Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umoja wa Mataifa wataka kusitishwa mapigano karibu na kiwanda cha nyuklia nchini Ukriane

Kituo cha kuzalisha umeme cha Dnieper huko Zaporizhzhia, Ukraine.
Unsplash/Yehor Milohrodskyi
Kituo cha kuzalisha umeme cha Dnieper huko Zaporizhzhia, Ukraine.

Umoja wa Mataifa wataka kusitishwa mapigano karibu na kiwanda cha nyuklia nchini Ukriane

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameeleza kuwa na wasiwasi mkubwa kwa hali inayoendelea ya mapigano ndani na karibu na kiwanda cha nyuklia cha Zaporizhzhia kilichoko kusini mwa nchi ya Ukriane. 

Taarifa ya Mkuu huyo wa UN imetolewa leo jijini New York Marekani wakati ambapo badala ya kupungua kwa mapigano kwa siku kadhaa zilizopita, kumekuwa na taarifa za matukio ya kutisha ambayo inaelezwa iwapo yataendelea kuna uwezekano mkubwa wa kuleta maafa.

“Ninatoa wito kwa watu wote wanaohusika kutumia akili na watafute sababu za kutochukua hatua zozote zinazoweza kuhatarisha uadilifu wa kimwili, usalama kwa ujumla na usalama wa kinu cha nyuklia ambacho ni kukubwa zaidi barani ulaya” amesema Guterres 

Guterres ameeleza uharibifu wowote utakaotokea katika kiwanda hicho hauta athiri Ukriane pekee bali unaweza sababisha janga kwa maeneo mengine ya karibu katika ukanda huo na kwingineko hali ambayo haikubaliki ndio maana ametoa wito wa kusitishwa mara moja kwa shughuli za kijeshi katika maeneo ya karibu na mtambo huo na kuacha kulenga vifaa vilivyokaribu na mazingira yake. 

“Ninahimiza kuondolewa kwa wanajeshi na vifaa vyovyote kwenye mtambo huo na kuepuka kupeleka vifaa zaidi au vikosi kwenye eneo hilo. Kituo hicho hakipaswi kutumika kama sehemu ya operesheni yoyote ya kijeshi.” 

Baada ya kuondoa vikosi vya kijeshi katika eneo hilo ameshauri pia kufanyike makubaliano ya haraka katika ngazi za kiufundi kwenye eneo lenye usalama ili kuhakikisha usalama wa eneo hilo la kiwanda. 

Katika taarifa hiyo Guterres amewashakikishia kuwa Umoja wa Mataifa unaendelea kuunga mkono kikamilifu kazi zinazofanywa na shirika la Kimataifa la nguvu za atomiki IAEA na juhudi zake za kuhakikisha kuna utendaji kazi salama katika kiwanda hicho cha Zaporizhzhia. 

“Ninahimiza wahusika wote kutoa ushirikiano kwa IAEA kwa haraka, usalama na bila kuweka vizuizi katika eneo hilo la kiwanda” alieleza wakati akihitimisha taarifa yake.