UN yapongeza kuongezwa kwa kipindi cha mpito Sudan Kusini

10 Agosti 2022

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Sudan Kusini, UNMISS umekaribisha tangazo la tarehe 4 mwezi huu wa Agosti la makubaliano kati ya pande za mkataba wa amani ulioboreshwa wa tarehe 12 mwezi Septemba mwaka 2018 wa kuongeza kipindi cha sasa cha mpito kwa miezi mingine 24. 

Taarifa ya UNMISS iliyotolewa leo Juba, mji mkuu wa Sudan Kusini imesema kitendo cha kuongeza muda wa serikali ya mpito kitatoa fursa ya utekelezaji wa majukumu yaliyosalia kwa mujibu wa mkataba huo mpya wa makubaliano. 

UNMISS imepongeza serikali ya Sudan Kusini kwa kufanikisha makubaliano hayo na pande zote zilizotia saini makubaliano hayo huku ikisihi mamlaka ziongeze juhudi zaidi kuleta wadau wengine wengi zaidi, wadhamini na mashuhuda. 

Ujumbe huo pia umesihi pande husika na wote waliotia saini kushirikiana kwa njia ya kasi zaidi ili kufanikisha utekelezaji wa vipengele vyote vilivyosalia, na kuhakiksha kuna mazingira rafiki ya kuwezesha uchaguzi huru, haki na halali mwishoni mwa kipindi cha mpito. 

Kwa upande wake UNMISS imesema inasalia imejizatiti kusaidia mchakato jumuishi wa kidemokrasia na inaendelea na mshikamano na wananchi wa Sudan Kusini katika kusaka amani ya kudumu, utulivu na maendeleo. 

Mkataba wa amani ulioboreshwa 

Mkataba wa amani wa Sudan Kusini ulioboreshwa, R- ARCSS ulitiwa saini tarehe 12 mwezi Septemba mwaka 2018 huko Addis Ababa nchini Ethiopia baada ya miezi 15 ya mashauriano kufuatia kuvunjika kwa msururu wa mikataba ya kusitisha mapigano yaliyozuka nchini Sudan Kusini mwezi disemba mwaka 2013. 

Mkataba huo pamoja na mambo mengine ulitaka kuweko kwa serikali ya Umoja wa Kitaifa ya mpito, ambayo iko hivi sasa na inaongozwa na RAis Salva Kiir pamoja na makamu wengine wa Rais. Halikadhalika kupangwa upya kwa majimbo hatua ambazo pia zimefanyika. 

Kuhusu uchaguzi mkuu, unatakiwa ufanyike siku 60 baada ya kuvunjwa kwa serikali ya Umoja wa Kitaifa ya mpito na ulikuwa ufanyike mwezi Desemba mwaka huu wa 2022 na sasa vyombo vya habari vinaripoti kuwa kutokana na mabadiliko haya, uchaguzi utafanyika tarehe 20 Desemba mwaka 2024. 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter