Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Viongozi wa serikali na dini lindeni waathirika wa ukatili wa dini: Guterres

Kundi la watu wakikataana na chuki na ubaguzi unaotegemea kabila na dini katika Jamhuri ya Afrika ya Kati. (2017)
OCHA/Yaye Nabo Sène
Kundi la watu wakikataana na chuki na ubaguzi unaotegemea kabila na dini katika Jamhuri ya Afrika ya Kati. (2017)

Viongozi wa serikali na dini lindeni waathirika wa ukatili wa dini: Guterres

Amani na Usalama

Hii leo dunia ikiadhimisha siku ya Kimataifa ya kuwakumbuka waathirika wa vitendo vya ukatili kutokana na dini na imani zao ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema siku hii ni maalum kwa ajili ya kutoa heshima kwa wale ambao wamepoteza maisha au ambao wameteseka kwa sababu ya kutafuta haki zao za kimsingi za uhuru wa mawazo, dhamiri, na dini au imani. 

Kupitia taarifa yake ya maadhimisho ya siku hii aliyoitoa jijini New York Marekani, Guterres amesema licha ya wasiwasi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, ambalo lilianzisha maadhimisho haya mwaka wa 2019, watu na jamii mbalimbali duniani kote wanaendelea kukabiliwa na kutovumiliana na vurugu zinazotokana na dini au imani.

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesisitiza mshikamano wangu thabiti na waathirika hao. “Matamshi ya chuki mtandaoni au nje ya mitandao ya kijamii, yanaendelea kuchochea vurugu dhidi ya wanajamii walio hatarini, ikiwa ni pamoja na makabila madogo na dini ndogo.” 

Amesisitiza ni lazima jamii nzima kufanya kazi zaidi ya kusaidia waathiriwa na kuchunguza hali zinazochochea kutovumiliana na chuki. “Juhudi kama vile Wito wangu wa Kuchukua Hatua kwa Haki za Kibinadamu na Mkakati na Mpango wa Utekelezaji wa Umoja wa Mataifa kuhusu Matamshi ya Chuki ni zana zinazoweza kutumika kushughulikia masuala haya tata na yanayosumbua.” Alisisitiza 

Dini imekuwa msaada mkubwa kwa waathirika wengi wa vita kaskazini mwa Uganda.
ICC-CPI/Pete Muller
Dini imekuwa msaada mkubwa kwa waathirika wengi wa vita kaskazini mwa Uganda.

Amekumbusha pia mataifa yana wajibu wa kuzuia na kushughulikia ubaguzi na unyanyasaji unaofanywa kwa jina la dini au imani kupitia sera za kina zinazokuza ushirikishwaji, utofauti, uvumilivu na mazungumzo ya kidini na kitamaduni.

Guterres amesema ukiukaji wa haki za binadamu unaofanywa kwa jina la dini au imani lazima uchunguzwe na kuadhibiwa, na fidia zinazofaa zinapaswa kutolewa kwa waathiriwa, kwa kufuata sheria za kimataifa za haki za binadamu. 

Amehitimisha taarifa yake kwa kuwaasa viongozi wa dini na serikali kuwa “ni muhimu Serikali zote, viongozi wa imani na watendaji wengine wenye ushawishi mkubwa kulaani uchochezi wote wa chuki na vurugu kwa misingi ya dini au imani. Juhudi za pamoja tu, za umoja na jamii nzima zinaweza kusababisha kuishi pamoja kwa usalama kwa wote na kumaliza doa hii kwenye jamii zetu.”