Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwaka mmoja wa watalibani Afghanistan, sera dhahiri za ukosefu wa usawa zashamiri

Kituo cha uwezeshaji wanawake kwenye mji mkuu wa Afghanistan, Kabul
UN Afghanistan
Kituo cha uwezeshaji wanawake kwenye mji mkuu wa Afghanistan, Kabul

Mwaka mmoja wa watalibani Afghanistan, sera dhahiri za ukosefu wa usawa zashamiri

Wanawake

Mwaka mmoja tangu watalibani watwae madaraka nchini Afghanistan, shirika la Umoja wa Mataifa la kushughulikia masuala ya wanawake duniani, UN-Women hii leo limesihi mamlaka hizo kufungua shule kwa ajili ya watoto wote wa kike, ziondoe vikwazo vya ajira kwa wanawake na ushiriki wao kwenye siasa za taifa hilo sambamba na kufuta sera zote zinazowanyima wanawake na wasichana haki zao.

Wito huo wa UN-Women umo kwenye taarifa iliyotolewa leo jijini New York, Marekani na Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, Sima Bahaous ikitanabaisha Afghanistan, ni nchi pekee duniani ambako watoto wa kike wanauziwa kwenda shule ya sekondari.

Mwaka mmoja wa kuzima ndoto za wanawake

Bi. Bahous anasema pamoja na watoto wa kike kunyimwa kuendelea na elimu ya sekondari, hali ya wanawake na watoto wa kike katika kipindi cha mwaka huu mmoja imeendelea kuzorota kila uchao.

“Umekuwa ni mwaka wa ongezeko la ukosefu wa heshima kwa haki zao za kuishi huru na kwa usawa, wakinyimwa fursa za kujipatia kipato, kupata huduma ya afya na elimu, na kujiepusha na mazingira ya ghasia,” amesema Mkuu huyo wa UNWomen.

Amesema watalibani wametunga sera za ukosefu wa usawa ili kuigawanya Afghanistan, “hakuna wanawake kwenye Baraza la Mawaziri, hivyo kuengua wanawake kwenye ushiriki wa siasa. Wanawake, wengi wao hawaruhusiwi kufanya kazi nje ya nyumbani na wanatakiwa kuziba nyuso zao kwenye maeneo ya umma.”

Wanawake wakipokea mgao wa chakula katika eneo la usambazaji wa chakula huko Herat, Afghanistan.
© UNICEF/Sayed Bidel
Wanawake wakipokea mgao wa chakula katika eneo la usambazaji wa chakula huko Herat, Afghanistan.

Kutenga wanawake kunaathiri taifa zima

Amefafanua kuwa kuwatenga wanawake dhidi ya fursa zote za maisha kunawapora wananchi wa Afghanistan nusu ya vipaji na nguvu kazi.

Ametoa wito kwa mamlaka pia kuhakikisha wanawake waandishi wa habari, watetezi wa haki za binadamu na wanaojihusisha na masuala ya kiraia waruhusiwe kuwa huru kujieleza, kupata taarifa na kufanya kazi bila uoga.

“Msaada kutoka jamii ya kimaifa kwa haki za wanawake Afghanistan na uwekezaji kwa wanawake wenyewe ni muhimu kuliko wakati wowote,” amesema Bi. Bahous huku akisisitiza kuwa shirika lake litaendelea kusalia Afghanistan kama ilivyokuwa kipindi chote cha mwaka huu mzima kwa kuwa kinachofanyika katika taifa hilo ni wajibu wa dunia nzima kuchukua hatua.