Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Msaada wa kisaikolojia nchini Gambia unasaidia watu waliofurushwa - IOM

Mwanasaikolojia wa kujitolea Amie akifanya kikao cha ushauri nasaha moja kwa moja na Kaddy, mwanamke wa Senegal ambaye alikimbilia Gambia.
Picha: IOM/Robert Kovacs
Mwanasaikolojia wa kujitolea Amie akifanya kikao cha ushauri nasaha moja kwa moja na Kaddy, mwanamke wa Senegal ambaye alikimbilia Gambia.

Msaada wa kisaikolojia nchini Gambia unasaidia watu waliofurushwa - IOM

Wahamiaji na Wakimbizi

Mgogoro ulipozuka katika kijiji cha Kaddy mapema Aprili mwaka huu, alilazimika kuacha kila kitu ili kuokoa familia yake. Makala hii iliyoandikwa na Robert Kovacs, Mshauri wa IOM katika Kuripoti na Mawasiliano nchini Gambia na kutafsiriwa na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa inaeleza namna msaada wa kisaikolojia ulivyo muhimu kwa watu wanaokimbia mizozo. 

"Tulipoteza kila kitu, tulipoteza wanyama wetu, tulipoteza chakula chetu. Tulipoondoka, hatukuweza kuchukua chochote pamoja nasi. Kila kitu kilichoachwa nyuma kimeharibiwa kutokana na mapigano nchini Senegal.” Anaeleza Kaddy. 

Pamoja na mume wake na watoto saba, Kaddy alikimbilia kaskazini mwa Gambia, hatimaye akapata njia ya kwenda kwenye kijiji kidogo katika wilaya ya Janack, katika eneo linalojulikana kama 'Foni'. 

Wakiwa wameondoka bila chochote, Kaddy na familia yake walilazimika kutegemea ukarimu wa jamii ya eneo hilo kwa chakula na makazi. "Tunahisi kama mzigo kwa jumuiya zingine zinazotusaidia." Kaddy anasikitika akiongeza kusema, "tunajisikia aibu 'kutunzwa', lakini hatuna chaguo." 

Kaddy yuko Gambia kwa mujibu wa Shirika la Kitaifa la Kukabiliana na Majanga la nchi hiyo, baada ya mapigano kuzuka mwezi Januari katika mpaka wa Gambia na Senegal katika maeneo yanayokaliwa na vuguvugu la wanaotaka kujitenga la Movement of Democratic Forces of Casamance (MFDC). Raia wengine 6,200 wa Gambia wamekimbia makazi yao, huku wengine 8,500 wakiathirika katika jumuiya zinazowapokea – kwa mujibu na Shirika la Kitaifa la Kukabiliana na Majanga la Gambia - kutokana na mzozo ulioanza kwa miongo minne nyuma. 

Kwa kutambua athari kubwa ya mzozo huo kwa ustawi wa watu waliofurushwa katika makazi yao, Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na Uhamiaji (IOM) limekusanya utaalamu wake katika kutoa msaada wa afya ya akili na kisaikolojia (MHPSS). Kwa ushirikiano na ‘Wakfu wa Wanaharakati Wanaosaidia’ Supportive Activists Foundation (SAF), IOM ilituma timu ya simu ya mkononi ya wanasaikolojia - inayojumuisha mwanasaikolojia, wafanyakazi wawili wa ustawi wa jamii, mwalimu na mhamasishaji wa jamii ambao wnatoa huduma za moja kwa moja kwa watu walioathirika. 

Mbinu moja kuu inayotumiwa na timu ya watu wanaotembea eneo moja hadi jingine ni elimu ya kisaikolojia, ambapo watu waliojitolea hukutana na kushirikisha jamii ili kujadili masuala ya afya ya akili na dalili na pia dalili zinazowezekana za mfadhaiko. "Madhumuni ni kuongeza ufahamu kuhusu uzoefu wa watu ambao wamepitia dhiki baada ya kiwewe au wameathirika vibaya kutokana na mabadiliko ya mazingira yaliyoletwa na mgogoro," anasema Solomon Correa, Mkurugenzi Mkuu wa SAF. 

Vikao hivi, vinavyoendeshwa kwa makundi, vinaboresha shughuli za kitamaduni na, kama vile vikao vya kawaida vya attaya (chai), ili kuwezesha majadiliano. 

“Wakati wa mazungumzo tunaweza kuwafundisha mbinu za kukabiliana na hali,” asema Amie, mwanasaikolojia wa kujitolea na anaongeza akisema kuwa, "baada ya kuwaelekeza juu ya dalili na dalili zinazowezekana za matatizo ya afya ya akili, mara nyingi hupenda sana kuzungumza nasi faraghani." 

Kupitia vipindi vya elimu ya kisaikolojia, timu inaweza kutambua watu walio na mahitaji maalum ya afya ya akili ambayo yanahitaji uangalizi zaidi na kufanya ziara za ufuatiliaji au rufaa, inapohitajika. 

Fatou ni mmoja kati ya wengi walionufaika na vikao vya kujitolea vya ana kwa ana. 

Mwananchi wa Gambia hapo awali akiwa Casamance na mume wake wa Senegal, familia yake yote ilikimbia mzozo ulipozuka. Fatou aliondoka nyumbani kwake ghafla na hakuwa na muda wa kukusanya mali yoyote, kwani alikuwa akijishughulisha na kuwahamisha salama watoto wake 10 ambao mmoja wao ni mlemavu wa viungo. Kwa zaidi ya miezi miwili, amekuwa akiishi katika boma la mjomba wake huko Janack. 

Fatou ameamua kufanya kazi ndogo ndogo za kila siku, ikiwa ni pamoja na kufanya vibarua katika mashamba wakati wa kuuza mazao kwa niaba ya wakulima ili kujikimu. Hata hivyo, mkazo wa kuandalia familia yake katika mazingira mapya, pamoja na kumbukumbu zenye uchungu zilizoibuka tena kutokana na kupigwa risasi alizoshuhudia, zimekuwa na athari mbaya kwa ustawi wake wa kiakili. 

"Hadi sasa, hili ni mojawapo ya mambo yanayonisaidia sana katika maisha yangu ya kila siku," Fatou anasema kuhusu usaidizi wa kisaikolojia ambao amepokea. "Nina furaha sana kuzungumza nao timu ya watu hawa wanaotembea hap ana pale na kushiriki hisia na shida zangu bila kusita." Vipindi vya Fatou na timu ya wataalamu hao wa saikolojia vimemsaidia kumpa hisia ya mshikamano na wengine ambao wamefurushwa: "Inanisaidia kujua kwamba hatuko peke yetu katika hili." 

Miezi kadhaa baada ya kuzuka kwa mzozo, inaonekana hakuna mwisho mbele. "Hatuna uhakika kama ni sawa kwetu kurudi au la. Kwa sasa, hatuna fununu.” Fatou anasema. 

Licha ya kutokuwa na uhakika wa siku zijazo, msaada wa kisaikolojia unaotolewa unasaidia walioathirika zaidi kukabiliana na mabadiliko makubw. Kama vile Kaddy anavyoshiriki, “Kuweza tu kuzungumza na mtu peke yake kuhusu matatizo yetu katika mzozo huu hututia moyo sana. Inatusaidia kujisikia vizuri zaidi ingawa hakuna uhakika kuhusu wakati ujao.” 

"Bada ya kushiriki katika vikao hivi, nimepunguza kuwa na wasiwasi." Fatou anakubaliana na Kaddy. 

Katika ulimwengu ambapo afya ya akili mara nyingi huwekwa kwenye kiti cha nyuma, kazi ya timu ya wanasaikolojia sita wanaohamahama inaonesha manufaa yanayopatikana wakati afya ya akili inapewa kipaumbele. 

Written by Robert Kovacs, IOM Reporting and Communications Consultant in The Gambia