Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

OCHA yataka mafuta yaliyochukuliwa kwenye ghala la WFP huko Tigray yarejeshwe

Msafara wa malori 50 ya WFP ukielekea Tigray nchini Ethiopia ukiwa na misaada ya kibinadamu.
© WFP
Msafara wa malori 50 ya WFP ukielekea Tigray nchini Ethiopia ukiwa na misaada ya kibinadamu.

OCHA yataka mafuta yaliyochukuliwa kwenye ghala la WFP huko Tigray yarejeshwe

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya dharura, OCHA, Martin Griffiths ameeleza kusikitishwa kwake na kuondolewa kwa nguvu kwa meli za mafuta kutoka katika maghala ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa chakula duniani WFP huko Mekelle, Tigray nchini Ethiopia.

Kupitia taarifa yake iliyotolewa jijini New York Marekani Griffiths amesema Meli 12 zilizokuwa zimebeba zaidi ya lita 570,000 za mafuta zilikusudiwa kusaidia Umoja wa Mataifa na washirika wake kusambaza vifaa vya misaada ya kibinadamu kwa watu ambao wanahitaji msaada.

“Bila misaada hivyo watu wataachwa bila chakula, virutubisho vya lishe, madawa na vitu vingine muhimu. Wakati ambapo utapiamlo na uhaba wa chakula unaongezeka, matokeo yanaweza kuwa mabaya.”

Mkuu huyo wa misaada amelaani utoroshwaji wowote wa mali za misaada. “ Usambazaji wa misaada ya kibinadamu lazima ulindwe kote Ethiopia. Uzuiaji wa misaada ya kibinadamu lazima ukomeshwe.”

Kupitia taarifa hiyo pia amerejea kutoa wito wa kurejesha huduma za kimsingi huko Tigray, ikiwa ni pamoja na huduma za benki na mifumo ya umeme, ambayo inaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa kuboresha hali ya usaidizi wa kibinadamu katika eneo hilo.

Tarehe 25 mwezi huu wa Agosti,2022 Mkurugenzi mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP alitoa taarifa ya kuitaka mamlaka ya Tigrayan kurejesha mara moja akiba ya mafuta iliyoibiwa kwa jumuiya ya kibinadamu.  

David Beasley alisema kundi la watu wenye silaha waliingia katika ghala la WFP huko Mekelle na kukamata kwa nguvu meli 12 zilizojaa zaidi ya lita nusu milioni za mafuta. 

Soma zaidi hapa