Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNMISS yasaidia kuondoa maji ya Mafuriko Bentiu Sudan Kusini

Mitumbwi imekuwa njia pekee ya usafiri kwa wakazi wa Old Fangak, Sudan Kusini.
© UNHCR/Samuel Otieno
Mitumbwi imekuwa njia pekee ya usafiri kwa wakazi wa Old Fangak, Sudan Kusini.

UNMISS yasaidia kuondoa maji ya Mafuriko Bentiu Sudan Kusini

Msaada wa Kibinadamu

Walinda Amani wa Umoja wa Mataifa katika Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini UNMISS wanafanya kazi ya kuondoa maji ya mafuriko yaliyotwama katika eneo kubwa la mji wa Bentiu jimbo la UNITY ili kuhakikisha uwanja wa ndege na barabara zinazopatakana na uwanja huo zinapitika.

Helikopta ya UNMISS ikiwa angani ilifanya tathmini ya eneo lililoathirika na mafuriko katika mji wa Bentiu kufuatia mvua kubwa inayoendelea kunyeesha katika jimbo la Umoja.

Video ya UNMISS inaonesha eneo kubwa likiwa limetuama maji na wananchi wanatumia mitumbwi kwa ajili ya safari kutoka sehemu moja kwenda nyingine kutokana na eneo kubwa kutopitika.

Wahandisi wanajeshi wa Pakistan walio katika Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda Amani nchini Sudan Kusini wakiwa na mashine za kuchimba mabwawa na mashine ya kuvuta maji wanafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha angalau njia za kuingia na kutoka uwanja wa ndege zinapitika.

Watoto hutengeneza boti zao wenyewe kwa kutumia turubai na chupa za plastiki wakati wa mafuriko makubwa huko Sudani Kusini.
© UNICEF/Helene Sandbu Ryeng
Watoto hutengeneza boti zao wenyewe kwa kutumia turubai na chupa za plastiki wakati wa mafuriko makubwa huko Sudani Kusini.

Afisa anayehusika na Mafuriko katika UNMISS Meja Waqas Matloob kutoka jeshi la Pakistana anasema mpaka sasa wamefanikiwa kutengeneza zaidi ya kilometa 80 za barabara na kuvuta zaidi ya lita milioni 1.2 za maji ya mafuriko.

Lakini anasema “Changamoto bado hazijaisha. Iwapo mvua kubwa itanyesha katika sehemu za kusini na magharibi mwa Sudan Kusini hapa tunapata mafuriko au kiasi kikubwa cha maji ambacho kinahitaji kuondolewa. Ni mchakato endelevu wa kuinua tena viunga  vya mji na kuondoa maji au kufanya matengenezo ya barabara za uwanja wa ndege na maeneo yanayozunguka uwanja.”

Kwa upande wake mkuu wa ofisi ya UNMISS jimbo la Umoja, Hiroko Hirahara anasema “Zaidi ya Bentiu na Rubkona, kuna maeneo mengine mengi ya mbali, ambayo yamekumbwa na mafuriko na kama mashirika mengine ya kibinadamu hayawezi kufanya kazi hali inayoathiri wakazi wa maeneo hayo.”

Mkuu hiyo ameeleza kwa sasa, wanajeshi wa UNMISS kutoka Pakistan, Mongolia, na Ghana walioko Bentiu wanasalia katika hali ya tahadhari ili kuhakikisha wanasaidia kikamilifu na kwa haraka changamoto zozote zinazoletwa na mafuriko ikiwa ni juhudi za kulinda raia na mali zao.