Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuondoka kwa nafaka Ukraine ni jambo zuri lakini vita sasa ikome – Guterres

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres (kulia) Rais Volodymyr Zelinskyy wa Ukraine (kati) na Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki wakiwa kwenye mkutano wa pamoja na waandishi wa habari mjiin Lviv Ukriane 18 Agosti 2022
UN/ Mark Garten
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres (kulia) Rais Volodymyr Zelinskyy wa Ukraine (kati) na Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki wakiwa kwenye mkutano wa pamoja na waandishi wa habari mjiin Lviv Ukriane 18 Agosti 2022

Kuondoka kwa nafaka Ukraine ni jambo zuri lakini vita sasa ikome – Guterres

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amezungumza na waandishi wa habari huko Lviv nchini Ukraine ambako pamoja na kupongeza mafanikio yatokanayo na kuanza kutekelezwa kwa makubaliano ya kusafirisha kutoka nchini humo bidhaa za nafaka na mbolea, amesema bado hatua kubwa inayotakiwa kuchukuliwa ni kumaliza vita vinavyoendelea.

Guterres amesema, chini ya mwezi mmoja meli 21 zimeondoka bandari za Ukraine zikiwa na nafaka ilhali meli 15 zimeondoka Istanbul Uturuki kuelekea Ukraine kuchukua shehena za nafaka na aina nyingine za vyakula.

“Tunavyozungumza zaidi ya tani 560,000 za nafaka na vyakula vingine kutoka kwa wakulima wa Ukraine zinaelekea soko la dunia. Na nina furaha zaidi kuwa meli iliyokodishwa na Umoja wa Mataifa ikiwa na ngano ya Ukraine inaelea Pembe ya Afrika kusaidia walio na uhitaji mkubwa kutokana na ukame,” amesema Guterres.

Zaidi ya yote, bei ya ngano ilishuka kwa asilimia 8 tu baada  ya kutiwa saini kwa mkataba wa usafirishaji nafaka kupitia Bahari Nyeusi na kipimo che bei cha shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo, FAO kilishuka kwa asilimia 9 mwezi Julai ikiwa ni mara ya kwanza tangu mwaka 2008.
Katibu Mkuu amesema hayo ni matokeo ya ushirikiano wa kimataifa, makubaliano muhimu katikati ya vita. Lakini “kwa uzoefu wangu mipango ya aina hii inakuwa hatarini kutibuliwa kwa hiyo lazima ilelewe.”

Lakini vita lazima ikome- Guterres

Katibu Mkuu amesema kitovu cha tatizo ambalo limempeleka Ukraine ni vita. Na kama alivyosema mara kwa mara uvamizi huu ni ukiukwaji wa mamlaka ya Ukraine na Katiba ya Umoja wa Mataifa.

Katibu Mkuu amesema watu wanahitaji amani, amani kwa msingi wa Chata au Katiba ya Umoja wa Mataifa. Amani kwa mujibu wa sheria za kimataifa. “Amani ambayo inaakisi matamanio ya watu duniani kote, hasa vijana, kwa ajili ya fursa na mustakabali bila ghasia.”

Amezungumzia pia mtambo wa nyuklia wa Zaporizhzhia na kusema ana hofu kubwa ya kile kinachoendelea kwenye eneo la mtambo huo.

Meli ya kwanza ya kibiashara  M/V Fulmar S, ikiwa inaelekea Ukraine kutoka Uturuki kupitia mpango wa nafaka kupitia Bahari Nyeusi.
UNOCHA/Levent Kulu
Meli ya kwanza ya kibiashara M/V Fulmar S, ikiwa inaelekea Ukraine kutoka Uturuki kupitia mpango wa nafaka kupitia Bahari Nyeusi.

Sitisheni uwepo wa wanajeshi na vifaa vya kijeshi Zaporizhzhia

“Mtambo huu haupaswi kuwa sehemu ya operesheni za kijeshi,” amesema Guterres akiongeza kuwa badala yake makubaliano yanahitajika haraka ili kuuweka mtambo wa nyuklia wa Zaporizhhia kama muundombinu wa kiraia na kuhakikisha usalama kwenye eneo hilo.

Guterres amesema wamejadiliana na shirika la Umoja wa Mataifa la nishati ya atomiki, IAEA na kwamba UN nchini Ukraine ina miundombinu ya kuweza kusaidia IAEA katika usalama wa mtambo huo iwapo Ukraine na Urusi watakubali.

Amesisitiza kuwa juhudi zote zifanyike ili mtambo huo na mazingira yake usiwe eneo lengwa la operesheni za kijeshi.

Zaidi ya yote amesema, vifaa vya kijeshi na wanawajeshi waondoke kwenye mtambo huo na hatua zozote za kupeleka majeshi au vifaa kwenye eneo hilo ziepukwe.

Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Rais Teyyip Erdoğan wa Uturuki ambapo Guterres amemshukuru Rais Zelenskyy wa Ukraine kwa mapokezi wakati huu ambapo taifa hilo linagubikwa na vita.

Urusi ilivamia Ukraine tarehe 24 mwezi Februari mwaka huu wa 2022.