Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakimbizi wa ndani nchini Somalia wafikia milioni moja

Mgogoro mkubwa wa maji umekumba sehemu kubwa ya Somalia baada ya mvua kutonyesha kwa misimu kadhaa
United Nations
Mgogoro mkubwa wa maji umekumba sehemu kubwa ya Somalia baada ya mvua kutonyesha kwa misimu kadhaa

Wakimbizi wa ndani nchini Somalia wafikia milioni moja

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR nchini Somalia limesema kiwango cha ukame nchini humo sio cha kawaida na kwamba kimesababisha idadi ya watu waliosajiliwa kuwa wakimbizi wa ndani kutokana na ukame kufikia milioni Moja, idadi ambayo ni ya juu. 

Takwimu hizo mpya zimetolewa na UNHCR na Baraza la Wakimbizi la Norway, NRC ambapo taarifa ya UNHCR iliyotolewa mjini Mogadishu Somalia hii leo inasema idadi hiyo ni kengele ya dharura na kwamba baa la njaa linanyemelea Somalia nzima hivyo msaada wa fedha unahitajika haraka ili kufikisha mahitaji bila kuchelewa.

Mwakilishi wa NRC nchini Somalia Mohammed Abdi amesema ni vyema msaada ukatolewa bila kuchelewa “Tumeona watu zaidi na zaidi wakilazimika kukimbia makazi yao na kuacha kila kitu chao nyuma kwasababu hakuna maji wa chakula kilichobaki huko vijijini” 

Somalia inashuhudia mwaka wa pili mfukulizo wa ukame mkali hali ambayo inaelezwa haijawahi kutokea tangu miaka 40 iliyopita. 

Taaarifa hiyo iliyotolewa leo imeeleza kuongezeka huku kwa wakimbizi wa ndani kutokana na uhaba wa chakula nchini Somalia kunatarajiwa kuongezeka kutoka takriban watu milioni 5 mpaka kufikia milioni 7 katika miezi ijayo. Hali hii inachochewa pia na mabadiliko ya tabianchi, kuongezeka kwa bei za chakula na vita nchini Ukraine. 

Muonekano wa kambi ya wahamiaji wa ADC ambayo kwa sasa inawakaribisha wakimbizi wapya wanaowasili  Baidoa, Somalia.
UN Photo/Fardosa Hussein
Muonekano wa kambi ya wahamiaji wa ADC ambayo kwa sasa inawakaribisha wakimbizi wapya wanaowasili Baidoa, Somalia.

Mwakilishi wa UNHCR nchini Somalia Magette Guise amesema nchi hiyo tayari ilikuwa inakabiliwa na uhaba wa fedha hata kabla ya mzozo wa hivi karibuni “Jumuiya zilizo katika mazingira magumu ndizo zilizoathirika zaidi na athari mabadiliko ya tabianchi hali iliyoacha familia nyingi bila ulinzi na kuongeza wakimbizi wa ndani” 

Nawanaofika katika kambi za misaada wanasema “wale walioachwa nyuma hawana chaguo lolote, ni suala la muda kabla hawajapoteza Maisha” kama alivyoeleza Hussein mzee wa miaka 80 aliyewasili katika kambi yeye na familia yake. 

UNHCR mwezi June mwaka huu ilitoa ombi la dola milioni 9.5 ikiwa ni sehemeu ya ombi la kusaidia kanda ya Afrika ambayo imeshuhudia ongezeko kubwa la wakimbizi wa ndani kutokana na ukame. 

Shirika hilo limeeeleza kwa sasa wao na washirika wao wa masuala ya kibinadamu wanafanya yale yanayowezekana kulingana na rasilimali zilizopo kutokidhi mahitaji, na wameomba jumuiya za kimataifa kujitolea zaidi ili kuwezesha kuokoa maisha.