Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwaka mmoja wa kuengua watoto wa kike kwenye elimu Afghanistan, kwagharimu dola milioni 500

Wasichana katika kituo cha kujifunzia katika Kijiji cha Gulab Khail katika Mkoa wa Maidan Wardak, Afghanistan.
© UNICEF/Azizzullah Karimi
Wasichana katika kituo cha kujifunzia katika Kijiji cha Gulab Khail katika Mkoa wa Maidan Wardak, Afghanistan.

Mwaka mmoja wa kuengua watoto wa kike kwenye elimu Afghanistan, kwagharimu dola milioni 500

Utamaduni na Elimu

Mwaka mmoja tangu watalibani wachukue madaraka nchini Afghanistan, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto, UNICEF, limesema kitendo cha Watoto wa kike kuenguliwa kwenye masomo kimegharimu asilimia 2.5 la pato la ndani la taifa hilo la barani Asia.

Uchambuzi mpya uliotolewa na UNICEF hii leo unabainisha kuwa iwapo kundi rika la sasa la watoto wa kike milioni tatu lilangaliweza kumaliza elimu ya sekondari na kuingia katika soko la ajira, Watoto wa kike na wanawake wangalichangia angalatu dola bilioni 4 kwenye uchumi wa Afghanistan.
 
Taarifa ya UNICEF iliyotolewa leo Kabul nchini Afghanistan inamnukuu Mwakilishi wa UNICEF nchini humo, Dkt. Mohamed Ayoya anasema “uamuzi wa tarehe 23 mwezi Machi mwaka huu wa kutoruhusu Watoto wa kike kurejea shule za sekondari ulikuwa wa kushtusha na wa kukatisha tamaa.”

Haki ya msingi ya mtoto wa kike imekiukwa

Dkt. Ayoya amesema uamuzi huo si tu kwamba unakiuka haki ya msingi ya elimu kwa mtoto wa kike, bali pia unawaweka katika kiwewe kikubwa, na hatari ya kutumikishwa na kunyanyaswa, ikiwemo usafirishaji haramu wa Watoto, na ndoa za utotoni. “Sasa huu uchambuzi mpya unadhihirisha wazi madhara ya uamuzi huu kwenye pato la ndani la taifa.”

Sasa huu uchambuzi mpya unadhihirisha wazi madhara ya uamuzi huu kwenye pato la ndani la taifa- Dkt. Mohamed Ayoya, Mwakilishi wa UNICEF, Afghanistan

Makadirio ya UNICEF katika uchambuzi huu, hayakujumuisha madhara yasiyo ya kifedha ya kumnyima mtoto wa kike haki ya elimu, kama vile uhaba unaotarajiwa wa walimu, madaktari na wauguzi wa kike, na matokeo ya ongezeko la Watoto wa kike wasiohudhuria shule ya msingi na ongezeko la gharama ya kiafya kutokana na ujauzito miongoni mwa barubaru.

Ni sawa na kuongeza ‘chumvi kwenye kidonda’

“Makadirio hayo pia hayajatilia maanani manufaa mapana ya elimu ikiwemo mafanikio ya kielimu, kupungua kwa ndoa za utotoni na vifo vya Watoto wa changa,” imesema taarifa hiyo.

Hata kabla ya watalibani kutwaa madaraka tarehe 15 mwezi Agosti mwaka jana, Afghanistani ilikuwa inahaha ikiwa na watoto zaidi ya milioni 4.2 wasiokuweko shuleni; asilimia 60 wakiwa ni watoto wa kike.

Kutosomesha mtoto wa kike ni gharama zaidi

UNICEF inasema ijapokuwa gharama za kutosomesha watoto wa kike na wa kiume ni kubwa kwa kuzingatia kipato kinachopotea, kutosomesha mtoto wa kike ni gharama zaidi kwa sababu ya uhusiano kati ya mafanikio ya kielimu na kucheleweshwa kwa ndoa za utotoni na kupata watoto mapema, kushiriki kwenye nguvu kazi, kufanya uchaguzi sahihi kwa ajili ya mustakabali wao na kuwekeza Zaidi kwenye afya na elimu kwa ajili ya watoto wao siku za usoni.

Uchambuzi unadokeza kuwa Afghanistani haitoweza kurejesha kile ilichopoteza kama pato la ndani la taifa wakati wa kipindi hiki cha mpito na kufikia ustawi sasa bila kukidhi haki ya mtoto wa kike ya kupata elimu ya sekondari.

UNICEF inamulika pia afya ya mwili

Kwa sasa, UNICEF inahaha kufikia barubaru wa kike huduma muhimu wanazohitaji kama vile kinga dhidi ya ukosefu wad amu mwilini, kuwasaidia na afya ya hedhi salama na huduma za kujisafi.

Shirika hilo pia linatoa huduma za kuzuia utapiamlo miongoin mwa watoto ambapo katika miezi 12 iliyopita, huduma za afya na lishe shuleni zimefikia barubaru wa kike 272,386 sambamba na vidonge vya kuongeza damu mwilini.