Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mongolia isiyo na nyuklia ni ishara ya amani katika ulimwengu wenye matatizo: Guterres

Katibu Mkuu António Guterres akisalimiana na walinda amani wa Mongolia ambao wana mchango mkubwa zaidi kwa kila mwananchi katika operesheni za ulinzi wa amani.
UN Mongolia/Rentsendorj Bazarsuk
Katibu Mkuu António Guterres akisalimiana na walinda amani wa Mongolia ambao wana mchango mkubwa zaidi kwa kila mwananchi katika operesheni za ulinzi wa amani.

Mongolia isiyo na nyuklia ni ishara ya amani katika ulimwengu wenye matatizo: Guterres

Tabianchi na mazingira

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa yupo ziarani nchini Mongolia ambapo hapo jana alieleza mshikamano wa Umoja wa Mataifa na nchi hiyo kuwa ni ishara ya amani katika ulimwengu wenye matatizo

Guterres alikuwa alizungumza hayo katika mkutano na waandishi wa habari katika mji mkuu, Ulaanbaatar, kufuatia mkutano wake na Waziri wa Mambo ya Nje, Battsetseg Batmunkh.

Alisema kuwa katika ulimwengu ulio na mgawanyiko mkubwa wa kijiografia na kisiasa, na ambapo mizozo inaenea kila mahali, nchi ya Mongolia kama eneo lisilo na silaha za nyuklia ni mfano kwa nchi zingine kufuata.

Hakuna tena silaha za nyuklia

“Tunaishi katika ulimwengu ambao kwa mara ya kwanza baada ya miongo kadhaa watu wanafikiri kwamba vita vya nyuklia vinaweza kutokea tena,” alisema mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa.

"Kuna njia moja tu ya kuwa na uhakika kabisa kwamba vita vya nyuklia haiwezekani, na njia hiyo ni ikiwa hakuna silaha za nyuklia."

Mongolia ni kituo cha hivi punde zaidi katika ziara ya Katibu Mkuu Barani Asia, iliyoanza nchini Japan siku ya Ijumaa.

Katibu Mkuu António Guterres katika hafla ya upandaji miti iliyohudhuriwa na Rais Khurelsukh Ukhnaa wa Mongolia.
UN Mongolia/Rentsendorj Bazarsuk
Katibu Mkuu António Guterres katika hafla ya upandaji miti iliyohudhuriwa na Rais Khurelsukh Ukhnaa wa Mongolia.

Pongezi kwa walinda amani

Katika miongo sita iliyopita, nchi hiyo imekuwa mchangiaji muhimu zaidi katika kazi za UN, alisema.

Guterres alitoa shukrani kwa walinda amani wa Mongolia wanaohudumu katika operesheni za amani za Umoja wa Mataifa, "mara nyingi katika mazingira yenye changamoto nyingi na kwa ujasiri katika jinsi wanavyolinda raia ambapo kwa bahati mbaya, wakati mwingine hakuna amani ya kuweka".

Katibu Mkuu alikutana na Rais wa Mongolia, Khurelsukh Ukhnaa, na maafisa wengine wakuu, mapema Jumanne ambapo walijadili hali ya kisiasa ya kijiografia katika eneo hilo, changamoto zinazoikabili nchi hiyo ikiwa ni nchi isiyo na bahari, na juhudi za kitaifa za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Katibu Mkuu António Guterres akutana na jamii za watu wanaohamahama wa Mongolia.
UN Mongolia/Erdenetuya Gurrenchin
Katibu Mkuu António Guterres akutana na jamii za watu wanaohamahama wa Mongolia.

Fanya amani na uoto wa asili

Kuhusiana na masuala ya utunzaji wa uoto wa asili Katibu Mkuu Guterres aliungana na vijana na walinda amani katika sherehe ya upandaji miti, ikiwa ni sehemu ya kampeni ya Mongolia ya kupanda miti Bilioni Moja kushughulikia mabadiliko ya tabianchi na kuenea kwa jangwa.

“Kizazi changu kilikuwa kijinga sana. Kizazi changu kilitangaza vita dhidi ya asili na mabadiliko ya tabianchi na kupotea kwa bayoanuwai, pamoja na uchafuzi wa mazingira," alisema.

Alisisitiza jinsi "asili inavyorudi nyuma" na dhoruba, jangwa, mafuriko na majanga, ambayo yanafanya maisha kuwa magumu sana kwa watu wengi ulimwenguni na kusababisha waathirika kuwa wengi.

"Kizazi chenu kina kazi muhimu ya kufanya amani na uoto wa asili," alisema. "Na kile tunachoenda kufanya leo, lazima iwe ishara ya mtazamo huo mpya wa kufanya amani na asili."

Katibu Mkuu pia alitembelea familia ya kuhamahama nchini Mongolia na kujifunza kuhusu maisha yao.

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa katika ziara yake alikutana na kundi la walengwa kutoka kwa miradi ya Umoja wa Mataifa, wakiwemo wafanyabiashara wanawake na wanaharakati wa vijana.