Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umoja wa Mataifa wasikitishwa na mauaji ya watoto katika ukanda wa Gaza

Watoto waliwa katika ukanda wa Gaza tarehe 8 Agosti 2022
Ziad Taleb
Watoto waliwa katika ukanda wa Gaza tarehe 8 Agosti 2022

Umoja wa Mataifa wasikitishwa na mauaji ya watoto katika ukanda wa Gaza

Amani na Usalama

Kamishna Mkuu wa Haki za Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet leo ameelezea kusikitishwa kwake na idadi kubwa ya Wapalestina, wakiwemo watoto, waliouawa na kujeruhiwa katika ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu mwaka huu, ikiwa ni pamoja na uhasama mkali unaoendelea kati ya Israel na makundi ya wapalestina wenye silaha huko Gaza mwishoni mwa juma lililopita.

Taarifa iliyotolewa leo kutoka Geneva Uswisi imemnkuu kamishna Mkuu Michelle Bachelet akieleza takwimu kuwa wiki iliyopita, watoto 19 wa Kipalestina wameuawa katika ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu, na kupelekea idadi ya vifo tangu kuanza kwa mwaka hadi 37. Watoto kumi na saba waliuawa wakati wa mapigano ya Gaza kuanzia tarehe 5-7 Agosti, na wengine wawili waliuawa mnamo Agosti 9.

"Kuumiza mtoto yeyote wakati wa vita kunasumbua sana, na mauaji na ulemavu wa watoto wengi mwaka huu ni jambo lisiloeleweka," alisema Bachelet.

Ofisi ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa imethibitisha kuwa kati ya Wapalestina 48 waliouawa, kulikuwa na raia wasiopungua 22, wakiwemo watoto 17 na wanawake wanne. Hali ya wengine 22 bado haijabainishwa. 

Kati ya Wapalestina 360 walioripotiwa kujeruhiwa, karibuni  theluthi mbili walikuwa raia, wakiwemo watoto 151, wanawake 58 na wazee 19. Katika matukio kadhaa, watoto walikuwa wengi wa majeruhi.

Mashambulio kadhaa ya Israeli yalilipua maeneo ya kiraia na kusababisha vifo vya raia na uharibifu wa mali za raia.

"Sheria ya kimataifa ya haki za binadamu iko wazi. Kuanzisha shambulio ambalo linaweza kutarajiwa kuua au kuumiza raia kwa bahati mbaya, au kuharibu mali za raia, kwa njia isiyolingana na madhubuti na faida ya moja kwa moja ya kijeshi inayotarajiwa, ni marufuku. Mashambulizi kama haya lazima yakome,” alisema Bachelet.

Mtoto amesimama kwenye vifusi vya nyumba yake huko Gaza.
Ziad Taleb
Mtoto amesimama kwenye vifusi vya nyumba yake huko Gaza.

Ukiukwaji wa sheria za kimataifa

Kwa kukiuka sheria za kimataifa za kibinadamu, taarifa hiyo imeeleza pia makundi yenye silaha ya Palestina yalirusha mamia ya roketi na makombora katika mashambulizi ya kiholela, na kusababisha vifo vya raia na uharibifu wa vitu vya kiraia nchini Israel na Gaza.

Kulingana na mamlaka ya Israeli, jumla ya Waisraeli 70 walijeruhiwa.

Kamishna Mkuu huyo ameitoa wito wa uchunguzi wa haraka, huru, usio na upendeleo, wa kina na wa uwazi kufanyika katika matukio yote ambapo mtu yeyote aliuawa au kujeruhiwa.

Kamishna huyo wa Haki za binadamu amesema ni  “kama hakuna uwajibikaji kabisa katika ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu iwe kwa ukiukaji wa sheria za kimataifa za kibinadamu na pande zote za uhasama huko Gaza, au kwa ukiukwaji wa mara kwa mara wa sheria za kimataifa za haki za binadamu za Israeli na sheria ya kukalia kwa mabavu katika Ukingo wa Magharibi, ikiwa ni pamoja na Jerusalem Mashariki kwani kumeendelea kutokea matukio ya matumizi ya nguvu yasiyo ya lazima na yasiyo na uwiano.”

Amesema hali hiyo ya kutokujali, pamoja na ukiukwaji wa muda mrefu, huchochea mzunguko wa vurugu na kujirudia kwa ukiukaji.

"Hali ya Palestina ni tete sana, na matukio kama vile Nablus yanahatarisha kuchochea uhasama zaidi huko Gaza. Kujizuia kabisa ni muhimu ili kuzuia umwagikaji zaidi wa damu, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa bunduki zinatumika kwa kufuata viwango vya kimataifa”.