweza, na kutengeneza madirisha na milango. Sio ngumu.”

Mratibu wa Misaada ya Kibinadamu Umoja wa Mataifa kwa nchi ya Ukraine amesema kwa sasa wanaunganisha pamoja mpango wa jumla wa majira ya baridi, ambao utahusu wapi hospitali na zahanati zinazohitaji jenereta kwa ajili ya umeme, kuangalia wapi kwenye uhitaji wa msaada wa fedha taslimu katika miezi ya majira ya baridi, wapi UNHCR na IOM zinahitaji kutengeneza madirisha na milango, na jinsi watakavyo kuwa wanaangalia hali za kimwili ya watu.