Msaada ni zaidi ya vitu, hata maongezi  yanaokoa maisha

Scovia Atuhura Habibaana, mkimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC akiandaa mboga nyumbani kwake huko Hoima nchini Uganda.
UN/ John Kibego
Scovia Atuhura Habibaana, mkimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC akiandaa mboga nyumbani kwake huko Hoima nchini Uganda.

Msaada ni zaidi ya vitu, hata maongezi  yanaokoa maisha

Msaada wa Kibinadamu

Kuelekea siku ya kimataifa ya usaidizi wa kibinadamu mwaka huu wa 2022 tunamulika watu wa kawaida waliosaidiwa au kusaidia wengine, ikiwa ni kuendana na maudhui ya mwaka huu yanayomulika wale watoao misaada kwenye maeneo yao.
 

Umoja wa Mataifa kupitia ofisi yake ya kuratibu misaada ya dharura, OCHA inasema ‘yahitaji juhudi za watoa misaada ya kibinadamu kusaidia jamii inayokabiliwa na majanga.” 

Mathalani nchini Uganda, taifa la Afrika Mashariki linalopokea wakimbizi, misaada hutoka si tu kwa mashirika ya kimataifa kama yale ya Umoja wa Mataifa bali pia watu binafsi.

Wananchi wa Uganda wamenisaidia sana- Mkimbizi kutoka DRC

Elias Muzungu, mkimbizi kutoka Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC hivi sasa anaishi kwenye makazi ya wakimbizi ya Kyangwali nchini Uganda.

Elias anasema walipoingia Uganda wakikimbia machafuko DRC, mashirika ya Umoja wa Mataifa kama lile la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, na la mpango wa chakula duniani, WFP yaliwasaidia sana kuanzia usajili, malazi hadi chakula.

Lakini wananchi wa Uganda, walinisaidia sana. Wananilipia karo za masomo, sasa hivi nasoma kompyuta, niña kamera na pia wananilipia chakula.

Elias anasema kama asingalisaidiwa na wananchi wa Uganda, angalikuwa na shida sasa.
“Msaada ni kitu kizuri,” anasema Elias akieleza bayana kuwa naye amejipanga ili siku za usoni aweze kusaidia watu wengine kama alivyosaidiwa.

Msaada si tu mali bali pia maongezi-

Kwa Flavia Ajok, mkazi wa Hoima nchini Uganda, anasema watu wengi wanadhani msaada ni vitu vinavyoshikika au kuonekana kama fedha, nyumba na kadhalika.

“Kuna wakati mtu anahitaji msaada wa neno tu, anahitaji mtu wa kuzungumza naye. Mtu anaweza kutaka kujiua lakini neno moja tu likabadili msimamo wake,” amesema Flavia akihojiwa na Idhaa ya Umoja wa Mataifa.

Donata Nyirakaboozi, mkimbizi mwenye ulemavu wa kutoona anayeishi katika kambi ya Kyangwali Uganda.
UN News/ John Kibego
Donata Nyirakaboozi, mkimbizi mwenye ulemavu wa kutoona anayeishi katika kambi ya Kyangwali Uganda.

Anakumbuka wakati alikuwa na shida yake, jamaa na marafiki walifika kumpatia msaada wa mali na kuondoka. Lakini hawakutambua kuwa nilihitaji msaada wa kisaikolojia. Rafiki yangu mmoja alijrejea na kuzungumza nami kwa dakika tatu. Msaada wa kisaikolojia uliniokoa.

Flavia anasema kwa wanawake, changamoto nyingi ni za ndoa na unakutana familia ina watoto na baba haleti malezi.

“Hapa mtu akinisaidia chakula cha watoto au kuwapeleka shuleni ninashukuru sana.”

Nikiwa Tanzania nilisaidiwa malazi na kupata kazi- Mugenyi

Raia mwingine wa Uganda Idi Mugenyi anakumbuka fadhila alizotendewa nchini Tanzania akiwa mkoani Mwanza na Dar es salaam. 

Sikuwa na pahala pa kulala, “jamaa mmoja anaitwa David alinipatia malazi,” mwingine alimuonesha pahala pa kupata kazi na maisha yakaendelea vema.

“Ni vizuri sana kusaidiana hasa wakati huu ambapo uchumi ni mgumu,” amesema Bwana Mugenyi.

Umoja wa Mataifa na usaidizi

Kwa wiki moja sasa OCHA inaendesha kampeni , #ItTakesAVillage ambayo kila mtu anaweza kushiriki kwenye mtandao wa kijamii na kutoa maoni, kuchapisha au kushirikisha wengine kama njia ya kuonesha mshikamano na watu wanaohitaij msaada na shukrani kwa wale wanaoweka rehani maisha yao kusaidia wengine.

Siku ya usaidizi wa kibinadamu duniani ilitengwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 2008 kufuatia shambulio la ofisi ya makao makuu ya Umoja wa Mataifa huko Baghdad, Iraq mwaka 2003, shambulio lililoua wahudumu wa kibinadamu 22.