Baada ya zaidi ya nusu karne ya kutokuwa na utaifa, Washona wapiga kura kwa mara ya kwanza Kenya
Baada ya zaidi ya nusu karne ya kutokuwa na utaifa, Washona wapiga kura kwa mara ya kwanza Kenya
Wakati raia wengine wa Kenya wakisubiri historia ya kumshuhudia Rais wa 5 wa nchi hiyo ya Afrika Mashariki, watu jamii ya Shona waliowasili Kenya mwanzoni mwa miaka ya 1960 wakitokea Zimbabwe wakieneza dini na wakiwa vijakazi wa waingereza hatimaye wameonja moja ya faida za uraia kwa kupiga kura kwa mara ya kwanza kwani tangu Kenya ilipopata uhuru mwaka 1963.
Washona walifika Kenya mwaka wa 1960 na kuishi kama watu wasio na utaifa kwa karibu miongo sita hadi, Julai 28, 2021, walipotambuliwa kama kabila la 45 la Kenya. Wakiwa na stakabadhi zote zinazohitajika, walijiandikisha kupiga kura, na hatimaye, Jumanne, Agosti 9, 2022 Washona, waliotoka Zimbabwe, walipiga kura kwa mara ya kwanza kama raia wa Kenya.
"Ilikuwa safari ndefu kwetu kama watu. Bila cheti cha kuzaliwa na kitambulisho cha kitaifa, si rahisi kufanya kazi katika nchi. Tunashukuru sana Serikali ya Kenya kwa kututambua kama jamii," anasema Benjamin Muregerera, kiongozi wa Jumuiya ya Washona. Alikua raia kamili wa Kenya wakati Rais Uhuru Kenyatta alipowatambua kama kabila la 45 ya nchi hiyo.
Washona walifika Kenya kutoka Zimbabwe kama wamishonari wa Kikristo katika miaka ya 1960. Walibeba pasipoti za Uingereza na walisajiliwa kama raia wa Uingereza.
Baada ya uhuru wa Kenya mwaka wa 1964, Washona walikuwa na nafasi ya miaka miwili kusajiliwa kama Wakenya, jambo ambalo wengi walikosa. Pia, hawakuweza kujiandikisha walikotoka kwa sababu hawakuwa tena raia wa nchi walikozaliwa, hivyo kuwafanya wasiwe na utaifa.
Kutokuwa na utaifa sio utambulisho mzurikuishi nao. Kimsingi, inakataza mtu kupata kile ambacho raia wanakichukulia kuwa haki za kuzaliwa. Ukosefu wa kitambulisho cha kitaifa, hati moja muhimu zaidi ambayo raia yeyote lazima awe nayo ili kupata huduma, ni kilema kikubwa. Alipoulizwa ni changamoto zipi walizokabiliana nazo kabla ya Utambulisho Muregerera, anayefahamika kwa jina la 'Mhofu' (jina la ukoo) alisema karibu kila biashara inahitaji kitambulisho cha taifa ambacho Jamii yake haikuwa nacho. Ilikuwa vigumu kwa Jamii iliposimamishwa na polisi kwa sababu hawakuwa na kitambulisho cha taifa. Baadhi walikamatwa kwa kukosa vitambulisho, na jaribio la kuwafukuza nchini lilisaidia kukutana na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR ambalo liliwasaidia kutatua hali yao ya kutokuwa na utaifa hadi kutambuliwa kwao mwaka 2021.
Wanachama wa Jamii ya Washona waliweza tu kuhudhuria shule hadi shule ya upili (sekondari) lakini walipata changamoto za kuingia katika elimu ya juu ambapo hati za utambulisho ni za lazima. Kutambuliwa kwa Jamii yao kama sehemu ya Kenya sasa kumeondoa mkwamo huo.
Kanisa la The Gospel of God Church yaani Kanisa la Injili ya Mungu ni kanisa la wamisionari la watu wa Shona ambalo Baba Joanne alianzisha. Bwana. Muregerera, aliyezaliwa nchini Kenya, ni kizazi cha kwanza cha Washona, na anafurahi kuwa amebeba kitambulisho cha kitaifa ambacho kina jina la baba yake, anasema, "siwezi kukuambia jinsi mimi na jamii yangu tunavyojisikia.”
Tangu kutambuliwa kwao, angalau wanajamii 5,000 wa jamii ya Washona wametuma maombi na kupokea vitambulisho vya Kenya huku wanajumuiya 1,649 wa jamii ya Washona, ambao walikuwa hawana utaifa wakiwa tayari wamekabidhiwa vyeti vya uraia.
Kijana mmoja aliyezaliwa mwaka 1990, Chinyanga aanasema vitambulisho hivyo ni nyenzo muhimu kwa urithi wao kwa sababu watoto wao watajua walikotoka kwa sababu watakuwa wamebeba jina lao la asili la Zimbabwe.
Washona wameishi bega kwa bega na wenyeji, na wanazungumza Kishona chao kwa ufasaha na lugha za kienyeji, ikiwa ni pamoja na Kiswahili. Wanasema hawakuwahi kukumbana na chuki na wakazi wa eneo hilo na wameoana na Wakenya ambao wamejiunga na imani yao.
Kuna zaidi ya Washona 5,000 waliosambaa katika wakazi wote wa Kenya huko Kiambu, Meru, Embu, Laikipia, Kericho, Narok, Kajiado, Mombasa na Malindi.