Mashine za kusaidia watoto kupumua zapelekwa Ukraine; ni ubunifu kutoka Kenya

Mtoto Alex akiw akwenye mashine ya kumsaidia kupata hewa ya oksijeni katika kituo cha watoto wachanga, Ukraine.
Vayu Global Health/Unitaid
Mtoto Alex akiw akwenye mashine ya kumsaidia kupata hewa ya oksijeni katika kituo cha watoto wachanga, Ukraine.

Mashine za kusaidia watoto kupumua zapelekwa Ukraine; ni ubunifu kutoka Kenya

Afya

Mashine 220 za kusaidia watoto wachanga kupata hewa ya oksijeni kutokana na kuwa hatarini kufariki dunia baada ya kuzaliwa ambazo zimetengenezwa nchini Kenya kwa msaada wa shirika la Umoja wa MAtaifa la kufanikisha upatikanaji wa dawa na tiba kwa gharama nafuu UNITAID zimepelekwa nchini Ukraine wakati huu ambapo vita vinakwamisha huduma za uzazi na kujifungua. 

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva ,Uswisi hii leo, msemaji wa UNITAID Herve Verhoosel amesema tangu kuanza kwa vita nchini Ukraine huduma za afya zimesambaratishwa na vita inaongeza msongo kwa wanawawake wajawazito na sasa kuna ripoti za ongezeko la kuzaliwa kwa watoto njiti.

Amesema watoto njiti wako hatarini kupata magonjwa ya njia ya hewa na mfumo wa fahamu iwapo watakosa hewa ya oksijeni na ndio maana, “shukrani kwa msaada wa UNITAID, Vayu Global Health, shirika linalobuni mbinu za gharama nafuu, linatoa mashine 220 za kusaidia kupumua na mifumo mingine 125 ya kusambaza oksijeni kwa watoto wachanga wenye shida ya kupumua. Mashine na mifumo hiyo inazuia mtoto kuharibikiwa macho, mapafu na ubongo kwa sababu anapatiwa hewa safi ya oksijeni.”

Bwana Verhoosel ameesma mashine hizo ambazo hazihitaji umeme na zinabebeka kwa urahisi zilishapitishwa kwa matumizi ya dharura nchini Marekani wakatai wa janga la COVID-19 na zitaleta mabadiliko makubwa hasa kwenye maeneo yenye changamoto.

Amefafanua kuwa, “fedha kutoka UNITAID zimesaidia kukamilisha mfumo wake wa kiuhandisi, na kuidhinishwa nchini Marekani. Mfumo huu unatengenezwa nchini Kenya. Na UNITAID ndio imefadhili mashine hizi kupelekwa Ukraine.”

Kwa mujibu wa Bwana Verhoosel, mbinu hii ya dharura kutoka Vayu Global Health inatumika pia katika nchi kadhaa za Afrika lakini pia Ubelgiji, na MArekani lakini fedha zaidi zitahitaijka kuzitengeneza kwa wingi zaidi.