Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Liberia yapiga hatua! Mtoto anaweza kuchukua uraia wa mama, UNHCR yapongeza

Nenbo la kampeni ya I Belong ya kuchagiza kuhusu umuhimu wa utaifa kwa watu ambao wanakabiliwa na changamoto hiyo
UNHCR
Nenbo la kampeni ya I Belong ya kuchagiza kuhusu umuhimu wa utaifa kwa watu ambao wanakabiliwa na changamoto hiyo

Liberia yapiga hatua! Mtoto anaweza kuchukua uraia wa mama, UNHCR yapongeza

Haki za binadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limepongeza Liberia kwa marekebisho makubwa ya kisheria ambayo sasa yanawezesha mtoto kuchukua uraia wa mama tofauti na awali ambapo mtoto alilazimika kuchukua uraia wa baba pekee, moja ya sababu ya watu kutokuwa na utaifa.

Taarifa ya UNHCR iliyotolewa leo jijini Geneva, Uswisi inasema, “katika maendeleo makubwa ya kuzuia ukosefu wa utaifa, Liberia imerekebisha sheria yake ya utaifa na kupatia wanawake na wanaume haki sawa ya kupatia watoto wao utaifa wao.”

Rais wa Liberia, George Weah, alitia saini kuwa sheria muswada wa mabadiliko ya sheria ya Utaifa na Ukazi tarehe 5 mwezi huu wa Agosti, na kuondoa vipengele vya kibaguzi vinavyozuia watoto kuchukua utaifa wa mama zao.

Bado kuna nchi 24 ambako wanawake ‘mwiko’ kupatia watoto utaifa wao

“Tunapongeza Liberia kwa hatua hii ya kihistoria ya kuondoa kikwazo cha kijinsia katika utaifa. Ubaguzi wa kijinsia katika utaifa unasalia kuwa sababu kubwa ya ukosefu wa utaifa miongoni mwa watoto, na hatua hii ni kauli nzito ya ahadi ya Liberia katika kutatua suala hili,” amesema Gillian Triggs, Naibu Kamishna Mkuu wa UNHCR akihusisha na ulinzi.

Liberia ni nchi ya tatu kurekebisha sheria na kupatia wanawake na wanaume haki sawa ya kupatia watoto wao utaifa wao tangu kuanza kwa kampeni ya #Miminiwa #IBelong mwaka 2014 inayolenga kutokomeza ukosefu wa utaifa ifikapo mwaka 2024. Mataifa mengine ni Madagascar na Sierra Leone.

UNHCR imesema itaendelea kushirikiana na serikali kutokomeza ukosefu wa utaifa na kutatua vynazo vyake.

Hadi sasa kuna mataifa 24 duniani kote ambayo hadi leo hii wanawake hawaruhusiwi kupatia watoto wao utaifa wao.

Ukosefu wa utaifa unaathiri mamilioni ya watu duniani, “bila utaifa, wanashindwa kupata haki za kisheria, halikadhalika nyaraka za kupata huduma muhimu ikiwemo elimu, afya na chanjo. Ukosefu wa utaifa unaathiri ngazi zote za maisha kuanzia kuzaliwa hadi kifo,” imesema UNHCR.