Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Karibu watoto 1000 wameuawa au kujeruhiwa na vita Ukraine: UNICEF

Msichana wa miaka 11 aliyepoteza miguu yote miwili katika shambulio la kombora katika kituo cha treni cha Kramatorsk apata nafuu katika hospitali ya Lviv nchini Ukraine.
© Courtesy of Lviv Territorial Medical Union Hospital
Msichana wa miaka 11 aliyepoteza miguu yote miwili katika shambulio la kombora katika kituo cha treni cha Kramatorsk apata nafuu katika hospitali ya Lviv nchini Ukraine.

Karibu watoto 1000 wameuawa au kujeruhiwa na vita Ukraine: UNICEF

Amani na Usalama

Takriban watoto 972 nchini Ukraine wameuawa au kujeruhiwa na ghasia tangu vita vilipoongezeka karibu miezi sita iliyopita, ikiwa ni wastani wa zaidi ya watoto watano wanaouawa au kujeruhiwa kila siku amesema mkurugenzi mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF.

Kupitia taarifa yake iliyotolewa leo mjini Geneva Uswis Catherine Russell amesema "Takwimu hizi ni zile ambazo Umoja wa Mataifa umeweza kuthibitisha. Tunaamini idadi ya kweli kuwa kubwa zaidi.” 

Ameongeza kuwa “Matumizi ya silaha za vilipuzi yamesababisha vifo vingi vya watoto. Silaha hizi hazibagui raia na wapiganaji, hasa zinapotumiwa katika maeneo yenye watu wengi kama ilivyokuwa nchini Ukraine huko Mariupol, Luhansk, Kremenchuk, na Vinnytsia na rodha inaendelea. 

Amesisitiza kuwa kwa mara nyingine tena, kama katika vita vyote, maamuzi ya watu wazima ya kutojali yanaweka watoto katika hatari kubwa kwani hakuna operesheni za silaha za aina hii ambazo hazisababishi watoto kudhurika. 

Bi Russell amesema “Wakati huohuo, mbali ya hofu zaidi ya watoto kuuawa au kujeruhiwa katika mashambulizi, karibu kila mtoto nchini Ukraine amekabiliwa na matukio yenye kuhuzunisha sana, na wale wanaokimbia machafuko wako katika hatari kubwa ya kutengana na familia zao, kukabiliwa na ghasia, dhuluma, unyanyasaji wa kingono, na usafirishaji haramu wa binadamu.” 

Madaktari waliondoa kipande cha makombora chenye urefu wa sentimeta nne na kuokoa maisha ya mvulana mwenye umri wa miaka 13 baada ya kujeruhiwa vibaya na makombora mashariki mwa Ukraine.
© Courtesy of Lviv Territorial Medical Union Hospital
Madaktari waliondoa kipande cha makombora chenye urefu wa sentimeta nne na kuokoa maisha ya mvulana mwenye umri wa miaka 13 baada ya kujeruhiwa vibaya na makombora mashariki mwa Ukraine.

Amesema wakati muda wa kurejea shuleni ukiwa umesalia zaidi kidogo ya wiki moja hii ni kumbusho ya kiasi gani Watoto wa Ukraine walivyopoteza masomo, kwani amesema

"Mfumo wa elimu wa Ukraine umesambaratishwa na kuongezeka kwa uhasama nchini kote. Shule zimekuwa zikilengwa au kutumiwa na pande zote katika vita na hivyo kusababisha familia kutohisi salama kupeleka watoto wao shuleni. Tunakadiria kuwa shule 1 kati ya 10 imeharibiwa au kusambaratishwa. Watoto wote wanahitaji kuwa shuleni na kujifunza, ikiwa ni pamoja na watoto walio katika dharura wakiwemo watoto nchini Ukrainia na wale waliolaziokika kukimbia sababu ya vita.” 

Mkuu huyo wa UNICEF amehitimisha taarifa yake kwa kuendelea kutoa wito kwa pande zote katika mzozo nchini Ukraine kusitisha uhasama mara moja na kuwalinda Watoto wote dhidfi ya vita hiyo ikiwa ni pamoja na kuacha kutumia silaha nzitonzito katika maeneo yenye watu wengi na kushambulia rai ana miundombinu yao kwani zaidi ya yote Watoto wa Ukraine wanahitaji amani.