Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ajira kwa vijana duniani inasuasua; hali ngumu zaidi kwa vijana wa kike- ILO

Viki Bokanda, ingawa ni mvulana mwenye umri wa miaka 15 anajifunza  ushoni kwenye kituo cha mafunzo stadi kwa wasichana  huko Kisangani, Kaskazini magharibi mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.
© UNICEF/UN0507530/Frank Dejongh
Viki Bokanda, ingawa ni mvulana mwenye umri wa miaka 15 anajifunza ushoni kwenye kituo cha mafunzo stadi kwa wasichana huko Kisangani, Kaskazini magharibi mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.

Ajira kwa vijana duniani inasuasua; hali ngumu zaidi kwa vijana wa kike- ILO

Ukuaji wa Kiuchumi

Suala la vijana kupata ajira tena kujikwamua kutoka hali ngumu ya maisha baada ya janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19 limeendelea kusuasua, imesema ripoti mpya ya shirika la Umoja wa Mataifa la kazi duniani, ILO iliyotolewa leo kuelekea siku ya vijana hapo kesho, ambapo shirika hilo linasema hali hiyo inathibitisha kuwa COVID-19 iliathiri zaidi vijana kuliko marika mengine, vijana wa kike wakiathirika zaidi.
 

Ikipatiwa jina  Mwelekeo wa Ajira kwa Vijana 2022: Kuwekeza katika kurekebisha mustakabali wa vijana ripoti inabaini kuwa janga la COVID-19 limeongeza mkwamo zaidi kwenye soko la ajira hasa kwa vijana wenye umri wa kati ya miaka 15 hadi 24 ambao ndio walipoteza zaidi ajira kuliko watu wazima kuanzia mapema 2020.

Takwimu zinasemaje?

Ripoti inasema kiwango cha vijana wasio kwenye ajira, elimu au mafunzo kwa mwaka 2020 kiliongezeka kwa asilimia 23.3,ikiwa ni ongezeko la asilimia 1.5 kutoka mwaka 2019, kiwango ambacho hakijaonekana katika kipindi cha miaka 15.

Idadi ya vijana wasio na ajira duniani inakadiriwa kufikia milioni 73 mwaka huu wa 2022, ikiwa ni nafuu kidogo kuliko mwaka 2021 ambapo idadi ilikuwa milioni 75, lakini ripoti inasema ni ongezeko kwa vijana milioni Sita ikilinganishwa na kabla ya COVID-19 mwaka 2019.

Pengo la kijinsia

Vijana wa kike hali ni ngumu zaidi,” inasema ripoti ikionesha kuwa mwaka huu wa 2022 makadirio ya vijana wa kike watakaokuwa kwenye ajira ni asilimia 27.4 ikilinganishwa na vijana wa kiume asilimia 40.3.

“Hii ina maana vijana wa kiume wana nafasi mara 1.5 ya kuajiriwa kuliko vijana wa kike,” imesema ripoti hiyo ikitanabaisha kuwa, pengo la kijinsia ambalo limeonesha dalili ndogo sana kuzibika katika miongo miwili iliyopita, ni kubwa zaidi katika nchi za kipato cha chini na cha kati ikilinganishwa na zile za kipato cha juu.

“Wanachohitaji zaidi vijana ni mfumo wa soko la ajira ufanyao kazi na wenye fursa za ajira za kiutu kwa wale walioko kwenye soko, sambamba na elimu bora na fursa za mafunzo kwa wale ambao bado hawajaingia.”  Martha Newton, Naibu Mkurugenzi wa ILO- Sera Kuu

Tofauti za kikanda

Kwa nchi za kipato cha chini na cha kati ajira kwa vijana kurejea katika hali kabla ya COVID-19 bado ni changamoto, inasema ripoti ikiweka bayana kuwa ni nchi za kipato cha juu pekee ambazo “zinatarajiwa kupunguza kiwango cha ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana na kukaribia kiwango cha mwaka 2019 ifikapo mwishoni mwa mwaka huu wa 2022.”

Barani Afrika, kiwango cha ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana cha asilimia 12.7 kinaficha suala kwamba vijana wengi wamechagua kutoingia kwenye soko la ajira kabisa.

“Mwaka 2020, zaidi ya kijana 1 kati ya 5 barani Afrika hakuwa ameajiriwa, hakuna na elimu wala mafunzo, (NEET) na hali inazidi kuwa mbaya,” imesema ripoti hiyo.

Kwa nchi za kiarabu, kiwango cha ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana kinaua kwa kasi na kinatarajiwa kufikia asilimia 24.8 mwishoni mwa mwaka huu.

Fursa za kunusuru vijana

Vijana wa kike na wa kiume watanufaika na kupanuliwa kwa uwekezaji kwenye shughuli za uchumi wa buluu, au shughuli za matumizi endelevu ya rasilimali ya bahari.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, nyongeza ya ajira milioni 8.4 inaweza kupatikana kwa vijana ifikapo mwaka 2030 kupitia utekelezaji wa sera bora za shughuli za kiuchumi zisizoharibu mazingira na zinazotumia rasilimali za bahari.

Halikadhalika uwekezeji kwenye teknolojia za kidijitali na huduma za malezi kwenye sekta ya elimu na afya.

Uwekezaji kwenye sekta ya elimu na afya utanufaisha vijana katika maeneo makuu manne: kuimarisha matarajio ya ajira kwa vijana; itakuwa rahisi kwa vijana wa kike na kiume wenye familia kusalia kwenye ajira; itasongesha ustawi wa vijana kwa kupanua fursa ya elimu na mafunzo na kujali afya ya vijana.

Ripoti inasema kwa kutekeleza hilo idadi ya vijana wasio na ajira, elimu au mafunzo, itapungua, na vile vile ajira ambazo watakuwa wanafanya vijana zitakuwa ni za utu.