Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zaidi ya wahudumu wa kibinadamu 140 waliuawa mwaka jana, wengi wao wa kitaifa

Anita, mkimbizi huyu wa ndani, hupeleka watoto wake mapacha kila wakati kwenye kituo cha afya cha Tchanga Tchanga ili kutambua hali yao ya lishe na hii ni kwa msaada wa Mfuko wa kibinadamu wa Africa Medicine nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
UNOCHA/Wassy Kambale
Anita, mkimbizi huyu wa ndani, hupeleka watoto wake mapacha kila wakati kwenye kituo cha afya cha Tchanga Tchanga ili kutambua hali yao ya lishe na hii ni kwa msaada wa Mfuko wa kibinadamu wa Africa Medicine nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Zaidi ya wahudumu wa kibinadamu 140 waliuawa mwaka jana, wengi wao wa kitaifa

Msaada wa Kibinadamu

Kuelekea siku ya usaidizi wa kibinadamu duniani tarehe 19 mwezi huu wa Agosti, Umoja wa Mataifa leo umesema kadri majanga yanavyozidi kuongezeka duniani maisha ya watoa misaada yako hatarini zaidi na kwamba mwaka jana pekee wa 2021 wahudumu zaidi ya 140 wa kiutu waliuawa duniani kote.

Taarifa ya ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya dharura, OCHA iliyotolewa leo New York, Marekani na Geneva, Uswisi inasema ni kwa kuzingatia hilo ndio maana leo inazindua kampeni ya wiki moja ya ushirikiano na watoa huduma za kiutu. Kampeni hiyo iliyopatiwa jina #ItTakesAVillage ikienda na msemo yahitaji Kijiji au jamii kulea mtoto, OCHA inasema inahitaji jamii ya watoa huduma za kibinadamu kwenye maeneo yenye mizozo ili kupeleka matumiani na misaada kwa wale walio kwenye shida. Ikichambua idadi ya waiokufa au kujeruhiwa wakitoa huduma za kiutu, OCHA inasema zaidi ya watoa huduma za kiutu 460 walishambuliwa mwaka jana ambapo kati yao 140 ndio waliuawa, idadi ambayo ni kubwa tangu mwaka 2013. Wahudumu wa kitaifa wako hatarini zaidi “Wote waliouawa walikuwa ni wafanyakazi wa kitaifa isipokuwa wawili pekee,” imesema taarifa hiyo ikiangazia changamoto wanazopata wahudumu wa kiutu kutoka nchi wanamohudumia. Katika kipindi hicho wahudumu wengine 117 walitekwa nyara. Mwaka huu pekee, wahudumu 168 wa kibinadamu wameshambuliwa na kati yao 44 wameuawa, imesema taarifa hiyo. “Mahitaji ya kibinadamu ni ya juu kuliko wakati wowote ule na wahudumu wa kibinadamu wanafanya kazi kwenye mazingira magumu zaidi,” amesema Martin Griffiths, Mkuu wa OCHA. Ni kwa mantiki hiyo anasema, “tunapoelekea kusherehekea siku ya kiutu mwaka huu, tunatoa shukrani kwa wahudumu wote wa kibinadamu ambao mara nyingi wanafanya kazi kwenye mazingira magumu kusaidia wengine, na tunakumbuka pia waliopoteza maisha yao wakiwa kazini.” Bwana Griffiths amesema siku ya kiutu duniani mwaka huu inajijenga katika msemo kuhusu juhudi za pamoja na kutoa wito kwa watu kokote waliko washukuru kazi ya kiutu inayofanywa na mtu yeyote yule. Hata wewe unaweza kushiriki kampeni Watu kokote waliko wanaweza kushiriki kampeni hii ya wiki moja kwa kutumia neno #ItTakesAVillage kwenye mtandao wa kijamii na kutoa maoni, kuchapisha au kushirikisha wengine kama njia ya kuonesha mshikamano na watu wanaohitaij msaada na shukrani kwa wale wanaoweka rehani maisha yao kusaidia wengine. Siku ya usaidizi wa kibinadamu duniani ilitengwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 2008 kufuatia shambulio la ofisi ya makao makuu ya Umoja wa Mataifa huko Baghdad, Iraq mwaka 2003, shambulio lililoua wahudumu wa kibinadamu 22.