Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vizazi vyote tuungane kuwasaidia vijana : Guterres

Nchini Sudan, vijana walikusanyika El Fasher, Darfur Kaskazini, katika Siku ya Kimataifa ya Vijana.
UNAMID/Amin Ismail
Nchini Sudan, vijana walikusanyika El Fasher, Darfur Kaskazini, katika Siku ya Kimataifa ya Vijana.

Vizazi vyote tuungane kuwasaidia vijana : Guterres

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Ikiwa leo ni siku ya vijana duniani, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito kwa jamii kuwasaidia vijana kwa kuwekeza kwenye kuwapatia elimu na kuwajengea uwezo wa kiujuzi kupitia mikutano pamoja na kufanya mabadiliko katika mifumo ya elimu.

Vijana, ni nusu ya wakazi wote duniani tena wakiwa na umri wa miaka 30 au chini ya hapo, na idadi hii inatarajiwa kufikia asilimia 57 ifikapo mwishoni mwa mwaka 2030. 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres anatuma ujumbe kwa jamii kwamba pamoja na kuwekeza katika kundi hili katika jamii, lakini pia jamii inapaswa kuunga mkono usawa wa kijinsia na fursa zinazotolewa zihakikishe zinawashirkisha vijana iwe ni maisha ya kiraia au hata yale ya kisiasa.

“Haitoshi kuwasikiliza tu vijana, tunahitaji kuwajumisha katika mifumo ya kufanya maamuzi katika ngazi za ndani, kitaifa kwa kimataifa kwani hiki ndicho kiini cha pendekezo letu la kuanzisha Ofisi ya Vijana katika Umoja wa Mataifa.” Amesema Guterres 

Vijana wafanyao kazi kwenye boti hiyo Uto ni Yalo wakiandaa kung'oa nanga kwenye mji mkuu Suva nchini Fiji ili kusambaza vifaa vya misaada kufuatia kimbunga kilichopiga nchi hiyo mwaka 2018
Uto ni Yalo Trust/Samuela Ulacake
Vijana wafanyao kazi kwenye boti hiyo Uto ni Yalo wakiandaa kung'oa nanga kwenye mji mkuu Suva nchini Fiji ili kusambaza vifaa vya misaada kufuatia kimbunga kilichopiga nchi hiyo mwaka 2018

Akiweka msisitizo katika kauli mbiu ya mwaka huu inayosema “Mshikamano wa vizazi kuunda ulimwengu wa vizazi vyote Mkuu huyo wa umoja wa Mataifa anasema “Katika siku hii muhimu, hebu tuungane vizazi vyote ili kuvunja vizuizi na tufanye kazi kama kitu kimoja ili kufikia ulimwengu ulio na usawa zaidi, wa haki na unajumuisha watu wote.”

Amefafanua vizuizi hivyo mara nyingi huwa ni ubaguzi wa umri, upendeleo na ubaguzi mwingine wa aina yoyote ambao unawatupa nje vijana kwenye maeneo ya kufanya maamuzi kuhusu Maisha yao. 

Ametolea mifano maeneo hayo kuwa ni pamoja na  masuala ya janga la COVID-19, Mabadiliko ya tabianchi, umasikini, ukosefu wa usawa na hata migogoro mingine yoyote inayokwamisha kufikiwa kwa Malengo ya Maendeleo Endelevu na kujenga mustakabali bora na wenye amani zaidi ambao dunia nzima inatafuta kufikia. 

Amesisitiza kushirisha marika yote “ni muhimu zaidi sasa kuliko hapo awali kwani ulimwengu unakabiliwa na msururu wa changamoto zinazotishia mustakabali wetu wa pamoja.”