Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto walioathiriwa na migogoro hawawezi kusubiri elimu yao

Watoto wakicheza mchezo kwenye Kambi ya Wakimbizi wa Palestina ya Shatila huko Beirut.
© UNICEF/UN0665257
Watoto wakicheza mchezo kwenye Kambi ya Wakimbizi wa Palestina ya Shatila huko Beirut.

Watoto walioathiriwa na migogoro hawawezi kusubiri elimu yao

Utamaduni na Elimu

Kutoka Ethiopia hadi Chad na Palestina, Elimu haiwezi kusubiri au ECW , ni mradi wa Umoja wa Mataifa wa elimu katika maeneo yenye dharura na migogoro ya muda mrefu, ambao umesaidia mamilioni ya wavulana na wasichana walioathiriwa na migogoro duniani kote kutimiza ndoto zao.

ECW inawapa watoto na vijana walioathiriwa fursa ya kujifunza bila malipo kwa usalama na bila woga ili waweze kukua na kufikia uwezo wao kamili.

Akiwa na umri wa miaka tisa, Bchiote Moorice alikimbia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kutafuta usalama wake.
UNICEF Ethiopia/Eyerusalem Yitna
Akiwa na umri wa miaka tisa, Bchiote Moorice alikimbia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kutafuta usalama wake.

Akiwa na umri wa miaka tisa, Bchiote Moorice na wadogo za wakiume watatu walikimbia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, (DRC)  bila chakula, maji au mahitaji ya kimsingi.
Baada ya kutoroka kwa huzuni, Bchiote na ndugu zake waliunganishwa tena na wazazi wao, na familia nzima ilihamia kambi ya wakimbizi magharibi mwa Ethiopia.

Huko, Bchiote na wadogo zake hatimaye waliweza kupata elimu yao kupitia programu iliyofadhiliwa na ECW iliyotolewa na UNICEF Ethiopia.

"Natarajia kuhudhuria chuo kikuu mwakani na siku za usoni kufanya kazi katika benki kubwa ya biashara," alisema kwa tabasamu kubwa.

Nia ya dhati ya kupata elimu

Shahd, 11, akiwa na walimu wake wa Shule ya Determination katika hospitali ya Augusta Victoria.
Jonathan Condo/State of Palestin
Shahd, 11, akiwa na walimu wake wa Shule ya Determination katika hospitali ya Augusta Victoria.

Ulizinduliwa ili kubadilisha mfumo wa misaada ambao unatelekeza mamilioni ya watoto na vijana walio katika mazingira magumu zaidi, ECW umeweza kusaidia wavulana na wasichana wengi kama Bchiote.

Shahd (sio jina lake halisi), kama watoto wengi wa umri wake wa miaka 11, ana ndoto kubwa. Anataka kuwa rais, au daktari, au hata mwanaanga wa kwanza wa kike wa Kipalestina.

Lakini, alilazimika kutumia siku nyingi akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Augusta Victoria, ugonjwa wake sugu wa figo ulimwekea kama wingu jeusi la mvua.

Hata hivyo, Shahd ameweza kuendelea na elimu yake katika Shule ya Uamuzi  akisogea karibu zaidi na kugeuza ndoto zake kuwa kweli.

Ufadhili wa ECW umewezesha Wizara ya Elimu ya Palestina kuanzisha Shule nne za Uamuzi , ambazo hutoa elimu rahisi kwa watoto wasioweza kushiriki katika madarasa ya kawaida kwa sababu ya magonjwa sugu na matibabu ya muda mrefu.

Takriban wanafunzi 150 nchini Palestina kwa sasa wanapatiwa mipango ya kibinafsi, usaidizi wa kisaikolojia na elimu jumuishi ili kuhakikisha kwamba hawaachwi nyuma katika masomo yao.

"Ningependelea kwenda shule ya kawaida na watoto wengine, lakini walimu na wauguzi katika hospitali ni wakarimu sana, na wanafanya vizuri," alisema Shahd.

Uvumilivu, urafiki, uwezo

Hadjé, Achta na Ngoleram wameketi chini ya mti nchini Chad, wakifurahia kivuli na hewa safi kutoka ziwani.
UNICEF Chad/Nancy Ndallah
Hadjé, Achta na Ngoleram wameketi chini ya mti nchini Chad, wakifurahia kivuli na hewa safi kutoka ziwani.

Katika siku ya mwisho ya shule kabla ya kuanza likizo, marafiki watatu wasioweza kutenganishwa nchini Chad wanaonesha ushirikiano, uhusiano mwema na ustahimilivu.

Hadje Al-Hadj, Achta Dogo, na Ngoleram Abakar, wanahudhuria Shule ya Msingi ya Kaya katika Mkoa wa Lac wa Chad, na wanaishi kwenye kambi wakimbizi wa ndani ya Kaya baada ya wao na familia zao kukimbia makazi yao ya awali kutokana na vurugu zinazoendelea katika Kanda ya Ziwa Chad.

Kambi hii iliundwa mwaka 2015 kufuatia mashambulizi kutoka kwa kundi la kigaidi la Boko Haram. Vurugu za mara kwa mara na vitisho vimewalazimu zaidi ya wakimbizi wa ndani 450,000 na wakimbizi katika Mkoa wa Lac.

Hadje alikuwa na umri wa miaka mitano tu wakati familia yake ilipohamia huko kutoka nchi jirani. Sasa ama miaka 11, kupitia programu hii ameweza kuzingatia elimu yake na kufanikiwa, pamoja na wanafunzi wengine 500 kutoka kambi ya Kaya
Vijana hawa na wengine katika Shule ya Msingi ya Kaya katika Mkoa wa Lac, wameweza kufikia mazingira salama, bora ya kujifunzia kuweka ndoto zao na maisha yajayo hai.

Kufahamu kazi nyingine za ECW, bofya hapa.