Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNFPA yaomba msaada wa dola mil 10.7 kusaidia wanawake na wasichana wa Sri Lanka

Wanawake wakijifunza darasani, katika kijiji kimoja huko Sri Lanka.
World Bank/Lakshman Nadaraja
Wanawake wakijifunza darasani, katika kijiji kimoja huko Sri Lanka.

UNFPA yaomba msaada wa dola mil 10.7 kusaidia wanawake na wasichana wa Sri Lanka

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu na afya ya uzazi UNFPA, limetoa ombi la dola milioni 10.7 kwa ajili ya kutoa usaidizi wa kuokoa maisha kwa wanawake na wasichana zaidi ya milioni mbili nchini Sri Lanka. 

Taarifa iliyotolewa leo na shirika hilo kutoka New York Marekani imesema kiasi hicho cha fedha kitaliwezesha shirika hilo kwa miezi sita kusaidia kundi hilo lililo katika hali mbaya katika kipindi hiki ambacho nchi hyo inakabiliwa na hali mbaya ya kiuchumi na kijamii tangu kupata uhuru wake hali iliyoathiri mifumo ya huduma ikiwemo ya afya. 

Mkurugenzi Mtendaji wa UNFPA Dkt. Natalie Kanem amesema utafiti wa Umoja wa Mataifa ulifanyika mwezi Mei mwaka huu 2022 unaonesa uwezekano wa wanawake na wasichana kukabiliwa na ukatili unaoongezeka wakati huduma ambao huduma ikiwa ni pamoja na za afya, polisi, simu za dharura na Makazi zimepungua kutokana na ukosefu wa rasilimali za kifedha.

“Mgogoro wa sasa wa kiuchumi nchini Sri Lanka una madhara makubwa kwa afya ya wanawake na wasichana, haki na utu. Kwa sasa kipaumbele chetu (UNFPA) nikupata majibu ya mahitaji waliyonayo ya kipekee ili kuwalinda na kuwafikia kwa kuwapatia huduma za afya na ulinzi wa kuokoa Maisha yao.” Amesema Dkt. Kanem

Juhudi zilizofanyika kwa miaka mingi zimesaidia kuweka uthabiti wa huduma kwa wanawake na wasichana nchini humo ambao inaelezwa asilimia 99 ya wanawake hujifungulia katika vituo vya afya lakini mafanikio kama haya sasa yapo mashakani.

Kwa zaidi ya miaka 50 UNFPA imekuwa ikifanya kazi na kundi hilo katika jamii, juhudi ambazo zimeleta faida thabiti kwa wanawake na wasichana wa Sri Lanka, moja kuu ni asilimia 99 ya wanawake hujifungulia katika vituo vya afya, wakisaidiwa na wafanyakazi wa afya, lakini mafanikio haya sasa yako chini ya tishio.

Nchini Sri Lanka Minabige, 49, anaishi na mumewe na binti yake katika kibanda kidogo cha chumba kimoja ambapo wanakula, kupika, kusali, kusoma na kulala kikiwa inchi chache kutoka kwa bomba la maji taka.
© WFP/Josh Estey
Nchini Sri Lanka Minabige, 49, anaishi na mumewe na binti yake katika kibanda kidogo cha chumba kimoja ambapo wanakula, kupika, kusali, kusoma na kulala kikiwa inchi chache kutoka kwa bomba la maji taka.

UNFPA wamesema inakadiriwa wanawake 215,000 kwa sasa ni wajawazito, wakiwemo wasichana 11,000 na karibu wanawake 145,000 watajifungua katika miezi sita ijayo.

Takriban wanawake 60,000 wanaweza kuhitaji huduma ya upasuaji na hii ndio sababu wanahitaji fedha hizo ili waweze kutoa si tu msaada wa fedha taslimu bali pia a vocha kwa wanawake wajawazito ili ziweze kusaidia upatikana ji wa huduma katika vituo vya afya , kutatua changamoto za miundombinu na usafiri.

“UNFPA imejitolea kuhakikisha tunakidhi mahitaji muhimu ya afya na ulinzi wa wanawake na wasichana. Lengo letu ni kuimarisha afya ya ngono, uzazi na huduma za kukabiliana na unyanyasaji wa kijinsia ili kupunguza aahri za muda mrefu za mgogo wa sasa.” Ameeleza Mkuu huyo wa UNFPA

Matumizi zaidi ya kumi yameainishwa kutekelezwa iwapo fedha hizo zitapatikana ambayo ni pamoja na;- 
•    Usambazaji wa vifaa na vifaa tiba kwa ajili ya kujifungulia na huduma za upasuaji, 
•    Kutoa fedha na vocha kwa wanawake ili waweze kuzifikia huduma za afya, 
•    Kutoa elimu na taarifa za dalili za hatari kwa wanawake wanapokuwa wajawazito, 
•    Kuwajengea uwezo wakunga katika vituo vya kujifungulia na vituo maalum vyakusaidia watu waliobakwa, 
•    Kutoa huduma ya malazi kwa waaathirika wa ukatili wa kijinsia na kingono, 
•    Kutoa elimu kwa barubaru juu ya afya ya hedhi na kuwapatia vifaa 
•    Kuongoza na kuratibu shughuli za kuimarisha mifumo ya kinga, ulinzi na rufaa kwa waathirika wa ukatili wa kijinsia.

Ombi hili la UNFPA la mil 10.7 ni kati ya ombi kuu la dola milioni 47 lililotolewa na Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kusaidia katika misaada ya kibinadamu kati ya mwezi Juni na Septemba mwaka huu 2022.